Picha
juu na chini ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete akikagua sehemu ya kukalia
katika Bunge jijini Dodoma alikotembea kukagua ukarabati na marekebisho
yanayoendelea tayari kwa kupokea wajumbe wa Bunge la Katiba baadaye
mwezi huu. Pichani juu kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mh. Anne Makinda na kushoto ni WAZIRI wa Nchi katika Ofisi ya
Waziri Mkuu (Sera na Uratibu wa Bunge), William Lukuvi.
Picha juu na chini ni Rais Jakaya Mrisho Kikwete akitembezwa sehemu
mbalimbali za majengo ya Bunge jijini Dodoma alikotembea kukagua
ukarabati na marekebisho tayari kwa kupokea wajumbe wa Bunge la katiba
baadaye mwezi huu.
Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akipiga picha na wafanyakazi wa kampuni ya ujenzi
inayokarabati na kufanyia marekebisho ukumbi wa bunge mjini Dodoma
tayari kwa kupokea wajumbe wa Bunge la katiba baadaye mwezi huu.
Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete,
Jumamosi, Februari Mosi, 2014, amekagua na kuridhishwa na kazi na kasi
ya marekebisho yanayofanywa katika Ukumbi wa Bunge mjini Dodoma ikiwa ni
maandalizi ya Vikao vya Bunge Maalum la Katiba linaloanza baadaye mwezi
huu.
Rais
Kikwete amesimama kwa muda mjini Dodoma kujiridhisha na mwenendo wa
maandalizi ya Bunge Maalum akiwa njiani kwenda Mbeya ambako atafanya
ziara ya kikazi ya siku mbili.
Rais
Kikwete amekagua Ukumbi huo na huduma nyingine muhimu kwa ajili ya vikao
hivyo ikiwa ni pamoja na bwalo la chakula kwa kiasi cha dakika 45 na
kuvutiwa na mwenendo wa kazi na kasi ya marekebisho kwenye ukumbi huo.
Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa William Lukuvi amemhakikishia
Rais Kikwete kuwa kazi yote ya kufunga viti na vipaza sauti, ambavyo
vitatumia mfumo wa kisasa wa mawasiliano ya kadi, ndani ya ukumbi huo
itakuwa imekamilika ifikapo Februari 10, mwaka huu, siku tisa kuanzia
sasa.
Baada ya
kusikiliza maelezo hayo, Rais Kikwete amesema kuwa ni vizuri uongozi
unaosimamia kazi hiyo ukajipa kiasi cha wiki moja baada ya Februari 10
kuhakikisha kuwa kweli kila mfuko unafanya kazi kabla ya shughuli za
Bunge Maalum la Katiba kuanza rasmi kwa kufunguliwa na Mheshimiwa Rais
mwenyewe.
Rais
Kikwete amewaambia watumishi wa Serikali na Bunge waliomtembeza kwenye
ukaguzi huo akiwamo Spika wa Bunge Mheshimiwa Anna Makinda na Katibu wa
Bunge Dk. Thomas Kashilila: “Nawapongeza sana kwa kuchapa kazi kwa
kasi na ufanisi. Kazi hii imekwenda kwa haraka sana kwa kutilia maanani
kilipomalizika kikao cha mwisho cha Bunge.”
Wakati Rais
Kikwete akikagua huduma hizo, mafundi wa stadi mbali mbali walikuwa
wanaendelea na kazi ikiwa ni pamoja na kufunga viti vyenye rangi
nyekundu na Nembo ya Taifa kwenye ukumbi huo.
Bunge
Maalum litakuwa na wajumbe 645 ambao ni Wabunge wa sasa wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la
Zanzibar na Wajumbe 201 ambao watateuliwa na Rais kutokana na
mapendekezo ya makundi mbali ambayo yanatajwa katika Sheria ya
Marekebisho ya Katiba.
0 comments:
Post a Comment