WANAFUNZI 43 wa shule za sekondari mkoani Dodoma ambao pia ni
yatima wamepata msaada wa kulipiwa ada na vifaa vya elimu zaidi ya sh
milioni 4.7 kutoka kwa wafadhili mbalimbali.
Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waisilamu Tanzania (Bakwata) Kata ya
Chang’ombe, Suleman Mabada, alieleza hayo jana alipokuwa akitoa taarifa
fupi kwenye sherehe ya mwaka mpya ya Kiislamu iliyoandaliwa na baraza
hilo. Sherehe hiyo iliambatana na uzinduzi wa mfuko wa Beitilimali.
Alisema kiasi hicho cha fedha kimewezesha wanafunzi hao kununuliwa
vifaa vya shule ikiwemo kulipa ada, madaftari, sare za shule na
michango ya madawati.
Alisema pamoja na ufadhili huo pia baraza hilo linatarajia kuendelea
kukusanya zaidi ya sh milioni 2.5 kutoka kila kaya ya Kiislamu, ili
kuzisaidia familia zisizo na uwezo zikiwemo za wajane, wazee wagonjwa,
walemavu na watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Alisema malengo ya makusanyo hayo ni kutunisha mfuko huo ambao uko kwa ajili ya maendeleo ya waumini na wanafunzi.
“Michango hiyo itakusanywa na mabalozi wa dini ya Kiislamu walioko
ndani ya kata yetu, hivyo kila muumini atalazimika kuchangia sh 1,000
na makusanyo hayo yatasaidia hao walengwa kupitia mfuko huo,” alisema
Mabada.
Katibu wa Bakwata Kata ya Chang’ombe, Bashuru Omar, alisema pamoja na
juhudi zinazofanyika za kuwasaidia waumini wasiojiweza, pia baraza
linakusudia kujenga kituo cha watoto yatima na shule ya Chekechea
pamoja na kuanzisha miradi mbalimbali.
Aliitaja baadhi ya miradi hiyo kuwa ni ufugaji wa nyuki na utoaji wa
mikopo isiyokuwa na riba kwa kinamama na kina baba ndani ya kata hiyo.
Chanzo;Tanzani Daima
0 comments:
Post a Comment