Home » » SERIKALI YA TANZANIA YAIONYA MALAWI

SERIKALI YA TANZANIA YAIONYA MALAWI

Na Maregesi Paul, Dodoma
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ameionya Serikali ya Malawi juu ya utata wa mpaka uliopo katika Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na nchi hiyo.

Alisema kuanzia sasa, Serikali ya Malawi hairuhusiwi kutumia eneo la mpaka unaogombaniwa hadi hapo mwafaka utakapopatikana.

Waziri Membe, alitoa onyo hilo bungeni jana, alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2012/2013.

“Mheshimiwa Spika, nimezungumza mengi na sasa ngoja nizungumzie suala la mpaka kati ya Tanzania na Malawi kwenye Ziwa Nyasa.

“Lipo tatizo la muda mrefu kati yetu na nchi jirani ya Malawi linalohusiana na mpaka kwenye Ziwa Nyasa, ambapo Malawi wanadai Ziwa lote Kaskazini ya Msumbiji kuelekea Ruvuma na Mbeya ni mali yao kwa mujibu wa Mkataba wa Heligoland uliowekwa saini Julai mwaka 1890.

“Tanzania kwa upande wetu, tunadai kwamba mpaka kati yetu na Malawi na Ziwa Nyasa unapita katikati ya ziwa hilo pale ambapo Malawi na Msumbiji wanapopakana usawa wa nyuzi 11 kusini hadi mwisho wa ziwa kule Kyela, usawa wa nyuzi 9 Kaskazini ya ziwa.

“Msingi wa madai yetu hayo ni kwamba, kwa mujibu wa nyaraka na ramani zilizotengenezwa na wakoloni wetu Waingereza mwaka 1928, 1937 na 1939, zinaonyesha kuwa mpaka wa ziwa hilo upo katikati.

“Aidha mkataba huo, unaotumiwa kama msingi wa madai yao, unabainisha katika ibara ya sita, kwamba nchi zinazohusika yaani Tanganyika na Nyasaland (Tanzania na Malawi sasa), zikutane ili kurekebisha kasoro kwa kadiri mazingira yatakavyolazimu.

“Jambo hilo siyo jipya, kwani tumekwishafanya zoezi hili katika mpaka wa bahari kati yetu na Comoro na Msumbiji Desemba 5, 2011 na Februari 17 kati ya Tanzania na Shelisheli. Hapo tulikaa, tukajadili na tumerekebisha mpaka wetu kule baharini kati ya Tanzania na Shelisheli.

“Katika utata wa mpaka wetu na Malawi, madai yetu Tanzania yanakuwa na nguvu zaidi tunapolinganisha kesi kama hii na iliyotokea kati ya Cameroon na Nigeria kuhusu mpaka wao kwenye Ziwa Chad lililopo katikati ya nchi hizo.

“Kesi ya ziwa hilo, ilipelekwa kwenye Mahakama ya Dunia na iliamriwa mpaka huo, upite katikati ya ziwa hilo katika mstari ulionyooka hadi mdomo wa Mto Ebeji na sheria hizo zinaeleza kuwa mstari ulionyooka ndiyo mpaka kati ya nchi hizo zinazopakana na ziwa.

“Hivyo, kutokana na maelezo hayo yote ni dhahiri kwamba, tunalo tatizo la kutatuliwa na tatizo hili ni la muda mrefu tangu miaka ya 1960 na 90 na suala hili lisingeweza kutatuliwa mara moja kwa sababu kuu mbili.

“Moja, kiongozi wa wakati huo, Dk. Kamuzu Banda alikuwa rafiki wa serikali ya makaburu wa Afrika Kusini, wakati sisi tulikuwa marafiki wa wapigania ukombozi, ikiwemo ANC ya Afrika Kusini.

“Pili, kutokana na Tanzania kuwa makao makuu ya vyama vya ukombozi na hivyo kufanya wapinzani wa Serikali ya Malawi kukimbilia Tanzania, hivyo kumfanya kiongozi wa Malawi kuamini Tanzania kilikuwa kichaka cha maadui dhidi ya Serikali ya Malawi.

“Baada ya utawala wa Banda (Kamuzu Banda, Rais wa zamani wa Malawi) kumalizika na kuingia madarakani Bakili Muluzi, Bingu wa Mutharika na sasa Joyce Banda, uhusiano ukaanza kuwa mzuri na kukaribisha mazingira mazuri ya kulijadili suala hilo.

“Mwaka 2005, Rais Mutharika aliwahi kumuandikia barua Rais Mkapa kumuomba iundwe kamati ya pamoja ya wataalamu ili kuchambua, kushauri na kutatua tatizo la mpaka kati ya nchi hizo mbili,” alisema Waziri Membe na kuongeza:

“Kwa kuwa mwaka huo ulikuwa ni kipindi cha uchaguzi wa Tanzania, Rais Mkapa alikuwa anaondoka na alimuachia madaraka Rais Kikwete ambaye naye alikutana na Mutharika mara mbili katika mikutano ya AU, Addis Ababa na walikubaliana ziundwe timu za wataalamu chini ya mawaziri wa mambo ya nchi za nje.

“Timu iliundwa na kuanza kukutana mwaka 2010 kwa kutengeneza hadidu za rejea ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa suala hilo. Wakati kamati hizi zinakutana, eneo hilo la mpaka likaanza kuchukua sura mpya ambapo liliashiria kuhatarisha usalama, kwani Serikali yetu ilipata habari za kuaminika kwamba, Malawi imetoa vitalu vya eneo la Kaskazini kwa kampuni ya utafiti wa gesi

“Aidha, makampuni hayo yaliomba kibali cha kufanya utatifi wa gesi katika ziwa hilo, ombi ambalo lilikataliwa na JWTZ na pia Serikali yetu ilipata ushahidi, kuwa kulikuwa na ndege zenye uwezo wa kutua majini na ufukweni zinazokadiriwa kuwa tano ambazo zilionekana zikivinjari na kutua katika Ziwa Nyasa upande wa Tanzania na kwenye ufukwe wa ziwa hilo, Januari 29 na Julai 2 mwaka huu.

“Serikali yetu, iliwasiliana na Serikali ya Malawi kwa maandishi tukiomba tufanye mkutano wa mawaziri kujadili mustakabali wa mpaka huu na hali ilivyo ambapo mkutano ulifanyika Julai 27 na 28 mwaka huu jijini Dar es Salaam na mambo matatu yakatokea.

“Kwanza pande zote mbili zilikiri lipo tatizo, pili Serikali hizi mbili zilikubaliana kwamba, Agosti 20 hadi 22, mwaka huu, wakutane mawaziri na wataalamu Mjini Mzuzu na tatu Serikali ya Tanzania iliitaka Malawi kutoruhusu kampuni yoyote kuendelea na shughuli za utafiti katika ziwa hilo.

“Mheshimiwa Spika, naomba niseme Serikali ya Tanzania inathamini uhusiano mzuri uliopo kati ya yetu na Malawi na tuna dhamira ya kudumisha ujirani mwema kwa manufaa ya watu wetu.

“Kwa hiyo, napenda kuitaka Serikali ya Malawi, iheshimu makubaliano yetu ya Julai 27 mwaka huu, njia nzuri na bora ya kutatua tatizo hili lililopo mbele yetu ni la mazungumzo ya amani na kuanzia sasa Serikali ya Malawi isiruhusu mtu yeyote au kampuni yoyote kufanya utafiti katika eneo la Ziwa Nyasa, lililopo Kaskazini mwa ziwa hilo,” alisema Waziri Membe.

Kwa mujibu wa waziri huyo, Ziwa Nyasa ni muhimu kwa maisha ya Watanzania wa mikoa ya kusini, kwa kuwa wamekuwa wakilitumia kwa shughuli zao za kila siku.

“Nasema hivyo kwa sababu Ziwa Nyasa ni muhimu kwa maisha ya wananchi wa eneo hilo takribani 600,000 na ziwa hilo ni urithi wao, ziwa hilo ni chanzo cha uzima wao na maendeleo yao na kwa vyovyote vile, Serikali yetu inayo dhamana ya kuwalinda watu wetu.

Wakati huo huo, Mbunge wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa (CUF), Mbunge wa Viti Maalum, Stela Manyanya (CCM) na Mbunge wa Viti Maalum, Hilda Ngoye (CCM), walitaka kwa nyakati tofauti, busara itumike ili kutatua mgogoro huo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa