Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa
Katika
hali ya kawaida, binti wa miaka 11 (jina linahifadhiwa kwa sababu za
kimaadili), mkazi wa kijiji cha Kongogo, Wilayani Bahi mkoani Dodoma
hivi karibuni aliolewa na binamu yake, kisha ndoa yake kuvunjwa na
Serikali.
Hakuna
taarifa nyingi za mabinti kuolewa katika umri mdogo katika wilaya hiyo
mbali ya kuwepo kwa watoto wadogo ambao huondolewa katika masomo na
wengine kushindwa kupata elimu kwa sababu wazazi wao huwapeleka migodini
na wengine maeneo ya mijini kutumikishwa majumbani.
Hata
hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Bahi, Betty Mkwasa, anasema wilaya yake
inaongoza mkoani hapa kwa kuwa na kiwango kikubwa cha vitendo vya
ukeketaji wa wanawake ikiwa nayo ni sehemu ya ukatili wa kijinsia.
Lakini
kwa tukio hilo, lililojitokeza katika moja ya familia ya wafugaji,
kunaweza kukafanya umuhimu wa kujikita katika utafiti wa kina
kuliangalia suala la kuolewa katika umri mdogo lina ukubwa gani mkoani
hapa.
"Hazungumzi
na mtu yeyote humu ndani na unaweza kumsemesha anakuangalia tu, ila
anazungumza na mimi (Mkwasa), ama wasichana wawili tu wa hapa ndani
ambao anashinda nao,"anasema Mkwasa ambaye sasa anamlea mtoto huyo.
Maneno
hayo yanathibitishwa na mwandishi wa makala haya, aliyefika nyumbani kwa
Mkwasa kwa nia ya kuzungumza naye baada ya kupata taarifa ya kuwepo kwa
mtoto huyo.
Anapoitwa
kwa nia ya kutambulishwa, anafika mlangoni na kubaki akiangalia tu huku
wakati mwingine akiinamisha macho yake chini na hata anaposalimiwa
haitikii, badala yake anaondoka na kwenda kujificha ndani.
Hali hii
iliweka ugumu katika kufanya mahojiano naye, lakini kwa usiri mkubwa
inatubidi kumtumia mmoja wa wasichana ambaye amekuwa muwazi kwake
kusikia nini kilichotokea.
Si kwamba
hazungumzi, la hasha binti huyu ni mzungumzaji mzuri na tunapotoka nje
na kuwaacha wawili ndani ya sebule hiyo tunawasikia wakizungumza na hata
kucheka kwa sauti.
Mkwasa
anasema siku za mwanzoni binti huyo alikuwa haongei na mtu yoyote lakini
baada ya kuhudumiwa na mwanasaikolojia ambaye hufika nyumbani kwake
kila baada ya siku tatu, alianza kuongea.
Akisimulia
tukio hilo, Mkwasa anasema mtoto huyo alikutwa akizubaa na akiwa
amechoka katika kijiji cha Mindola baada ya kutoroka kwa mwanamume
aliyeolewa naye.Anasema alipigiwa simu na viongozi wa kijiji hicho na
kuagiza apelekwe katika kituo cha polisi.
"Nilikuwa
kwenye kikao mjini, nikawaambia OCD (Mkuu wa Kituo cha Polisi cha
Wilaya), akae naye mtoto huyo hadi nitakaporejea, nilimwona mtoto.
Hakuwa katika hali nzuri sana kwanza alikuwa mwoga, halafu hakuwa
anaongea na mtu yeyote,"anasema.
Anasema
polisi walimshauri kumpeleka mtoto huyo kwa daktari kwa ajili ya vipimo
ambapo iligundulika kuwa ameshaingiliwa sana kimapenzi na kuambukizwa
magonjwa ya zinaa.
"Alipewa
dawa na tukarudi nyumbani. Licha ya kulalamika kuwa anasikia maumivu,
hata kaa yake pale nyumbani kwa siku za awali haikuwa nzuri,"anasema
Mkwasa.
Anasema
baada ya siku mbili mtoto huyo alionekana anajisaidia haja ndogo
iliyochanganyika na damu, hali iliyomfanya kumrudisha tena hospitali
alifanyiwa vipimo na kupewa dawa.
CHANZO MWANANCHI
CHANZO MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment