Makamu Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, John Malecela
Vita ya urais kupitia CCM inazidi kushika kasi baada ya Makamu
Mwenyekiti Mstaafu wa chama hicho, John Malecela kuutaka uongozi
kumchukulia hatua Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kwa kuanza
mapema kampeni.
Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya Katibu wa
Uhamasishaji na Chipukizi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Paul
Makonda kumtuhumu Lowassa kuwa anakiyumbisha chama hicho kutokana na
kampeni za kutaka kuwania urais wa 2015.
Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika
nyumbani kwake mjini Dodoma jana, Malecela alisema Sekretarieti ya CCM
inapaswa kuwachukulia hatua kali makada wanaojipitisha maeneo mbalimbali
nchini kwa nia ya kusaka urais, kabla ya chama hicho kupanga muda.
Aliwafananisha walioanza mbio za urais kupitia CCM
na watu wanaowahi kukimbia kabla ya kipenga kupigwa na kusema hawawezi
kupimwa sawa na wale wanaosubiri kuanza rasmi kwa kampeni. Alimpongeza
Makonda kwa ujasiri wa kukemea hatua hiyo ya Lowassa bila woga.
Alipoulizwa juu ya suala hilo, Lowassa alijibu
kupitia msaidizi wake kuwa hana la kusema. “Nimezungumza na Mheshimiwa
Lowassa juu ya suala hilo lakini amenituma niwaambie kuwa hana ‘comment’
(hana la kusema),” alisema msaidizi wake huyo.
Fulana hadharani
Alipoulizwa swali la kwa nini ameamua kumtaja
Lowassa pekee huku kukiwa na makada wengi wanaojipitisha kupiga kampeni
za urais, kabla ya kujibu, Malecela ambaye aliwahi kuwa Makamu wa Kwanza
wa Rais na Waziri Mkuu, aliingia ndani ya nyumba yake na kutoka akiwa
ameshikilia mfuko uliokuwa fulana mbili.
Alitoa fulana hizo, moja ikiwa na rangi nyeusi na
kahawia na nyingine yenye rangi nyekundu na nyeupe zikiwa zimeandikwa
‘Friends of Edward Lowassa’ (Marafiki wa Edward Lowassa).
“Hivi kuna mwingine aliyefanya hivi? Na hizi
zimegawiwa nchi nzima. Ehhh! Hivi kuna mwingine kafanya hivi? Sijui,
niongezee nini tena zaidi ya hapo,” alisema Malecela huku akionyesha
fulana hizo.
Malecela ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza la Ushauri
la Taifa la CCM, alisisitiza kuchukuliwa kwa hatua haraka kwa vitendo
hivyo akisema harakati za Lowassa kuwania urais kupitia chama hicho
zimesababisha mgawanyiko.
“Jinsi tunavyochelewa kuchukua hatua ndivyo
tunavyoweza kuleta mpasuko ndani ya chama. Hapa najiuliza, ile misingi
imara ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi iko wapi? Mpaka tumwachie
mtoto (Makonda) akemee haya? Je, hapa chama kiko wapi?” alisema.
Alitahadharisha kuwa chama kisipotoa karipio au
tamko kuhusu suala hilo, wanaotumia fedha kwa lengo la kutafuta umaarufu
na ushawishi ili kupata madaraka wataharibu misingi bora ya uongozi
iliyowekwa na waasisi wa CCM.
“Kinachonisikitisha zaidi ni kuona juhudi za uongozi wa sasa wa
chama ngazi ya juu ikiwa ni pamoja na sekretarieti inayoongozwa na
Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana na Katibu Mwenezi Nape Nnauye za kutetea
chama hiki zinatiwa mchanga,” alisema na kuongeza kuwa juhudi hizo
zisibezwe.
Malecela aliishauri Sekretarieti ya CCM kuchukua
hatua mara moja, kwa maelezo kuwa Makonda asingesema hayo yote kama hana
uhakika wa ushahidi.
Alisema waasisi wa chama hicho walikijenga kwa
tabu na hakuna aliyediriki kutumia fedha kutaka madaraka... “Nidhamu,
busara na uchungu wa rasilimali za taifa hili kwa masilahi ya wananchi
ndivyo vilivyotuongoza kufuata misingi na maadili ya uongozi ndani ya
chama na Serikali.”
Alisema vijana na wanachama wa CCM wanataka kujua msimamo wa chama chao.
Akizungumzia kauli hiyo ya Malecela, Nnauye
alisema: Tumemsikia, ushauri wake tutaufanyia kazi.” Hakutaka
kuzungumzia zaidi suala hilo.
Tangu Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli
kuandaa hafla kubwa kusherehekea Mwaka Mpya nyumbani kwake Monduli
ambako alitangaza kuanza rasmi safari aliyoiita ya matumani ya ndoto
zake, ambayo pia itatimiza ndoto za Watanzania za kupata elimu bure,
majisafi na maendeleo ya uhakika, makada wa chama hicho wameingia katika
malumbano makubwa.
Malumbano hayo ambayo Malecela amesema hayana tija
kwa chama na hayaleti umoja na mshikamano ambao umekuwapo kwa miaka
mingi, yalipamba moto baada ya hivi karibuni baadhi ya wenyeviti wa
mikoa wa chama hicho, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Geita, Joseph Kasheku
‘Msukuma’ kumjia juu Mwenyekiti wa Singida, Mgana Msindai kwa kudai
wenyeviti wote walikuwa wanamuunga mkono Lowassa.
Hata hivyo, Msindai ambaye pia ni Mwenyekiti wa
wenyeviti wa CCM wa mikoa, alikanusha kutoa kauli hiyo kwa maelezo
kwamba alikuwa akiwazungumzia wenyeviti aliokuwa amefuatana nao Monduli
katika hafla hiyo.
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment