Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mapendekezo ya CCM ya kutaka kufanya marekebisho katika baadhi
ya vifungu katika Ibara ya 1 ya Rasimu ya Katiba yamegonga mwamba baada
ya kukosa theluthi mbili ya kura kutoka Zanzibar.
Hali hiyo imejitokeza katika kamati tatu kati ya 12 ambazo zimeanza kutoa matokeo ya kura baada ya mjadala.
Wakitoa taarifa kwa waandishi wa habari,
mwenyeviti wa Kamati Namba 1, Ummy Mwalimu na Namba 10, Anna Abdallah,
walisema kuwa theluthi mbili imekosekana katika baadhi ya vifungu kwenye
ibara hiyo.
Walisema kwamba vipengele vilivyokosa theluthi
mbili ya kura zilizopigwa, vitapelekwa bungeni pamoja na hoja
zilizotolewa na wengi na wachache. Abdallah alisema ibara nyingi
walizozipigia kura katika kamati yake hazikupata theluthi mbili ya kura.
“Kwa mfano muundo wa serikali kwa vyovyote vile
hatupati theluthi mbili, ila tunapata walio wengi wanataka nini. Walio
wengi wanataka mfumo wa serikali mbili, kwa hiyo taarifa yetu itakuwa na
maoni ya wajumbe wengi, na ile wachache,” alisema Anna.
Alikiri kuna wajumbe wachache ambao wanataka muundo wa shirikisho la serikali tatu, lakini hawawezi kusema hao ndio wameshinda.
Alitolea mfano wa ibara ya pili ya sura ya kwanza
ambayo inazungumzia mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo
waliafikiana kuongeza milima na anga.
Alisema kuwa ibara hiyo ilikubaliwa na wajumbe wote baada ya kuongezwa maeneo hayo mawili.
“Maeneo yenye utata ikiwamo kwenye muundo wa
serikali ndio tumeshindwa kupata theluthi mbili ya kura zilizopigwa na
wajumbe kutoka pande mbili za Muungano,” alisema.
Naye Mwalimu alisema ibara ya 1 katika sura ya kwanza hawakupata theluthi mbili pande zote mbili.
Alisema uamuzi huo si wa mwisho, bado watakwenda katika Bunge la Katiba kupigiwa kura za jumla.
Pamoja na kamati nyingine kuendelea kupiga kura,
habari za ndani zinasema upatikanaji wa theluthi mbili katika ibara hiyo
ya kwanza umekuwa mgumu.
Akizungumzia hali hiyo, mjumbe wa Bunge hilo, Zitto Kabwe
alisema kushindwa kuungwa mkono kwa mapendekezo hayo, maana yake ni
kwamba vifungu vinabaki kama vilivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba.
“Kukosa theluthi mbili inaweza kuwa na maana kubwa kuwa mapendekezo ya Tume yanabaki kama yalivyo,” alisema Zitto.
Naye John Mnyika alisema hatua hiyo inamaanisha kuwa uchakachuaji wa Rasimu ya Katiba umeshindwa.
“Taifa livute subira kwenye kura hizi za awali,
kwani kura zitapigwa tena bungeni, lakini ni muhimu wananchi wafuatilie
kwa makini yanayojiri katika kamati licha ya vikwazo vilivyowekwa kwa
vyombo vya habari,” alisema Mnyika.
Hata hivyo, kukosekana kwa theluthi mbili ya kura
katika kamati kunadaiwa kuchangiwa pia na utoro wa wabunge wengi wa CCM
katika vikao vya kamati.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ili
iweze kupitishwa na Bunge itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa theluthi
mbili kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya idadi ya wajumbe kutoka
Zanzibar.
Sitta atembelea kamati
Wakati huohuo, mwenyekiti wa Bunge la Katiba,
Samuel Sitta juzi alizunguka katika kamati zote 12 kuona mwenendo wa
shughuli na alipata maoni kutoka kwa baadhi ya kamati kuhusu mazingira
ya kazi.
Alisema baadhi ya kamati zilimwambia kuwa kumbi ni
ndogo na kwamba jana waliamua kubadili baadhi ya sehemu za kufanyia
vikao hivyo.
“Kwa mfano, ukumbi wa kamati namba 5 uliopo
ghorofa ya tano ni mdogo sana. Mimi nilikaa pale nikaanza kutoka jasho,
sasa kukaa pale kwa siku nzima ni tatizo kwa kweli,” alisema.
Alisema Kamati Namba 5 sasa imehamishiwa katika Hoteli ya St. Gasper.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment