Home » » Bunge lataka taarifa ya Kamati ya Pinda matokeo mabaya ya mitihani

Bunge lataka taarifa ya Kamati ya Pinda matokeo mabaya ya mitihani

Margaret Sitta
 
Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii, imeitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuwasilisha taarifa ya utekelezaji ya mapendekezo ya tume ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, iliyoundwa kuchunguza chanzo kilichopelekea kuwapo kwa matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka jana.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Margaret Sitta, alisema jana kuwa mpaka sasa taarifa hiyo haijawasilishwa katika Kamati hiyo hivyo inapelekea kuwapo kwa ugumu wa utekelezaji wake.

Alisema Kamati yake inategemea kupata mapendekezo ya utaratibu wa uendeshaji wa mitihani pamoja na alama zake. “Japokuwa tume ile ingekuja na mapendekezo mengi kama vile uchache wa walimu, upungufu wa maabara, lakini kubwa zaidi wangekuja na mapendekezo ya masuala la mitihani,” alisema Sitta.

Sitta alisema nia na dhumuni la Kamati yake kupata taarifa ya tume ni kuona kama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inatekeleza mambo waliyoagizwa na tume hiyo kupitia ripoti iliyotolewa.

Kadhalika, Kamati hiyo, imeitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kusitisha mpango wake wa kuanzisha alama mpya za matokeo kwa kuwa Baraza la mitihani Tanzania (Necta) kupitia bodi yake haikushirikishwa katika uanzishwaji wa mchakato huo.

Alisema mchakato huo haukuishirikisha bodi kutoka Necta ambao ndiyo wadau wakuu wa elimu nchini pamoja na wataalamu wa elimu.

Aliongeza kuwa pindi Necta kupitia bodi yake itakaposhirikishwa katika uanzishwaji wa mfumo huo mpya, ndipo taarifa itatangazwa ya kuanzishwa kwa mfumo huo mpya wa matokeo.
Tume iliyoundwa na Pinda kuchunguza matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka jana iliongozwa na Profesa Sifuni Mchome ambaye kabla ya kuwasilisha taarifa yake kwa umma, aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa