Home » » Wabunge: Watendaji wa kata wakusanye kodi

Wabunge: Watendaji wa kata wakusanye kodi

KAMATI ya Bunge ya Bajeti, imependekeza watendaji wa kata watumike kukusanya kodi katika halmashauri nchini, kama njia mojawapo ya kukabiliana na upotevu mkubwa wa fedha. Akitoa mapendekezo hayo bungeni jana, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Andrew Chenge alisema halmashauri zimekuwa zikipoteza mabilioni ya fedha kwa kutumia mawakala katika ukusanyaji wa kodi.
“Kwa sababu hiyo kamati inashauri watendaji wa kata sasa watumike kukusanya kodi badala ya mawakala. Wakivuka malengo wapate bonasi,” alisema Chenge.

Chenge alikuwa akiwasilisha maoni ya kamati yake, kuhusiana na hotuba ya bajeti ya Serikali ya mwaka 2013/14 iliyosomwa bungeni wiki iliyopita na Waziri wa Fedha, Dk. William Mgimwa.

Hata hivyo katika taarifa yao, wabunge wa kamati hiyo walishauri Serikali iwe inachagua maeneo machache ya kipaumbele kila mwaka kuliko ilivyo hivi sasa.

“Serikali ichague maeneo machache ya vipaumbele kila mwaka. Mfano inaweza kuanza na matatu tu kama vile kilimo, miundombinu na nishati,” alisema.

Alisema suala la ununuzi serikali ambalo huchukua karibu asilimia 70 ya bajeti yake, huchangia katika upotevu wa mabilioni ya fedha zake kila mwaka kutokana na udanganyifu mkubwa na rushwa.

Chenge alipendekeza serikali iwe na jedwali la bei elekezi kwa vitu vinavyonunuliwa kwa wingi serikalini na akapendekeza jedwali hilo liwe limeandaliwa kufikia mwaka ujao wa fedha.

Pia alisema kuna matatizo makubwa ya ukusanyaji kodi katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutokana na udanganyifu unaofanywa na baadhi ya watumishi wake pamoja na rushwa.

Aliitaka Serikali kulipatia fedha Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), ambalo limekuwa likitumia zaidi ya Sh trilioni moja kununulia mafuta mazito kuendesha mitambo ya umeme, bila kuathiri shughuli za Serikali.

Alisema ni muhimu watendaji serikalini wabadili fikra zao na wawe tayari kuwajibika na kuwajibishwa wanapoharibu mambo ikiwa ni pamoja na kufuata utawala wa sheria.

Chenge pia aliitaka Serikali itekeleze ahadi yake ya kuipatia Benki ya Rasilimali ya Taifa (TIB) Sh bilioni 100 kila mwaka, kwa miaka mitano iweze kuimarisha mtaji wake.

Akishiriki kwenye mjadala huo, Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo alisema bomba la gesi asilia kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam ni lazima lijengwe kwa ajili ya kupunguza gharama za umeme.

“Tujenge bomba haraka ili nchi yetu iweze kuwa tofauti. Hata kama vikijengwa viwanda vya mbolea na saruji kule Mtwara, vitaajiri Watanzania wote siyo Wamakonde tu,” alisema.

Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila (NCCR Mageuzi), alisema Serikali imekuwa goigoi katika suala zima la ukusanyaji wa kodi kubwa na badala yake imebaki kukamua ushauri kwa walala hoi.

“Serikali hii ni ya kifisadi ndiyo maana haikusanyi kodi. Leo mnachukua ushuru kwa akina mama wa sokoni, halafu mnayaacha makampuni makubwa, tungeweza kuwaacha akina mama hawa na vijana waliojiajiri wenyewe,” alisema.


CHANZO: MTANZANIA

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa