Ndugu zangu,
Jana saa kumi jioni nilishachukua nafasi yangu kwenye kijiwe hicho ( Pichani) cha wafanyabiashara ndogo ndogo Soko Kuu, Iringa.
Kwa
kawaida, ndani ya banda hili la biashara kwa muda kama ule wa jana,
watu huwa bize kuangalia mechi za Ligi Kuu zinazorushwa na Azam TV
kutokea Dar. Na jana kulikuwa na Big Match; Azam dhidi ya Mbeya City.
Lakini,
kwa umuhimu wa hotuba ya Rais, hata wapenzi wale wa soka waliamua kwa
hiyari yao kusamehe soka na kubaki na hamu ya kufuatilia mambo muhimu
kwa nchi, na kwa wakati huu.
Na
hakika, aliyoanza nayo JK kwenye hotuba yake ndio haswa ilikuwa hamu ya
Watanzania hawa niliojumuika nao kumsikiliza Rais wa Nchi.
Walikuwa
na hamu sana ya kupata mtazamo na ufafanuzi wa Rais wao juu ya yaliyo
karibu sana nao ( Proximity): Katiba na wimbi la Ujangili. Katiba
inahusu mustakabali wao na watoto wao. Inahusu pia ulinzi wa rasilimali
zao. Kwamba Katiba iliyo bora inaweza pia kuwazuia ‘ Majangili wa
Kisiasa’ kuingia au kubaki madarakani huku wakifanya ‘ ujangili’ wa mali
ya umma wakilindwa na mfumo dhaifu unaotokana na Katiba dhaifu.
Na
Wananchi wale wanajua pia, kuwa wimbi la ujangili dhidi ya wanyamapori
wetu unawahusisha pia vigogo wakiwemo wanasiasa. Wanataka kujua namna
gani wahusika watadhibitiwa ili wasije kuwamaliza wanyamapori wetu kwa ‘
Ujangili’ wao.
Suala
la Afrika Mashariki na kutengwa kwa nchi yetu linawagusa na kuwakera
Watanzania wengi. Wamefurahi kuwa Rais wa Nchi kalizungumzia Bungeni.
Kwamba msimamo wetu kama nchi hatujitoi Afrika Mashariki.
Na
ni ukweli, kuwa si ni Wana Jumuiya ya Afrika Mashariki na tutabaki kuwa
hivyo. Hatuwezi kuwa jumuiya ya watu wa Afrika Magharibi, Kusini au
Kaskazini.
Rais
ameahidi kuendelea kuzungumza na Marais wenzake na tunaamini kuwa
itafika mahali wenzake nao watatambua, kuwa hakuna Afrika Mashariki bila
Tanzania.
Lakini,
kwa Watanzania , Jumuiya ya Afrika Mashariki haiwaumizi sana kichwa
kuliko haya ya Katiba , ujangili na mengineyo wanayokutana nayo nje ya
milango yao kila kukicha. Mambo yenye kauthiri maisha yao ya kila siku.
Maana,
tunajua, kuwa hakuna nchi ya Afrika Mashariki itakayotulazimisha
tushirikiane kwenye tusilotaka kushirikiana. Tukiweka msimamo wetu kama
taifa utabaki kuwa hivyo, hata waje na vifaru vya kivita, tutapigania
msimamo wetu na tutashinda.
Na
katika hili iko wazi, kuwa kwa sasa Watanzania hatutaki yaingizwe
kwenye jumuiya masuala ya Uhamiaji, Ajira, Ardhi, Sarafu Moja na nchi
yetu kuwa ndani ya Shirikisho la Kisiasa. Mengine yote tumesema sawa.
Na
Tanzania haitakuwa nchi ya kwanza duniani kuchagua mambo ya
kushirikiana kwenye jumuiya. Mfano hai ni kwenye Jumuiya ya Ulaya, nchi
ya Norway ni mwanachama lakini haimo kwenye ushirikiano wa masuala ya
Uhamiaji ( Schengen) Hivyo hivyo kwa Uingereza.
Kwenye
Jumuiya hiyo hiyo ya Ulaya, Norway, Sweden na Uingereza hawamo kwenye
kushirikiana kwenye sarafu moja ya Euro. Na kuna mifano mingine. Yote
haya yanatokana na matakwa ya wananchi wa nchi hizo kupitia kura za
maoni. Kwamba wananchi wa nchi hizo wamekuwa tayari kuwa kwenye Jumuiya
ya Ulaya lakini kuna maeneo ambayo wamekataa kuyaingiza kwenye jumuiya.
Na
sisi Watanzania tutakuwa watu wa ajabu sana, katika mazingira yetu ya
sasa, tukakubali kuyaingiza kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki maeneo ya
Uhamiaji, Ajira, Ardhi, Sarafu , na hata kuwa ndani ya Shirikisho la
kisiasa.
Hivyo basi, kuhusu Afrika Mashariki, Watanzania tuko nyuma ya Rais wetu kimsimamo, na hatutasogea hata hatua moja.
Lakini,
kuna ya kwetu ya kila kukicha na yenye kutuhusu na kutuathiri leo, na
yatawahusu na kuwaathiri watoto na wajukuu zetu kesho na kesho kutwa.
Ni
haya ya Katiba, Ujangili, kutunga sheria za kubana vyombo vya habari
ilihali uporaji na kujimilikisha maelfu ya ardhi bila hata kuyatumia
kunaofanywa hata na wanasiasa wetu kukiendelea.
Haya yana athari ya mbaya kwa mwananchi kila kukicha na tuendelee kupambana nayo kwa kasi zaidi…
0 comments:
Post a Comment