Home » » Ardhi, uraia vyazua dukuduku

Ardhi, uraia vyazua dukuduku

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Miongoni mambo yaliyozungumzwa na Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na kuibua hisia za wajumbe ni suala la uraia, maadili ya viongozi wa umma pamoja na utaratibu wa kumpata Rais.
Suala la uraia pengine ndilo linaloweza kuelezwa kwamba liliwakera baadhi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba ambao hawakutaka uraia uwe wa Jamhuri ya Muungano, badala yake walikuwa wakitaka uwe wa nchi washirika.
Kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni jana na Jaji Warioba, uraia utakuwa ni mmoja wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na umeorodheshwa miongoni mwa mambo ya Muungano.
“Uraia ni msingi wa utambulisho unaompa raia haki ya kulindwa na nchi yake, ikiwa ni pamoja na haki zake za binadamu za asili na zisizoondosheka kama zilivyotambuliwa au zitakavyotambuliwa,” alisema na kufuatiwa na kelele za baadhi ya wajumbe zilizoashiria kutokukubaliana naye.
Jaji Warioba hakujali kelele hizo na kuendelea: “Uraia ndiyo kigezo na sifa ya kupewa dhamana ya uongozi wa taifa na kuajiriwa katika mihimili ya Serikali na vyombo vya ulinzi na usalama. Rasimu inapendekeza kutambuliwa kwa uraia wa kuzaliwa na uraia wa kujiandikisha ambao katika kujidhihirisha kwake, ni uraia wa nchi moja usiojenga au kuleta hisia za kuwabagua au kuwatenga raia katika matabaka na madaraja yanayotokana na tofauti ya hali au fursa zao.”
Kuhusu taasisi ya urais, Warioba alisema kuna mapendekezo manne makubwa ambayo ni kumwondoa Rais kutoka kwenye Bunge, namna atakavyochaguliwa, matokeo yake kuhojiwa mahakamani pamoja na kupunguzwa kwa madaraka yake.
Jaji Warioba alisema wananchi pia walizungumzia kuporomoka maadili ya viongozi na kuwa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi iliyopo haina mamlaka ya kutosha ya kuchukua hatua.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa