Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Februari mwaka huu, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), lilitangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne wa mwaka 2013.
Katika matokeo hayo, wanafunzi 151,187 walipata
daraja sifuri, sawa na asilimia 42.91 ya watahiniwa 404,083 waliofanya
mtihani huo.
Bila shaka idadi ya watahiniwa waliofeli ni kubwa
na huenda wapo baadhi yao waliokata tamaa ya kuendelea na masomo baada
ya kufeli kwa kiwango hicho kikubwa.
Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mpwapwa iliyopo
Dodoma, Rukonge Mwelo anasema umefika wakati kwa Serikali kuanzisha
masomo ya ujasiriamali kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari ili
wale wanaofeli wasibaki njiapanda.
“Kuna wanafunzi wamepata sifuri kwenye mitihani yao lakini hao hao wakija kwenye kazi za mikono wanapata alama A,” anasema.
Anasema baadhi ya wanafunzi wanashindwa kufanya
vizuri katika mitihani kutokana na kuwepo kwa mazingira mabaya ya
kujifunzia, ikiwamo kukosekana kwa walimu na vifaa vya kujifunzia.
Mwelo anaongeza kusema: “Kama kila wilaya itakuwa
na kituo cha mafunzo ya ufundi stadi kwa watu waliofeli itasaidia sana,
kwa sababu kufanikiwa siyo lazima ufike kidato cha nne.”
Anatoa mfano wa wanafunzi walioacha shule na
kujiingiza katika biashara ya kusafirisha abiria kwa kutumia pikipiki
baada ya kukatishwa tamaa na wenzao waliopata sifuri.
Hata hivyo, mzazi Marry Kashinde anasema hata ujasiriamali nao unahitaji elimu ili mtu aweze kufanikiwa.
Anasema baada ya binti yake kufeli aliomba
afunguliwe biashara ya kuuza nguo za watoto, lakini alishindwa kuendea
kwa kukosa ujuzi wa kazi hiyo.
“Mimi nina ushahidi wa kutosha kuwa hata
ujasiriamali unahitaji elimu, siyo lazima iwe elimu rasmi lakini mtu
ajue hata namna tu ya kufunga mahesabu ya biashara yake,” anasema.
Anatoa ushauri kwa kusema: “Mzazi anatakiwa kujua
mtoto wake anapenda kufanya nini mapema kabla hata hajamaliza masomo
yake. Kile anachopenda ndicho aendelezwe kwa gharama yoyote.”
Mwalimu mstaafu Erick Kimbe anasema wapo wanafunzi waliofeli kwa
bahati mbaya kutokana na sababu mbalimbali, hata hivyo, wanaweza
kufaulu ikiwa watapewa nafasi ya kurudia mitihani hiyo.
Anasema hakuna sababu kwa mzazi kukata tamaa na
kuamua kumwacha mtoto wake nyumbani bila kazi yoyote, badala yake
azungumze naye ajue masomo gani anaweza kufaulu kama akipewa nafasi ya
kurudia.
“Ipo mifano ya watu wengi waliorudia mitihani na
kufaulu, ingawa baadhi ya ndugu na jamaa zao waliwaona hawana akili kwa
sababu tu walifeli mara ya kwanza,” anasema na kuongeza:
“Hakuna mtoto asiyeweza kila kitu, lazima kuna
kitu anakimudu vyema tena wakati mwingine kuliko hata hao wanaoonekana
kama wana akili darasani.”
Ni vyema kukumbuka kuwa watoto wengi wanafeli kwa
sababu wazazi wao hawana muda wa kutosha kufuatilia maendeleo ya watoto
wa shuleni. Mzazi au mlezi lazima akubali kuwa yeye ni sehemu ya matokeo
mabaya anayoyapata mwanaye.
Wahenga walisema kuteleza siyo kuanguka, hivyo
basi mshike mkono mwanao, jipange upya, nafasi ya kurekebisha makosa na
kusonga mbele ni kubwa kinachotakiwa ni kuamini kuwa kushindwa mara ya
kwanza kunatoa nafasi ya kujipanga upya.
Historia inataja watu wengi wenye mafanikio
makubwa duniani ambao walianza kwa kushindwa, lakini baadaye
walifanikiwa katika yale waliyokusudia.
Baadhi yao walishindwa zaidi ya mara moja lakini hawakukata tamaa, walitiwa moyo na ndugu na jamaa waliowazunguka.
Tajiri Bill Gates alipofungua kampuni yake ya
kwanza ya Tra-O-Data alishindwa na kuamua kuifunga, Mwanahisabati
maarufu, Isaac Newton ana historia ya kushindwa kulihudumia shamba la
familia yao.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment