Home » » SOFIA SIMBA AWATAHADHARISHA UWT

SOFIA SIMBA AWATAHADHARISHA UWT

Na Mwandishi Wetu, Dodoma
MWENYEKITI wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba, amewataka wajumbe wa jumuiya hiyo, kuchagua viongozi makini watakaoweza kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi mkuu ujao.

Sophia aliyasema hayo mjini hapa jana, alipokuwa akifungua Kikao cha Baraza Kuu la UWT.

Alisema kwamba, uhai na ushindi wa Chama Cha Mapinduzi unategemea uwepo wa Jumuiya ya Wanawake, ambayo ni imara na kielelezo halisi cha chama hicho tawala.

Kwa mujibu wa Sophia, UWT ni mhimili mkubwa wa CCM, hivyo wajumbe wa jumuiya hiyo wanatakiwa kuwa makini katika chaguzi zake mbalimbali.

Simba alisema endapo jumuiya hiyo haitakuwa makini katika uchaguzi wa viongozi wake katika kipindi hiki cha uchaguzi, CCM nayo itatetereka, kwa kuwa wanawake hao ni sehemu ya nguzo ya chama.

“Tuwe makini katika kuchagua viongozi wetu wa jumuiya, kwani uhai wa chama chetu unatutegemea sisi UWT.

“Ni muhimu sana kuwa makini kwa sababu hii timu tunayoichagua sasa ndiyo timu yetu ya ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015,’’ alisema Sophia.

Akizungumza kuhusiana na kikao hicho, Sophia alisema ni kikao cha kawaida ambacho kitafanya kazi mbalimbali, ikiwamo kuweka alama kwa wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya jumuiya hiyo.

Alisema kwamba, pamoja na kazi hiyo, pia kikao hicho cha siku mbili kitajadili hali ya uchaguzi wa ngazi mbalimbali pamoja na taarifa ya uendelezaji wa viwanja vya UWT.

Pia alisema kwamba, mkutano huo utaweka mikakati ya jumuiya hiyo katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa