Home » » Wapewa siku 14 kupata soko kwa mazao ya wakulima

Wapewa siku 14 kupata soko kwa mazao ya wakulima

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi ametoa siku 14 kwa wataalamu kuhakikisha kwamba soko kwa mazao ya wakulima yanayosubiri bei nzuri linapatikana.
Aidha amewataka wakuu wa wilaya za mkoa huo kutokaa ofisini na kusubiri taarifa za wataalamu.
Dk Nchimbi aliyasema hayo jana alipokuwa akitembelea ghala la kuhifadhia zao la mpunga la wakulima ambao wanasubiri bei nzuri ya mazao yao Wilaya ya Bahi (AMCOS).
Mkuu huyo wa mkoa alitumia ziara hiyo ambayo ni sehemu ya uzinduzi wa msimu wa kilimo kimkoa kwa mwaka 2014, kuhimiza mabadiliko ya kiutendaji ili kufanikisha juhudi za kuinua kilimo mkoani mwake.
Mkuu huyo alisema wakulima katika maeneo mengi ya mkoa huo wamekuwa wakilalamikia masoko huku wataalamu na wakuu wa idara wakileta visingizio mbalimbali bila kuwasaidia wakulima hao.
Alisema ni vyema sasa wataalamu kutumia usomi huo kutafuta suluhisho la changamoto mbalimbali badala ya kuwa wataalamu wa kutoa ufafanuzi wa changamoto hizo.
Aidha aliwageukia wakuu wa wilaya waliokuwapo katika uzinduzi huo na kuwataka wasikae maofisini na kuwahimiza wasaidizi wao kwenye halmashauri kuwajibika.
Alisema atakayeona ameshindwa milango iko wazi kujiondoa katika nafasi yake.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa