Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Kumekuwa na mvutano mkubwa katika vikao vya mashauriano kati ya
 Serikali na Kamati ya Bunge ya Bajeti, ambao pamoja na mambo mengine 
unaelezwa kuchangiwa na hatua ya Serikali kukataa kuweka wazi vyanzo vya
 mapato kwa wajumbe wa kamati hiyo.
                
              
Kutokana na hali hiyo, majadiliano kuhusu mwelekeo
 wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2014/15, yamejikita katika 
makadirio ya matumizi pekee ambayo ni Sh19 trilioni, bila kufafanua 
fedha hizo zinatarajiwa kutoka katika vyanzo vipi.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo zinasema 
mvutano baina ya timu ya Serikali inayoongozwa na Waziri wa Fedha, Saada
 Nkuya Salum kwa upande mmoja na Kamati ya Bajeti inayoongozwa na Mbunge
 wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge ni dhahiri hakuna makubaliano
 ambayo yamefikiwa hadi sasa.
Wajumbe wa kamati hiyo wamekuwa wakitaka kufahamu 
vyanzo vya mapato ili kujiridhisha iwapo Serikali imezingatia ushauri wa
 Bunge kuhusu kuongeza vyanzo vipya, badala ya kuongeza kodi katika 
vyanzo vilevile kila mwaka.
“Tunashangazwa na makadirio ya matumizi ya Sh19 
trilioni kwa mwaka ujao wa fedha wakati wameshindwa (Serikali) kukusanya
 Sh18 trilioni na kusababisha upungufu wa fedha katika bajeti ya sasa. 
Wakijitahidi watamaliza mwaka huu wa fedha (Juni 30), wakiwa na upungufu
 wa zaidi ya Sh600 bilioni, sasa tunataka kujua ni vyanzo gani 
vitatumika kupata hizo trilioni 19?”
Chanzo kingine kilisema madai ya wabunge kutaka 
kufahamu vyanzo vya mapato yanatokana na kupewa taarifa za siri kwamba 
Serikali inakusudia kuongeza kodi katika vyanzo vilevile vya miaka yote,
 vikiwamo sigara, mafuta, soda na bia, hali ambayo walihisi kuwa ni 
kupigwa teke kwa mapendekezo waliyoyatoa mwanzoni mwa mwaka jana.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima 
alipoulizwa sababu za Serikali kuficha vyanzo vyake kwa wabunge kupitia 
ujumbe mfupi wa maandishi ya simu alijibu: “Nashauri swali hilo 
lielekezwe kwenye chanzo chako kwa kuwa mimi sina taarifa hizo.”
Naibu Spika wa Bunge Job Ndugai alisema taarifa 
zilizopo ni kwamba Kamati ya Bajeti na Serikali walikuwa wakiendelea na 
majadiliano na kwamba vikao husika vitaendelea leo... “Hakuna taarifa 
zozote rasmi kutoka ndani ya kikao hicho, tusubiri maana Alhamisi siyo 
mbali tutafahamu tu, tuwe na subira.”
Kabla ya kuundwa kwa Kamati ya Bajeti, Chenge 
aliongoza Kamati Maalumu iliyoundwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda 
kuchunguza mwenendo wa ukusanyaji wa mapato ya Serikali. Iliwasilisha 
taarifa iliyobaini madudu katika mfumo wa bajeti.
Katika ripoti yake, kamati hiyo ilibainisha kuwapo
 kwa udhaifu katika ukusanyaji wa mapato na kwamba kwa mwaka wa fedha 
2012/13 pekee, Serikali ilipoteza Sh3.95 trilioni kutokana na kasoro 
zilizopo.
Mapendekezo ya Bunge
                
              Ripoti hiyo iliyowasilishwa kwa Spika Makinda 
Februari 8, mwaka jana na baadaye kuwasilishwa serikalini, ina 
mapendekezo ya vyanzo vipya 24 vya mapato ambayo Chenge alisema kama 
yangetekelezwa yangeiwezesha Serikali kupata ziada ya Sh14.86 trilioni 
katika bajeti zake za 2014/15 na 2015/16
Vyanzo hivyo ni pamoja na uvuvi katika eneo la Bahari Kuu ambalo
 lilitajwa kuwa moja ya maeneo ambayo yamekuwa yakiikosesha Serikali 
mabilioni ya shilingi kutokana na meli za kigeni kuvua kiholela bila 
kukaguliwa.
Uchambuzi wa kamati hiyo ambayo wajumbe wake wengi
 ndiyo wanaounda Kamati ya Bajeti, ulionyesha kuwa Sheria ya Mamlaka ya 
Uvuvi wa Bahari Kuu ya 1998 ni kikwazo cha upatikanaji wa kiasi cha 
Sh352 bilioni kila mwaka kutokana na kutokuwa na kifungu cha kutoza 
mrabaha.
Pia ilitaja miradi ya gesi kwamba baada ya yote 
kukamilika, likiwamo bomba la Mtwara hadi Dar es Salaam, inaweza 
kuliingizia taifa Sh716.61 bilioni kwa miaka mitatu kuanzia 2015 – 2017.
“Kwa mfano, kiasi kilichogundulika ni futi za 
ujazo trilioni 32 ambazo ni sawa na mapipa bilioni 6 ya mafuta. Kwa bei 
ya sasa gesi hii ina thamani ya Dola za Marekani bilioni 660,” alisema 
Chenge.
Alisema iwapo mgawo wa Serikali ni angalau 
asilimia 10 na ikaamua kuutumia kama dhamana au mauzo ya mbele 
(collateral or forward sale), itapata Dola za Marekani bilioni 6.6, sawa
 na Sh10.56 trilioni ambazo zinaweza kutumika katika bajeti za 2014/2015
 na 2015/2016.
Kamati hiyo pia ilibaini kwamba iwapo Serikali 
ingetimiza ahadi yake ya kuliwezesha Shirika la Petroli Tanzania (TPDC),
 kutumia fursa ya uwekezaji kwa asilimia 20 katika mkataba wa utafutaji 
wa mafuta wa Mnazibay zinaweza kupatikana Sh33.8 bilioni kwa mwaka.
Makaa ya mawe yalitajwa kuwa yanaweza kusaidia 
kuokoa kiasi cha Sh1.1 trilioni kwa mwaka, kiasi ambacho kinatumiwa sasa
 na Serikali kwa ajili ya kugharamia mafuta ya kuzalisha umeme.
Ilishauriwa kuwa Serikali inapaswa kufanya uamuzi kutumia gesi kama chanzo cha mapato kwa kuweka dhamana kiasi kidogo cha gesi.
Walipendekeza kuanzishwa kwa tozo mpya katika 
huduma za usafirishaji wa fedha kupitia simu za mkononi, hivyo 
kuiwezesha nchi kuingiza Sh25.5 bilioni kwa mwaka na uanzishwaji wa ada 
ya utumiaji wa kadi za simu za mkononi yenye uwezo wa kuingiza Sh255.5 
bilioni kwa mwaka.
Kauli ya Serikali
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alisema 
katika bajeti ijayo, Serikali itachukua hatua za kuongeza mapato yake 
ili kukwepa upungufu wa fedha uliojitokeza katika bajeti ya 2013/14 na 
kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Tutakuja na mapendekezo ya jinsi ya kukusanya 
mapato ya ndani, maana kujitegemea kuna heshima yake na kunachochea 
maendeleo. Tutakuja na mapendekezo hayo na tunaomba wananchi na wabunge 
watuunge mkono” alisema Nchemba.
Alisema hatua nyingine ni kuimarisha usimamizi wa fedha 
zinazopatikana licha ya kuwa ni kidogo. “Tutakavyotengeneza Sheria ya 
Bajeti, lengo lake ni kuimarisha usimamizi wa fedha zote zinazotumika 
ili kuleta thamani ya fedha iliyokusudiwa” alisema Nchemba.
Alisema jambo lingine ni kuhakikisha fedha ambazo 
hazitokani na kodi zinatumika kutekeleza miradi iliyokusudiwa na si 
vinginevyo.
“Wananchi wanaweza kuchanga fedha nyingi kwa ajili
 ya ujenzi wa shule, jengo linapokamilika wahandisi hujitokeza na kudai 
kuwa limejengwa chini ya kiwango. Katika eneo hili kuna upotevu mkubwa 
wa fedha ambao tutaudhibiti,” alisema.
Nchemba aligusia suala la ukwepaji wa kodi na 
kusema nchi imekuwa ikiwategemea wafanyabiashara wadogo na wafanyakazi 
pekee na kusema watakuja na njia nyingine ya kuongeza vyanzo vya mapato.
“Tunalenga kupunguza kodi kwa wafanyakazi ili 
kuwapunguzia gharama za maisha ambazo zinapanda kila siku. Pia tutaziba 
mianya ya ukwepaji wa kodi,” alisema.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment