WAZIRI
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo amewasilisha bajeti ya
wizara yake kwa mwaka ujao wa fedha wa 2014/2015 ya shilingi trilioni
1.082 huku kati ya fedha hizo sh. bilioni 957.1 zikiwa ni fedha za
miradi ya maendeleo na sh. bilioni 125.3 ikitengwa kwa ajili ya matumizi
ya kawaida.
Profesa Muhongo amesema
bajeti ya mwaka wa fedha wa 2014/2015 inakusudia kuimarisha na
kuendeleza sekta za nishati na madini ili kuongeza mchango wake katika
kujenga uchumi imara wa Taifa utakaotoa ajira mpya kwa Watanzania na
kupunguza umaskini nchini.
Akiwasilisha hotuba ya
Wizara hiyo bungeni mjini Dodoma jana, Profesa Muhongo alisema bajeti ya
mwaka huu imelenga kuwainua maskini na kusisitiza kuwa Wizara hiyo ni
ya miradi na sio mipango hivyo wananchi ni vyema kuchangamkia fursa
zilizopo kunufaika.
Aidha Profesa Muhongo
alisisitiza kauli yake kuwa hakutakuwa na mgawo wa umeme kutokana na
wizara hiyo kujipanga vilivyo na kwamba kama utatokea mgawo basi ni wa
magazetini na kwenye mitandao na si vinginevyo.
Sera na Sheria katika Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia
Alisema Serikali
iliidhinisha Sera ya Gesi Asilia mwezi Oktoba, 2013 ili kuimarisha
usimamizi wa Sekta Ndogo ya Gesi Asilia ambapo Rasimu ya Sera ya
Uwezeshaji na Ushirikishaji Wazawa (Local Content Policy) ziliandaliwa.
Alisema lengo la sera
hiyo ni kuhakikisha kuwa Watanzania wanashiriki ipasavyo katika shughuli
zote za rasilimali za mafuta na gesi asilia kwa manufaa ya kizazi cha
sasa na vijavyo.
"Rasimu ya Sera hiyo
imesambazwa kwa wadau mbalimbali wakiwemo Waheshimiwa Wabunge, Wizara,
Taasisi za Serikali na Washirika wa Maendeleo ili kupata maoni yao.
Wizara ingependa kupata maoni yenu kabla ya tarehe 30 Juni,
2014,"alisema Profesa Muhongo.
Pia alisema Serikali
imekamilisha Rasimu ya Kwanza ya Sera ya Petroli itakayotoa mwongozo
kuhusu usimamizi wa shughuli za utafutaji, uzalishaji na ugawanaji
mapato yanayotokana na Mafuta na Gesi Asilia pamoja na usafishaji,
uhifadhi, usafirishaji na usambazaji mafuta.
Alisema katika mwaka
2014/15 Rasimu hizo zitawasilishwa katika Mamlaka husika kwa ajili ya
kuidhinishwa ambapo kukamilika kwa sera husika kutaimarisha usimamizi wa
Sekta Ndogo ya Mafuta na Gesi Asilia kwa maendeleo ya kizazi cha sasa
na vijavyo.
"Mheshimiwa Spika,
napenda kulijulisha Bunge lako tukufu kuwa rasimu ya sheria ya gesi
asilia imekamilika. Rasimu imepelekwa kwa wadau ili kupata maoni yao
kabla ya kuikamilisha na kuiwasilisha katika kikao cha Bunge cha mwezi
Novemba, 2014," alisema Profesa Muhongo.
Kuendeleza Shughuli za Uchimbaji Mdogo wa Madini
Ali s ema kat i k a
mwaka 2013/14, shughuli za uchimbaji mdogo zimeendelea kukua na kutoa
mchango mkubwa katika kupunguza umaskini, ambapo zaidi ya Watanzania
milioni moja wamejiajiri katika shughuli hizo.
Hata hivyo katika
kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010 - 2015, Ibara ya 56
(d) ambayo pamoja na mambo mengine, inasisitiza juu ya kuwawezesha
wachimbaji wadogo kupata mikopo na mitaji, Wizara imeendelea kutoa
mikopo ya masharti nafuu na ruzuku kwa wachimbaji wadogo kupitia Benki
ya TIB.
Alisema mwezi Aprili,
2014 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alikabidhi hundi zenye jumla ya dola za
Marekani 537,000 sawa na shilingi milioni 880.68 kwa miradi kumi na moja
(11) ya wachimbaji wadogo ambayo ilikidhi vigezo vya kupata ruzuku.
Pia Wizara inatarajia
kuipatia miradi mingine 18 ya wachimbaji wadogo mikopo yenye jumla ya
shilingi bilioni 2.3 ifikapo mwishoni mwa mwezi Juni, 2014.
"Nawasihi wachimbaji
wadogo kuandaa michanganuo yao ya miradi kwa ajili ya kuomba mikopo na
ruzuku kupitia TIB ili watakaokidhi vigezo wapate ruzuku ama mikopo kwa
ajili ya kuendesha shughuli zao za uchimbaji mdogo kwa tija. Wachimbaji
wadogo wanashauriwa kupata ushauri wa bure wa kitaalamu kutoka Shirika
la Taifa la Madini (STAMICO),"alisema.
Hata hivyo aliongeza
kuwa wizara itaendelea kushirikiana kwa karibu sana na wachimbaji wadogo
waaminifu watakaotumia vizuri ruzuku wanazopewa na watakaorejesha
mikopo na kulipa kodi za Serikali.
Alisema ili kuendelea
kuwawezesha wachimbaji wadogo kwa mitaji na mikopo, Wizara imetenga
kiasi cha sh. bilioni 2.5 katika Bajeti yake ya mwaka 2014/15 kwa ajili
ya kukopesha wachimbaji hao.
Aidha katika juhudi za
kuendeleza shughuli za uchimbaji mdogo, kwa mwaka 2013/14 wizara
iliendelea kutoa mafunzo kwa nadharia na vitendo kwa wachimbaji wadogo
ambapo jumla ya wachimbaji wadogo 420 walipatiwa mafunzo katika maeneo
ya Handeni na Kilindi (250), Musoma (90) na Tunduru (80).
Aliongeza kuwa katika
mwaka 2013/14 jumla ya maeneo 10 yenye ukubwa wa hekta 67,677.61
yametengwa kwa ajili ya wachimbaji wadogo. Maeneo hayo ni Nyamwironge
(Kakonko), Ibaga (Mkalama), Makanya (Same), Mwajanga (Simanjiro), Itumbi
B na Saza (Chunya), Ilujamate (Misungwi), Kalela/Kigogwe/ Samwa
(mpakani mwa Wilaya za Kasulu, Buhigwe na Kigoma Vijijini), Maguja
(Nachingwea) na Nyangalata (Kahama/ Nyang'hwale).
Pia jumla ya maeneo
yaliyotengwa hadi sasa kwa ajili ya wachimbaji wadogo ni 25 yenye ukubwa
wa kilomita za mraba 2,166.24. Aidha, jumla ya viwanja 8,800 vyenye
ukubwa wa jumla ya kilomita za mraba 2,047.14 vimegawiwa kwa wachimbaji
wadogo.
"Katika mwaka 2014/15,
wizara itaendelea kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kadri
itakavyoonekana inafaa pamoja na kuongeza ajira kwa wachimbaji wadogo,
utengaji wa maeneo unalenga kupunguza migogoro ya maeneo kati ya
wachimbaji wadogo na wakubwa,"alisema.
Waziri Muhongo
aliwashukuru viongozi wote wa dini nchini kwa kukubali kushirikiana na
Wizara ya Nishati na Madini katika kuelimisha jamii kwa kauli mbiu
isemayo "Uendelezaji wa Rasilimali za Gesi Asilia, Mafuta na Madini kwa
Amani na Maendeleo ya Nchi Yetu."
Alisema kupitia
viongozi hao wizara imeendelea kuelimisha jamii juu ya rasilimali zake
katika makongamano mbalimbali nchini ambapo alivishukuru vyombo vya
habari na wadau wengine kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati na Madini
katika kutoa habari na kuelimisha wananchi juu ya uendelezaji wa
rasilimali zetu kwa manufaa ya Taifa.
"Nawaomba viongozi wa
dini na wadau wengine tuendelee kushirikiana ili kuleta maendeleo
endelevu kupitia rasilimali za nishati na madini. Napenda kuwahakikishia
kuwa Wizara ya Nishati na Madini haitarudi nyuma katika kutafuta
ufumbuzi wa matatizo na changamoto mbalimbali zinazoikabili na
itaendelea kushirikisha jamii na wananchi kwa ujumla katika hatua zake
za utekelezaji,"alisema Profesa Muhongo.
Chanzo;Majira
0 comments:
Post a Comment