Dodoma
Zaidi ya wananchi 29 wa Kijiji cha Kinusi Wilaya
ya Mpwapwa waliokuwa na mashamba na makaburi katika Mlima Kitononge wamekubali
kumpisha mwekezaji aliyegundua madini ya Shaba baada ya kuwapo kwa mvutano wa
fidia za kuhamishwa katika eneo hilo.
Mwekezaji huyo ambaye ni Kampuni ya C.S.N
Company amekubali kuchangia shughuli mbalimbali za maendeleo katika kijiji
hicho, jambo ambalo wananchi hao wamekubaliana naye kuanza kuchimba madini
hayo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Ussa Mnyama alisema
tayari wananchi 29 wameshalipwa fidia ya mashamba na makaburi katika mlima huo
ili kumpisha mwekezaji huyo ambaye amesema wamekubaliana kukisaidia kijiji
hicho katika shughuli za kimaendeleo.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Juma
Chibaya alikiri kumalizana na wananchi hao ambapo zaidi ya Sh40 milioni
zilitumika kuwalipa ili kuwapisha wao kuchimba madini katika mlima huo.
Chibaya alisema pamoja na mambo mengine lakini
wamekubaliana na uongozi wa kijiji hicho kusaidia shughuli mbalimbali za
maendeleo ambapo kwa kuanzia wataanza na kutengeneza madawati 100 ya Shule ya
Msingi Kinusi.
Alisema wananchi hao wamepongeza hatua ya
mwekezaji kufikia hatua ya makubaliano na wao na pia kitendo cha kukubali
kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii kwa ajili ya maendeleo ambayo ni muhimu
katika jamii kwani ni jambo la muhimu zaidi kwao. (Masoud Masasi).
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment