Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Profesa Mwesiga Baregu.
Baadhi ya wanasiasa, wajumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, wanaharakati na wanasheria wamekosoa zoezi la upigaji kura katika kupitisha rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba (BMK), wakieleza liligubikwa na hila, kampeni, uchakachuaji, mabavu, vitisho na kwamba, rasimu hiyo haiendani na matakwa ya wananchi wa Zanzibar.
Baadhi wameeleza kuanza kuchambua rasimu hiyo kifungu kwa kifungu ili kupima uzito na tafsiri ya Ibara 28 zilizofutwa kabla ya kuueleza umma namna maoni yao yalivyochakachuliwa.
Wamesema upitishwaji wa rasimu hiyo ulitawaliwa na mabavu na Watanzania siyo wajinga kwa kuwa wanaona kinachoendelea hivyo wataamua.
PROF. BAREGU: WATANZANIA NDIYO WAAMUZI
Aliyekuwa Mjumbe wa Tume hiyo, Profesa Mwesiga Baregu, alisema Watanzania siyo Chadema wala CCM, bali ni wengi, ambao waliona kilichojiri ndani ya Bunge hilo, hivyo, wataamua.
Alisema uongozi BMK umeshindwa kuwafanyia kazi na kuheshimu maoni ya wananchi, ambao waliahidiwa kupata katiba itakayobeba maoni na kutunza maslahi yao kwa jumla.
Profesa Baregu alisema mchakato wa katiba ulivyoanza chini ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba iliyofanyiwa marekebisho, ulilenga kukusanya maoni ya Watanzania ili kupata katiba inayotokana na maoni yao.
“Malengo yaliyowekwa mwanzoni siyo yaliyofikiwa. Tume iliwasikiliza Watanzania na kutoa rasimu ya kwanza na ya pili iliyosheheni maoni yao. Lakini BMK limeyapindua na kutoa katiba, ambayo haikutakiwa na wengi,” alisema na kuongeza: “Watanzania mbele ya safari wataamua.”
“Uamuzi wa kupiga kura ya ndiyo na hapana haukuwa wa msingi, bali maridhiano ya wote ndani ya jamii. Hakukua na haja ya kura ya kushinda au kushindwa. Ndiyo maana Tume ilitengeneza rasimu kwa maridhiano,” alisema.
Alikosoa uamuzi wa kumuweka Mwenyekiti wa BMK, Samuel Sitta, ambaye ameongoza Bunge hilo kama Bunge la kawaida lenye wapinzani na chama tawala na kuona ni suala la ushindani baina ya pande mbili.
MUASISI SMZ: HAIENDANI NA MATAKWA YA WANZANZIBARI
Muasisi wa CCM Zanzibar, Hassan Nassoro Moyo, amesema rasimu iliyopitishwa haiendani na matakwa ya wananchi wa Zanzibar.
Alisema kitendo kilichobaki kwa wananchi ni kuikataa rasimu hiyo katika kura ya maoni na kusema nguvu za wajumbe wa Bunge hilo walioipitisha, zimekwisha na kwamba, hatua iliyobaki ni ya wananchi.
Alisema kitendo alichokifanya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, anakiunga mkono, kwani ni cha kijasiri katika kutetea maslahi ya Zanzibar.
WANASHERIA ZNZ: TULITARAJI MARIDHIANO
Raisi wa Chama cha Wanasheria Zanzibar, Awadhi Ali Saidi, alisema walitegemea mchakato wa katiba utajenga maridhiano, lakini imeonekana kuleta mfarakano, ubaguzi na vitisho.
Alisema uongozi wa BMK umechangia Taifa kugawanyika, kwani umeshindwa kuleta maridhiano kuhusiana na rasimu iliyopendekezwa na wananchi waliowengi.
WANANCHI: KATIBA NI YA TANGANYIKA
Dadi Kombo Maalim alisema katiba iliyopitishwa ni ya Tanganyika na siyo ya Wazanzibari, hivyo hakubaliani nayo, kwani wajumbe wa BMK walioipigia kura wamejali maslahi yao na siyo ya wananchi.
Alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutoiunga mkono rasimu hiyo, ambayo inaweza kuipeleka nchi pabaya zaidi, huku akiwataka wananchi wenzake kutoiunga mkono.
Mussa Mbarouk alisema Wazanzibari wamechakachuliwa na hakukuwa na uwazi na ukweli katika rasimu hiyo, hivyo hawakubaliani nayo na wapo tayari kuikataa.
Mwakilishi wa Jimbo la Kiwani, Pemba (CUF), Hija Hassan Hija, alisema katiba hiyo ni ya udanganyifu na haikupata theluthi mbili ya Wazanzibari, bali CCM wametumia mabavu ili kuwakandamiza.
Alisema endapo rasimu hiyo itapitishwa kuwa katiba rasmi baada ya kura ya maoni, wananchi wategemee kudhalilishwa, kuonewa na kukandamizwa.
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Dimani (CCM), Hafidhi Ali Tahir, alisema rasimu hiyo imekwenda katika utaratibu mzuri na hakuna ghilba wala udanganyifu, kwani michango ilikuwa wazi na haikuwa ya siri.
Aliwataka wananchi kujitayarisha kupiga kura ya ndiyo, kwani rasimu hiyo imewasaidia Wazanzibari zaidi kuliko Watanganyika, kwani mambo mengi waliyoyataka, yamo yakiwamo masuala ya gesi na mafuta na ina manufaa kwa taifa.
Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) Zanzibar, Zeudi Abdillah Mvano, alisema kuna utata mtupu katika rasimu hiyo, ambayo haijazingatia matakwa ya Wazanzibari.
Alisema idadi zililotolewa bungeni za wananchi waliopiga kura siyo sahihi, kwani zimekuwa zikikwazana za awali kabla ya kura na baada ya kupigwa kura, ambazo zilionekana kuzidi.
Mvano alisema rasimu hiyo siyo sahihi, kwani haijapata ridhaa ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar na Waziri wa Katiba na Sheria wa Zanzibar, ambao hawajaiunga mkono.
DK. SLAA: ULIGUBIKWA NA HILA
Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willibrod Slaa, alisema watawaelimisha wananchi ili watambue namna maoni yao waliyotoa kwenye Tume yalivyochakachuliwa na athari za rasimu ya BMK.
Alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, amewadanganya Waislamu kwa kuwa Ibara ya 40 ya rasimu ya BMK inaeleza bayana kwamba, serikali haitajihusisha na masuala ya dini na kwamba, kueneza dini ni jukumu la dini husika.
Alisema kwa Ibara hiyo, Pinda ameudanganya umma kwa kuwa sheria haiwezi kuvunja katiba akisema 'Katiba inakataza, sheria itaweza?'
Dk. Slaa alisema hivi sasa wanasheria wanachambua kifungu kwa kifungu cha rasimu hiyo ili kuainisha uzito na tafsiri ya kilichopendekezwa kisha wataueleza umma uhalisia wa kilichotokea.
Kuhusu zoezi la upigaji kura, alisema liligubikwa na kila aina ya hila, ikiwamo kampeni za wazi kabla ya mjumbe kupiga kura.
“Uliona kwamba, mtu anasimama kabla hajasema ndiyo au hapana anatoa kwanza sifa ya hiyo rasimu. Kulikuwa na kampeni ya wazi wakati wa upigaji kura na mwenyekiti alikaa kimya,” alisema.
Dk. Slaa alisema upigaji wa kura kwa njia ya mtandao na simu ulilenga uchakachuaji kwa kuwa hakukuwa na mfumo mahsusi wa kusimamia.
Alisema Chadema ina taarifa za uhakika kwamba, zoezi hilo lilisimamiwa na Idara ya Usalama wa Taifa na kwamba, Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta, alisimamia zoezi la kuhesabu kura hadi usiku wa manane.
Alisema inashangaza zoezi la kuhesabu kura za wajumbe wachache ndani ya Bunge linachukua muda kuliko zoezi la kuhesabu kura za uchaguzi mkuu uliohusisha watu wengi nchi nzima.
“Jambo lingine lililoniogofya ni jinsi watu hao (wajumbe), wanaoweza kutoa upotoshwaji wa hali ya juu kwa kusema rasimu ina haki za makundi kadha wa kadha wakati Ibara ya 20 ya rasimu hiyo hiyo ikieleza kuwa haki hizo haziwezi kudaiwa mahakamani. Hii ni sawa na kukupa haki kwa mkono wa kulia na kuinyang’anya kwa mkono wa kushoto. Kwa hiyo, sisi hatuwezi kuruhusu upotoshwaji huu,” alisema.
Alisema haki hizo zilikuwa zinazuiwa kudaiwa mahakamani na katiba ya mwaka 1977, Ibara ya 6 na 7 na kwamba, kilichofanyika ni kuhamisha ibara hizo na kuzipeleka ibara ya 20.
“Udanganyifu na upotoshwaji huu ni uongo wa mchana kweupe. Wanasema kilichojadiliwa na kupitishwa ni rasimu ya Tume ya Jaji Warioba, lakini wamefuta Ibara 28, ambazo zilikuwa moyo wa rasimu na kuingiza 42, ambazo siyo maoni ya wananchi. Kufuta Ibara hizi kumebomoa msingi mzima wa mawazo ya wananchi. Hili hatuwezi kukubali,” alisema.
THDRC: KATIBA IMEPITISHWA KIMABAVU
Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umesema umeshangazwa na ubabe na mabavu yaliyotumika katika kupitisha katiba inayopendekezwa, huku kukiwa na utata mkubwa katika theluthi mbili ya Zanzibar.
Mratibu wa THRDC Taifa, Onesmo Olengurumwa, alisema awali walitoa hesabu kuwa kura ni 210, lakini ghafla zikaongezeka na kufika 219, huku kura za waliopiga kwa njia mbalimbali hazikuwekwa wazi.
“Ni changamoto kwa kuwa wao wana nguvu, wana wingi, wanajiendesha watakavyo. Hatuna uwezo wa kufanya mabadiliko leo au kesho. Lakini Watanzania wanaangalia kwa kuwa viongozi wanaliingiza Taifa katika machafuko na mpasuko mkubwa,” alisema.
“Wasifikiri watu wamenyamaza, bali wanatafuta upenyo ili kusema kinachofanyika ni kinyume cha sheria…Katiba haijapitishwa kwa mujibu wa sheria, bali watakavyo. Wameshangilia sana kwa kuwa wanajua ni kitu hakiwezekani, bali kimelazimishwa,” alisema.
Alisema kwa mazingira yaliyokuwapo, wamejitahidi kupata theluthi mbili kwa kuwa wasingekubali watoke bila katiba na kwamba, wajumbe wengi wako mafichoni na wametishiwa kuuawa.
Olengurumwa alisema Asasi za Kiraia (Azaki) wanatafakari kuona nini cha kufanya kwa kuwa hali hiyo haivumiliki na kwamba, kuanzia sasa hawatawaacha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) pekee, bali wataungana kwa kuwa nchi ni ya wote.
MNYIKA: MAHARAMIA WAMEPITISHA KATIBA HARAMU
Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika, amesema uharamia uliofanywa na BMK umelipasua Taifa na kwamba, mpasuko huo unaweza kuwa mgogoro hasi wenye madhara kwa wananchi au wenye kuleta mabadiliko chanya.
“Maharamia wanashangilia kilevi katika BMK baada ya kukamilisha uharamia dhidi ya rasimu ya katiba ya wananchi kwa kupata theluthi mbili kwa njia kiharamia. Katiba haramu, katiba ya maharamia, katiba ya mafisadi, katiba ya CCM wahafidhiana na mawakala wake, inapaswa kupingwa mtaani na mahakamani kwa mbinu mbalimbali,” alisema.
Alisema rasimu hiyo itapingwa kwa mikutano, migomo, maandamano, mashtaka au katika sanduku la kura.
“Theluthi mbili ilianza kutafutwa tangu wakati wa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, tulipinga muundo wa Bunge Maalumu na uteuzi wake; madhara yake yamedhihirika sasa,” alisema.
Aliongeza: “Rais Kikwete akaongezea udhaifu huo kwa kutumia madaraka vibaya kuteua wanaCCM mahafidhina na mawakala wao kwa wingi katika uteuzi wa 201 kuongezea katika hodhi haramu ya wabunge na wawakilishi wa chama chake.”
Alisema Sitta amekamilisha uharamia huo kwa marekebisho haramu ya kanuni za BMK, ambayo yaliruhusu kura za nje ya Bunge hilo na mianya mingine ya wizi wa kura.
“Sitta na maharamia wenzake kama wameshindwa hata kuelewa waraka wa viongozi wa dini na kuuita kuwa “hauna utukufu wa Mungu na wa kipuuzi”, ni wazi wamelewa madaraka wasaidiwe kwa kupumzishwa,” alisema.
MBOWE: UKAWA KUENDELEA NA MAPAMBANO
Mwenyekiti wa Ukawa, Freeman Mbowe, amesema umoja huo utaeandelea kupigania rasimu ya katiba iliyopendekezwa na Tume ya Warioba na siyo rasimu iliyopitishwa na Bunge hilo.
Akizungumza na NIPASHE, Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema alisema rasimu iliyojadiliwa na kupitishwa hawaitambui kwa kuwa imeundwa kwa mawazo ya wabunge wa CCM na vibaraka waliokuwapo ndani ya Bunge hilo.
Alisema Ukawa itakaa chini na kutoa tamko kwa wananchi jinsi ya utani na dhihaka vilivyofanyika bungeni na kusababisha kupitisha rasimu, ambayo haina mawazo ya wananchi.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment