Home » » CHAVITA DODOMA WAKOSA OFISI

CHAVITA DODOMA WAKOSA OFISI

Na Debora Sanja, Dodoma
CHAMA cha Viziwi Wilaya ya Dodoma Mjini (CHAVITA) kimedai kuendeshea shughuli zake chini ya mti kutokana na kukosa ofisi. Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Mratibu wa Mradi wa Mafunzo ya Lugha ya Alama Wilaya ya Dodoma Mjini, Ramadhani Kimolo, wakati wa mafunzo ya lugha ya alama.

Alisema chama hicho kimeamua kutoa malalamiko yao baada ya kutuma maombi yao katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Manispaa ya Dodoma, kuomba ofisi lakini hawajajibiwa hadi leo.

“Kutokana na hali hii muda mrefu tumekuwa tukiendesha shughuli zetu chini ya miti na maeneo ambayo si rasmi.

“Chama chetu kinalazimika kukutana na kufanya shughuli katika Uwanja wa Nyerere, nyumbani kwa mmoja wetu wa wanachama au katika ofisi ya CHAVITA Mkoa.

“Ukosefu wa ofisi ya kudumu umekuwa pia ukisababisha upotevu wa nyaraka za kiofisi ambazo mara nyingi tumekuwa tukizihifadhi nyumbani, wakati mwingine huliwa na wadudu kama vile panya na mchwa,” alisema Kimolo.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Dodoma Mjini, Kondokaya Kikwesa, alisema Serikali inatambua vyama vyote vina umuhimu wake kikiwamo chama cha viziwi.

“Tatizo lililopo ni upatikanaji wa vyumba vya ofisi ambapo hata hivyo ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Manispaa inashughulikia suala hilo kwa ajili ya kuwaondolea kero hiyo ya muda mrefu ya kukosa ofisi ya kudumu,” alisema Kikwesa.

Aliziomba taasisi kujitokeza kusaidia jamii za watu wenye ulemavu wakiwamo viziwi, kuwapatia mahitaji mbalimbali kama vile elimu, afya, majengo, chakula, usafiri na vitendea kazi.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa