MKUU wa Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Christopher Kangoye amewataka vijana 120 wa wilaya hiyo waliopata ajira ya kupitia kampuni ya Suma JKT, kuzingatia uadilifu na uzalendo ili wawe na tija kwa taifa.
Vijana hao walipata ajira baada ya kumaliza mafunzo ya mgambo katika Kata ya Kimagai nje kidogo ya Mji wa Mpwapwa.
Kati ya vijana 166 waliohitimu mafunzo hayo kwa ustadi, vijana 120 walibahatika kuingia kwenye ajira moja kupitia SUMA JKT ambalo ni tawi la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) hapa nchini ambalo limejikita katika uzalishaji.
Kangoye, ambaye alikuwa Kamanda wa mafunzo na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Wilaya, aliwataka vijana kuwa waadilifu na kuonesha uzalendo kwa nchi yao.
Alisema mafunzo ya mgambo na JKT yamekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi hasa vijana ambao kwa sasa vijana wengi wamekuwa wakikosa uzalendo kadri siku zinavyozidi kusonga mbele na kutishia mustakabali wa amani ya taifa kutokana na uzalendo kupungua.
Alisema ajira 120 ambazo vijana hao wamezipata zimesaidia kupunguza idadi kubwa vijana wa wilaya hii ambao walikuwa hawana ajira rasmi za kujipatia kipato na kuendesha maisha yao.
Mratibu wa Mafunzo na Mshauri wa Mgambo wilayani Mpwapwa, Sajini Taji Wiliam Emmanuel alisema jumla ya vijana 370 walianza mafunzo hayo, hata hivyo waliobahatika kumaliza ni vijana 166 na waliopata ajira ni vijana vijana 120.
Aliitaka jamii kuondokana na dhana potofu kuwa mafunzo ya mgambo ni mateso kwa jamii bali alisema mafunzo hayo yanawasaidia vijana kuwaweka katika mazingira mazuri kiafya.
Alisema vijana hao watasafiri Desemba 15, mwaka huu kuelekea Dar es Salaam ambapo watasambazwa maeneo mbali ya mikoa ya Tanzania bara.
Chanzo;Habari Leo
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment