Dodoma. Naibu Katibu Mkuu wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mwigulu Nchemba, amemwonya Spika wa Bunge,
Anne Makinda kuacha kutumia vibaya fedha za Serikali kwa kuwapa posho
wabunge kwa ajili ya kwenda kwenye michezo nje ya nchi.
Nchemba ambaye ni Mbunge wa Iramba Magharibi
alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akichangia Muswada wa Sheria ya
Marekebisho ya Sheria ya Ushuru wa bidhaa ya mwaka 2013 iliyowasilishwa
na Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salumu.
Mkuya katika maelezo yake alisema kuwa kodi hiyo
imefutwa kwa laini za simu kwa mtu mmoja mmoja na badala yake imeongezwa
katika kodi kutoka asilimia 14.5 hadi asilimia 17.
Katika mchango wake, mbunge huyo alionya kuwa
kumekuwa na tabia ya kutumia vibaya fedha za umma jambo alilosema
linaanzia ndani ya bunge.
“Naomba tukubaliane katika kubana matumizi, na
hivyo ninakuomba Mheshimiwa Spika tuanze na ofisi yako achana na kutoa
fedha kwa kuwapa wabunge kwa ajili ya kwenda Dubai kwa burudani,”alisema
Nchemba.
Alisema umefika wakati ambao Serikali inatakiwa
kufanya uamuzi wa kutumia fedha katika mambo muhimu ambayo yanaigusa
jamii kuliko mambo ambayo hayana maana. Kwa upande mwingine aliwalaumu
watendaji kuwa wameiangusha Serikali ya Chama Cha Mapinduzi kwa
kushindwa kutoa ushauri na usimamizi mzuri katika makusanyo ya kodi.
Kwa upande wake Mbunge wa kuteuliwa James Mbatia
aliinyooshea vidole Serikali kuwa ndiyo iliyovuruga mchakato mzima wa
makusanyo ya kodi ambayo muswada wake ulishapitishwa.
Mbatia alitoa sababu kuwa ndani ya Serikali wamekuwa wakiamua mambo lakini kwenye utekelezaji wake wanagawanyika
Chanzo;Mwananchi.
Chanzo;Mwananchi.
0 comments:
Post a Comment