IMEELEZWA kuwa kuna
uwezekano mkubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Dodoma kuchimba maji ardhini na
kuendesha kilimo cha umwagiliaji licha ya mkoa huo kijiografia kuwa na
hali ya ukame.
Hayo yalielezwa jana
mkoani hapa na Mkurugenzi wa Utafiti wa Kilimo na Maendeleo Kanda ya
Kati, Leon Mroso wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya kilimo
cha umwagiliaji.
Mroso alisema kuwa Mkoa
wa Dodoma ni moja kati ya mikoa ambayo hupata mvua kidogo huku ardhi
yake ikiwa na maji mengi ambayo alisema endapo yatachimbwa yanaweza
kusaidia kilimo cha umwagiliaji.
“Dodoma inapata mvua milimita 500-600 kwa mwaka ambapo kwa takwimu hizo hiyo ni mvua kidogo sana...
“Kutokana na kuwepo kwa
maji mengi ardhini kuna uwezekano mkubwa wa kutumia mashine za kuvuta
maji hayo kwa ajili ya umwagiliaji,”alisema Mroso.
Aidha aliitaka jamii
nchini kujiunga katika vikundi kwa lengo la kupata mkopo katika taasisi
za kifedha nchini ili kuwawezesha kuchimba visima na kununua mashine za
kuvutia maji pamoja na kufanikisha kilimo cha umwagiliaji mkoani hapo.
“Kama vikundi
vitajiunga mfano pale ambapo hakuna umeme wakanunua vipande vya umeme
jua kama 60 hivi wanaweza kuendesha mashine za kuvuta maji na kufanya
kilimo cha umwagiliaji kuwa na tija kubwa,” alisema.
Hata hivyo aliwataka
watafiti nchini kujenga tabia ya kushirikiana na wadau mbalimbali katika
kutoa elimu kwa jamii hasa wakulima ili kuweza kutimiza lengo la kilimo
hicho ikiwa ni pamoja na kuvuna maji ya mvua.
Chanzo:Majira
0 comments:
Post a Comment