Home » » WAFANYAKAZI CHEMBA WATISHIA KUGOMA

WAFANYAKAZI CHEMBA WATISHIA KUGOMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAFANYAKAZI wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma wanakusudia kugoma kufanya kazi baada ya serikali wilayani humo kuzuia mishahara yao kwa miezi mitatu sasa kwa madai ya kutochangia sh 50,000 za mbio za Mwenge.
Uamuzi wa wafanyakazi hao wakiwemo wa idara nyeti ya Afya, Elimu, Kilimo na Maji katika halmashauri hiyo kugoma unakuja kutokana na mateso ya kufungiwa mishara yao benki hadi watakapotoa fedha hizo.
Wakizungumza mwishoni mwa wiki kwa sharti la kutotajwa majina yao kuhofia utumishi wao, baadhi yao walisema uongozi ukiongozwa na Mkuu wa Wilaya Francis Mtinga na Mkurugenzi Dk. William Mafwere, umekuwa ukitumia mabavu kuwanyanyasa katika haki zao.
Wakithibitisha unyanyasaji wanaofanyiwa, wafanyakazi hao walionyesha barua kumbukumbu namba CDC/A,60,3VOL1,76 ya tarehe 14/7/2014 kichwa cha habari, ‘Malipo ya sherehe za mwenge’ iliyosainiwa na Mselem Aziz kwa niaba ya Mkurugenzi.
Katika barua hiyo, uongozi huo ulitoa tahadhari kwa wafanyakazi hao kulipa fedha hizo haraka kabla ya 20/7/2014, vinginevyo mishahara yao itasimamishwa hadi hapo watakapolipa deni, jambo linalotekelezwa tangu Julai hadi sasa.
Walipotafutwa kutoa ufafanuzi wa madai hayo, Mkurugenzi na Mkuu wa Wilaya walipishana katika kauli zao, wakati Dk. Mafwere akidai hakuna kitu kama hicho kwake, DC Mtinga alikiri kuwepo zoezi hilo kwa lengo la kulipa deni la fundi nguo.
"Sikiliza bwana usiniulize upuuzi huo, kwangu hakuna kitu kama hicho…kwanza wewe nani hadi uulize mambo kama hayo,” alihoji Dk. Mafwere na kudai anaingia kanisani kusali.
DC Mtinga, alisema uamuzi wa kuzuia mishahara hiyo, inatokana na watumishi hao kutokuwa na ubinadamu dhidi ya fundi aliyechukua jukumu la kuwashonea suti nzuri kwa bei hiyo bila kulipwa ujira wake.
"Kumbuka gharama ya suti leo hii sio shilingi 50,000 lakini mafundi hawa tena waliosafiri toka Shinyanga na Dodoma walivyojikufuru na kushona kwa bei hiyo halafu wasilipwe hata shilingi!..haiwezekani nao ni binadamu bwana!” alisema DC huyo.
Wilaya ya Chemba ni miongoni mwa Wilaya mpya zilizoanzishwa nchini mwaka juzi ikigawanyika kutoka Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa