Home » » MIILI YA WATU YASITISHA UJENZI WA BARABARA

MIILI YA WATU YASITISHA UJENZI WA BARABARA

Na Debora Sanja, Dodoma
UJENZI wa barabara na uchimbaji wa mitaro ya maji katika eneo la uwekezaji la Njedengwa katika Manispaa ya Dodoma, umesitishwa kwa muda usiojulikana kutokana na kubaini kuwapo kwa miili ya watu katika eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, mradi huo umesimamishwa kwa ajili ya kupisha shughuli za utambuzi wa makaburi yaliyopo katika eneo hilo.

Kauli hiyo ilitolewa na mshauri katika mradi huo, Samweli Mtawa, alisema hatua hiyo imefikiwa baada ya mifupa ya binadamu kuonekana imetapakaa katika eneo hilo, hali iliyosababisha ndugu wa marehemu kulalamika kuwa wanataka kuhifadhi mifupa ya ndugu zao katika hali ya usalama zaidi.

Alisema awali wakati wa kufanya tathimini katika mradi huo walitaka kuyatambua makaburi yote yaliyopo katika mradi huo wayahamishe, lakini ndugu wa marehemu hao walionekana kuyasahau mahali yalipo makaburi hayo.

“Hali hiyo ilisababisha kazi kuendelea bila kujua sehemu ambapo makaburi yalikuwapo.

“Wakati kazi ikiwa inaendelea ndipo tukaanza kukuta mifupa ya binadamu imetapakaa katika eneo hilo na ndipo walipofikia uamuzi wa kusitisha shughuli zote za ujenzi hadi watakapoyahamisha makaburi hayo,” alisema Mtawa.

Alisema uamuzi wa kusitisha shughuli za ujenzi katika eneo hilo umefikiwa na yeye mwenyewe, Ofisa Mipango wa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Mkuu (CDA), Mwidick Skila, kampuni inayojenga barabara hiyo ya Maginga na kampuni inayochimba mitaro ya maji katika mradi huo ya Oriental.

Mradi huo unafadhiliwa na Benki ya Dunia (WB) na kusimamiwa na CDA.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa