Home » » ‘Wanasiasa msishabikie Katiba kwa maslahi yenu’

‘Wanasiasa msishabikie Katiba kwa maslahi yenu’

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba ambao ni wabunge na wawakilishi wamewataka wanasiasa wenzao kutoshabikia muundo wa utawala kwenye Katiba mpya kwa maslahi ya kupata vyeo. Badala yake wamewataka kuhakikisha Katiba mpya, inagusa maisha ya watu na uchumi kiujumla ili kuwasaidia wananchi kuondokana na umasikini na kupata maendeleo.
Akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya wenzake alioambatana nao, Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu alisema kwa hali ya sasa inavyoonekana baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kuwasilisha rasimu ya pili ya katiba, wanasiasa wamekuwa wakishabikia muundo wa serikali tatu kwa maslahi yao zaidi, ya kupata vyeo na wasahau wananchi ambao ndiyo wenye katiba hiyo mpya inayotarajiwa kutungwa.
Zungu aliambatana na Mbunge wa Kibaha Vijijini, Hamoud Jumaa, Mbunge wa Temeke Abbas Mtemvu, Mbunge wa Kinondoni Idd Azzan, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalumu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Haji Omar Kheir ambaye ni Mbunge wa Tumbatu na Mwakilishi wa jimbo la Chwaka, Issa Haji Ussi.
“Wanasiasa tuwe makini tuhakikishe katiba inagusa sana uchumi katika kuwainua wananchi, lakini sio kushabikia utawala huku wengine wakitaka kupata vyeo. Tuangalie na hivyo vyeo wanavyoshabikia vinaongeza gharama na watakaoumia ni wananchi,” alionya Zungu.
Naye Jumaa aliwataka wanasiasa wenzake kuvumiliana na kuweka mbele maslahi ya wananchi hivyo waweze kutoa katiba ya kuwasaidia wananchi badala ya kujiangalia wao wanafaidikaje.
Mtemvu alisema Jaji Warioba amegusia makundi aliyoyataka yeye na kutoa mfano mabaraza ya katiba ambayo yapo kisheria hayajagusiwa hivyo wananchi wameshindwa kujua maoni ya mabaraza hayo. Mabaraza ya katiba ya wilaya yalikuwa 170.
Alishangaa Tume ya Warioba kushabikia juu ya uongozi na kuacha mambo mengine kwenye rasimu hiyo ya katiba hasa yanayowagusa wananchi kama wafugaji, wakulima na wavuvi.
Ussi alisema uwasilishaji wa Jaji Warioba umebainisha ulikuwa na ajenda maalumu na ndiyo sababu akaweza kushauri serikali tatu huku akijua fika hakuna Mzanzibari aliyetaka serikali tatu na waliohojiwa ni wachache.
Kwa upande wa Kheir alitaka wajumbe wa katiba na wananchi kwa ujumla kujifunza historia za nchini na nchi nyingine na kusisitiza,
“waangalie nchi nyingi kama Misri na Libya ziliungana lakini haikufika mwaka mmoja ukavunjika, Sudan Kusini ilijitenga na Sudan, sasa hali mbaya inataka kuungana tena sasa sisi muungano wetu umekaa miaka 50 tunaleta sababu za kutaka uvunjike”.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa