Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anadaiwa kuingilia kati mkakati wa kumng’oa madarakani, Spika wa Bunge, Anne Makinda.
Mkakati huo unaongozwa na Mbunge wa Nzega, Dk Khamis Kigwangalla (CCM).
Habari zilizopatikana jana bungeni mjini Dodoma
zilisema juzi asubuhi, Pinda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wabunge wa CCM,
alimwita Dk Kigwangalla katika kikao kilichowajumuisha baadhi ya
wajumbe wa Kamati za Uongozi na Maadili za wabunge wa chama hicho,
ambako suala la kutaka Spika ang’oke lilijadiliwa.
Habari hizo zilisema wakati Pinda akichukua hatua
hiyo kupitia mkondo wa chama, Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge, nayo ilianza kukutana juzi mchana ili kujadili hoja ya Dk
Kigwangalla iliyowasilishwa kwake na Ofisi ya Katibu wa Bunge.
Kamati hiyo inatarajiwa kuendelea na kikao chake
leo ambapo mbunge huyo ataitwa kwenda kutoa maelezo yake, kabla ya
kumsikiliza Spika Makinda.
Habari kutoka ndani ya kikao cha CCM, ilisema Dk
Kigwangwalla alishawishiwa aondoe hoja yake kwa sababu anaiongezea
misukosuko Serikali na chama hicho tawala, hasa kwa kuzingatia kuwa
tayari mawaziri wengine akiwamo Pinda walikuwa wakishinikizwa wajiuzulu
kutokana na athari za Operesheni Tokomeza Ujangili. Dk Kigwangalla
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, alikiri kuitwa katika vikao vya CCM, lakini hakuwa
tayari kuweka bayana kile kilichojiri katika vikao hivyo kwa maelezo
kuwa ni siri za chama.
“Wewe (mwandishi) jua tu kwamba ni kweli nimeitwa
kwenye vikao, lakini yaliyojiri huko ni kwa ajili ya chama na siyo mambo
ya kuweka wazi,” alisema mbunge huyo.
Taarifa ambazo zililifikia gazeti hili juzi usiku,
zilisema Dk Kigwangalla alitarajiwa kukutana tena na waziri mkuu ili
kumpa mrejesho wa tafakuri yake.
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jenista Mhagama ambaye
pia ni Mbunge wa Peramiho, alisema hakukuwa na kikao chochote kuhusu
suala hilo kwa sababu Pinda alikuwa Dar es Salaam kwa shughuli za
kikazi.
“Pengine tusubiri na tutashauriana kuona kama kuna umuhimu wa kuwa na mashauriano ndani ya chama,” alisema.
CHANZO;MWANANCHI
CHANZO;MWANANCHI
0 comments:
Post a Comment