Home » » Ndugai:Viongozi wanachochea mgogoro wakulima, wafugaji Kiteto

Ndugai:Viongozi wanachochea mgogoro wakulima, wafugaji Kiteto

Naibu Spika wa Bunge,Job Ndugai
 
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai   amesema mgogoro wakulima na wafugaji katika wilaya ya Kiteto mkoani Manyara unachangiwa na viongozi wa serikali kutokana na ubaguzi.
Ndugai ambaye pia ni Mbunge wa Kongwa (CCM),   alisema  viongozi hao wamekuwa wakichochea mgogoro kutokana na kuchukua rushwa ya ng’ombe kwenye kila boma la mfugaji kwa ajili ya kuwafukuza wakulima katika maeneo yao wanayolima.

Akizungumza juzi na mamia ya wakulima kutoka wilaya mbalimbali waliokusanyika katika mji mdogo wa Kibaigwa, Ndugai alisema  mkutano huo haujafanyika Kiteto kutokana na kutokuwapo amani wala demokrasia.

Alisema anamuomba Rais aliangalie jambo hilo kwa jicho la kipekee ili liweze kwisha na wakulima waweze kulima katika msimu huu wa kilimo.

“Tatizo la kule ni ubaguzi tu pale Kiteto hakuna ugomvi wa makabila yoyote na Wamasai ugomvi ule ni wa viongozi kwani wanachangisha ng’ombe kwa kila boma... We umewahi kuona wapi kikao cha kikabila Mwenyekiti wake akawa Mkurugenzi wa Halmashauri?,”alihoji Ndugai.

Alisema anatambua kuwapo kwa mgogoro mkubwa wa wakulima na wafugaji katika maeneo ya Kiteto lakini  unakuzwa na viongozi ambao wanawakumbatia wafugaji na kuwafukuza wakulima kwa madai kuwa wanaharibu mazingira.

Aliwataka viongozi wa Mkoa wa Manyara na Dodoma kushirikiana na kuliangalia suala hilo kwani haliko sawasawa.

 “Watendaji hawabadiliki na kama hawabadiliki basi kuna haja ya kuchukua hatua itakuwaje itangazwe hifadhi mkulima aondolewe halafu mfugaji abaki kama si ubaguzi,”
“Wafugaji wamekuwa wakichangishana fedha kwa ajili ya kuwakomoa wakulima,  jambo jingine la ajabu ni pale wanapodai kuwa wakulima wapo katika eneo la hifadhi  ni sheria gani ambayo imesajili kuwa hifadhi hilo eneo wakati hakuna jambo kama hili hayo yote yanatokana na ubaguzi unaofanywa na viongozi, ” alisema Ndugai

Aliwataka wakulima kuendelea kulima na wasikubali kunyanyaswa na mtu yoyote kwa madai kuwa ni eneo la hifadhi wakati halijawekwa kisheria.

 “’Kilimo cha Kiteto ni kilimo kikubwa sana kina matrekta zaidi ya 1,000 na matrekta hayo mengine yamepatikana kwa mkopo  lakini kama hiyo haitoshi chakula kinachozalishwa ni kingi mno ambacho kinalisha nchi nzima na nje ya nchi na zaidi kinauzwa katika soko la kimataifa la Kibaigwa,”alisema Naibu huyo.

Alifafanua kuwa  hata hati ya hifadhi hiyo haipo na amejitahidi kutafuta kwa muda mrefu na hajaiona na kudai kuwa kitendo cha wakulima waondoke na wasiendelee kulima ni sawa na kutaka watu waendelee kufungwa na kukimbia familia zao.

 “Lugha ya kuwaita wananchi wavamizi wakati ni Watanzania huo ni ubaguzi tena unatakiwa kukemewa tukae pamoja tutatue migogoro na ndiyo jambo tulilojifunza kwa Mandela na si ubaguzi unaofanywa hivi sasa na Viongozi wa Kiteto,” alisema Ndugai. Aliwataka wananchi kujiandaa kupiga kura ya maoni na kujiandikisha katika maeneo yao.

 Awali akisoma taarifa kwa niaba ya wakulima wenzake, Katibu wa Wakulima Josephat Mponda, alisema kuwa wanashangaa kuitwa wavamizi wakati wameanza kulima katika maeneo hayo miaka mingi.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa