Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kujadili
Bajeti ya Serikali 2013/14 linatarajiwa kuanza Mei 6, mwaka huu huku
likiwa limetengewa siku chache ambazo zitasababisha liendeshwe kwa kasi
ili kukamilisha shughuli zake.
Utaratibu wa sasa unalilazimisha Bunge hilo kuwa
limefanya uamuzi wake (kupitisha au kutokupitisha), Bajeti ya Serikali
pamoja na Sheria za Fedha ifikapo mwishoni mwa Juni kila mwaka, ili
kuruhusu utekelezaji wa bajeti husika kuanza Julai Mosi, siku ya kwanza
ya mwaka mpya wa fedha.
Ratiba ya Bunge hilo ambayo tayari imepata idhini
ya Kamati ya Uongozi iliyokutana Alhamisi iliyopita, inaonyesha kuwa
Bunge la Bajeti litakutana kwa siku 52, zikiwa ni pungufu kwa siku 28 au
wiki nne, ikilinganishwa na mkutano kama huo mwaka jana.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai alikiri
kupunguzwa kwa siku za Bunge la Bajeti akisema hali hiyo inatokana na
uchache wa siku pamoja na utaratibu mpya wa kuhakikisha bajeti
inapitishwa mapema ili ianze kutekelezwa Julai Mosi.
“Kamati ya Uongozi haikuwa na njia nyingine zaidi
ya kuminya siku ili kukimbizana na muda uliopo, hivyo ni kweli siku
zimepungua, lakini hatukuwa na jinsi maana tunatakiwa tumamalize
shughuli za bajeti mwishoni mwa Juni,” alisema Ndugai na kuongeza:
“Kama mnavyofahamu, siku nyingi zimetumika kwenye
Bunge Maalumu la Katiba, kwa hiyo hizo zilizobaki ndizo tulizozipangia
kazi nyingi zilizopo na hata ukiangalia wakati wa bajeti huwa kamati
zinakutana kwa wiki tatu, lakini tumewapa wiki moja tu.”
Mkutano wa 11 wa Bunge ambao ulijadili Bajeti ya
2013/14, ulitumia siku 80, ukifanyika kuanzia Aprili 9 hadi Juni 28,
2013 lakini zamu hii Bunge la Bajeti hadi litakapoahirishwa Juni 27,
litakuwa limekutana kwa siku 52.
Kuchelewa kuanza kwa Bunge la Bajeti
kumesababishwa na Bunge Maalumu la Katiba ambalo linahitimisha ngwe yake
ya kwanza Ijumaa wiki hii, likiwa limekutana kwa siku 67. Bunge la
Katiba linawajumuisha wabunge wa Bunge la Jamhuri na wale wa Baraza la
Wawakilishi.
Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema
tayari Kamati ya Uongozi imepitisha ratiba husika na kwamba mkutano huo
wa 15 utatanguliwa na Kamati za Bunge zitakazokutana Dar es Salaam kwa
siku tano tu, kuanzia Aprili 28, mwaka huu kabla ya wabunge kusafiri
kwenda Dodoma Mei 5.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi alisema licha ya kuwapo kwa shughuli
za Bunge Maalumu la Katiba, Serikali iko tayari kwa bajeti zote za
wizara pamoja na Bajeti Kuu.
“Sisi serikalini kwa jumla tuko tayari maana
wakati mawaziri wakiendelea na Bunge Maalumu, wataalamu walikuwa
wakiendelea na maandalizi na kimsingi, kila kitu kiko kama kinavyotakiwa
kuwa, kuanzia tutakapohitajika mbele ya kamati (za Bunge) hadi bungeni
kwenyewe,” alisema Lukuvi.
Athari kwenye mijadala
Uchache wa siku hizo, umesababisha kupungua kwa siku 13 za
mjadala katika wizara ambazo kutokana na umuhimu wake, mwaka jana
zilitengewa siku zaidi ya moja kwa ajili ya kuwapa wabunge nafasi ya
kujadili kwa kina na kutoa mapendekezo ya marekebisho.
Miongoni mwake ni Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo
chini yake zipo wizara za Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Sera, Uratibu na Bunge pamoja na Uwekezaji na Uwezeshaji
ambazo kwa pamoja zitajadiliwa kwa siku tatu tu, badala ya tano
zilizotengwa mwaka jana.
Wizara ya Maji ambayo mwaka jana ilipewa siku
tatu, mwaka huu imetengewa siku moja, sawa na wizara nyingine 10 ambazo
mwaka jana zilitengewa siku mbili.
Wizara hizo ni pamoja na Ofisi ya Rais, ambayo
inasimamia Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Utawala Bora na Uhusiano na
Uratibu na Makamu wa Rais inayosimamia Muungano na Mazingira.
Nyingine zilizoathiriwa na utaratibu huo ni
Kilimo, Chakula na Ushirika, Maliasili na Utalii, Mambo ya Ndani ya
Nchi; Elimu na Mafunzo ya Ufundi; Ujenzi; Uchukuzi; Afya na Ustawi wa
Jamii; Nishati na Madini; Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo pamoja na
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Serikali za
Mitaa, Dk Hamis Kigwangalla alisema: “Sisi tunalazimika kuomba siku za
ziada ili tuweze kutekeleza wajibu wetu vizuri, fikiria kamati yangu
inasimamia mikoa 25 kwa maana hiyo kwa siku tano tulizopewa ina maana
siku moja tupitie bajeti za mikoa mitano.”
Aliongeza: “Katika hali hii ni ngumu sana, la
sivyo tutakuwa rubber stamp (muhuri) kwenye mapendekezo, hivyo tumeomba
tuanze mapema kabla ya kamati nyingine na tumekubaliana na wajumbe wangu
ikiwezekana tufanye kazi hadi usiku wa manane ili tuweze kukamilisha
kwa wakati.”
Alisema ugumu wa kazi katika kamati yake unatokana
na kusimamia matumizi ya mikoa ambayo ni zaidi ya Sh4.3 trilioni, kiasi
ambacho kinakaribia kufikia theluthi moja ya bajeti nzima ya Serikali.
“Tukirashiarashia tu kwa fedha nyingi namna hii,
tunaweza kujikuta tumepitisha madudu mengi na kusababishia taifa hasara
ya kiasi kikubwa cha fedha,” alisema.
Bajeti Kuu
Hata hivyo, siku za mjadala kwa ajili ya bajeti
kuu zimebaki saba kama ilivyokuwa katika mkutano wa 11 mwaka jana. Dk
Kashililah alisema Bajeti Kuu ya Serikali itawasilishwa bungeni Juni 12
saa 10:00 alasiri na itatanguliwa na taarifa ya hali ya uchumi
itakayosomwa asubuhi.
Ratiba hiyo inaonyesha kuwa mjadala wa bajeti
utafanyika kati ya Juni 16 na 24 na kufuatiwa na upitishwaji wa miswada
ya Sheria ya Fedha na ule wa matumizi
Dk Kashililah alisema kabla ya kuwasilishwa kwa Bajeti Kuu, umetengwa
muda wa ushauriano baina ya Serikali na Bunge kupitia Kamati ya Bajeti
ili kuzingatia hoja zenye masilahi kwa taifa katika majumuisho ya bajeti
husika.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment