Home » » VETA KUANZA KUUNDA MAGARI

VETA KUANZA KUUNDA MAGARI

na Mwandishi wetu, Dodoma
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), inatarajia kuanza kuunda magari.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Mkurugenzi wa Utumishi na Utawala wa VETA, Aloyce Shayo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho na Nanenane yaliyohitimishwa juzi kitaifa katika viwanja vya Nzuguni mjini hapa.
“VETA ni kimbilio la watu wengi ingawa tuna changamoto kubwa; kwamba mahitaji ya wananchi ni mengi lakini kwa bahati mbaya hatuna uwezo wa kupokea vijana wengi zaidi katika vyuo vyetu.
“Kwa kuwa tuna lengo la kujiimarisha zaidi, tunatarajia kuanzisha kozi ya ufundi wa umeme na mitambo ambayo itatuwezesha kuunda magari na roboti hapa nchini kwani uwezo wa kuunda vitu hivyo tunao.
“Utaratibu huu tunatarajia kuufanikisha kwa kushirikiana na viwanda mbalimbali kama vile Toyota, Nissan na vinginevyo kwani bila kufanya hivyo nadhani hatutafanikiwa zaidi,” alisema Shayo.
Akizungumzia maonesho hayo, alisema VETA imekuwa ya kwanza na kupewa tuzo ya ngao na cheti kutokana na ushindi huo.
“Katika kundi letu tunapambana na vyuo vikuu na taasisi zote nchini zinazofanya utafiti, sasa mnaweza kuona kwamba mchuano si rahisi, hapa tuna ushindani mkubwa lakini wote hao wanakuwa nyuma yetu,” alisema.
Katika hatua nyingine, alisema kuanzia mwaka kesho, VETA itaanzisha kozi ya stashahada ya mawasiliano ya kompyuta kwani kozi hiyo ni muhimu kwa maendeleo ya taifa.
“Dunia imebadilika kwa sababu kila kitu sasa kinakwenda kwa mitandao na kwa kulijua hilo, na sisi tunajipanga kuanzisha diploma ya ICT ili taifa liwe na watalaam wanaokwenda na wakati kama zilivyo nchi zilizoendelea,” alisema.

Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa