Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri mkuu, Mizengo Pinda.
Waziri mkuu, Mizengo Pinda, aliliambia Bunge jana wakati
akiwasilisha hotuba ya muelekeo wa kazi za Serikali, makadirio ya
matumizi ya fedha ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Bunge kwa mwaka 2015/16
kuwa, mauaji hayo yamesababisha hofu kwa watu wenye ulemavu wa ngozi
pamoja na familia zao kuishi kwa hofu, mashaka na kushindwa kushiriki
kikamilifu katika shughuli za maendeleo.
“Vitendo hivi vimeleta taswira isiyo nzuri kwa nchi yetu
ikizingatiwa kwamba watu wengi ndani na nje ya nchi wanafahamu kuwa
Watanzania wanaishi kwa upendo, kuheshimiana na kuthamini amani, jambo
ambalo nchi nyingi zinaendelea kuiga,” alisema.
Alisema tangu mauaji hayo yalipoanza mwaka 2006, watuhumiwa 181
walikamatwa na kuhojiwa na kwamba kati ya yao 131 walifikishwa
mahakamani, ambapo 46 walifunguliwa kesi za kuua na kujeruhi na kwamba
kati yao washtakiwa 13 wamehukumiwa kifo.
Aidha, mshtakiwa mmoja alihukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa hatia
ya kujeruhi, wakati wengine 73 wameachiwa huru baada ya kukosekana
ushahidi wa kuwatia hatiani.
Kutokana na hali hiyo, Pinda alisema kuanzia mwaka 2006 hadi sasa
watu 43 wenye ulemavu wa ngozi wameuawa, huku mwaka huu pekee wakiwa
wameuawa watu tisa.
Alisema watuhumiwa sita hawajakamatwa na upelelezi wa kesi 10 bado
unaendelea, huku watuhumiwa wawili wakiuawa na wananchi kabla ya
kufikishwa polisi. Pinda alisema chanzo kikubwa cha mauaji hayo ni imani
za kishirikina kwa tamaa za kupata utajiri au chezo. “Mimi siamini
kwamba cheo, wadhifa, mali au utajiri hupatikana kwa njia haramu kama
hizo.
Utajiri hupatikana kwa kufanyakazi kwa juhudi na maarifa na siyo
vinginevyo…serikali itaendelea kupambana na watu wanaojihusisha na
vitendo hivyo kwa nguvu zake zote,” alisema. Awali, akizungumza bungeni
kabla ya kutoa hutuba, Pinda alisema Kanda ya Ziwa inaongoza kwa mauaji
ya watu wenye ulemavu wa ngozi, ambapo kati ya watu 43 waliouawa 41
wametoka katika kanda hiyo.
Ufafanuzi huo alitoa wakati alipokuwa akitoa majibu ya ziada katika
swali la msingi lililoulizwa na Mbunge wa Viti Maalum, Martha Umbulla
(CCM), ambaye alitaka kujua sababu za mauaji ya albino kuendelea licha
ya kwamba kumekuwa na juhudi za kukomesha vitendo hivyo.
Alisema ili kuelimisha na kuhamasisha wananchi wa mikoa hiyo
ikiwamo Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga, Kagera na Mara kuacha imani
hizo za kishirikina, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG)
pamoja na viongozi wa dini watatembelea na kuhamasisha wananchi wa
ameneo hayo kubadili tabia. Aliliambia Bunge kuwa tume hiyo ya haki za
binadamu na madhehebu ya dini yatatembelea kanda hiyo na kuzungumza na
wananchi na kutoa elimu inayolenga kuleta mabadiliko. Alisema serikali
ina amini kuwa kampeni hiyo pamoja kazi za mahakama itapunguza mauaji ya
albino nchini.
Vitendo vya kuwakata viungo albino vilianza 2006 kwa imani potofu
kuwa ni chanzo cha utajiri , mafanikio kisiasa na kiuchumi. Baadhi
wanaamini kuwa vinasaidia kupanda vyeo na kufanikiwa kazini.
BVR
Alisema matumizi ya mfumo wa kisasa wa Biometric Voters
Registration (BVR) katika maboresho ya Daftari la Kudumu la Wapira Kura
ulioanza Februari 23, mwaka huu, hautatumika kwa ajili ya kupiga au
kuhesabu kura.
"Napenda kulikumbusha Bunge lako na wananchi wote kwamba, Tanzania
itatumia mfumo wa BVR kwa ajili ya uandikishaji tu na hautatumika kwa
ajili ya kupiga au kuhesabu kura kama wengine wanavyoamini.
Hata hivyo, hakutoa sababu za kutotumia mfumo huo katika kupiga au
kuhesabu kura. “Wale wote wenye sifa watapiga kura kwa utaratibu wa
kawaida wa kutumia karatasi maalum na matokeo yatatolewa na kubandikwa
vituoni kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwenye chaguzi zilizopita.”
“Tume ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea kutoa elimu, taarifa na
ratiba kwa umma kuhusu zoezi la uandikishaji linavyofanyika katika
maeneo yote nchini,” alisema. Alisema Nec imeanza maandalizi ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2015 pamoja na maandalizi ya kupiga kura ya maoni ya
Katiba inayopendekezwa.
HALI YA SIASA
Akizungumzia hali ya siasa nchini, alisema imeendelea kuimarika,
demokrasia imeendelea kukua na mwamko wa wananchi kushiriki katika
shughuli za siasa umeongezeka. Alisema idadi ya vyama vya siasa vyenye
usajili wa kudumu imeongezeka kutoka 17 mwaka 2005/06 hadi 22 mwaka
2014/15. Aidha, alisema hadi kufikia Februari, 2015, vyama vingine nane
vimewasilisha maombi ya usajili wa muda.
KESI 10 KUBWA ZA RUSHWA
Kuhusu mapambano dhidi ya rushwa, Pinda alisema Taasisi ya
Kupambana na Kudhibiti Rushwa (Takukuru) inatakiwa kukamilisha uchunguzi
wa tuhuma 10 za rushwa kubwa, kuchunguza tuhuma 2,783 zilizopo na mpya
zitakazojitokeza 2015/16.
KERO ZA MUUNGANO
Pinda alisema kero 15 za Muungano zinajadiliwa na Kamati ya Pamoja
ya Serikali ya Muungano wa Tanzania (SMT) na Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar (SMZ).
Alisema kati ya hoja hizo, tisa zimepatiwa ufumbuzi na sita zipo katika hatua ya utatuzi.
Alizitaja hoja zilizo katika hatua ya utatuzi kuwa ni mgawanyo wa
mapato ambaio inajumuisha mgawo wa misaada kutoka nchi za nje na
misamaha ya mikopo.
Nyingine ni hisa za SMZ zilizokuwa katika Bodi ya Sarafu ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki na faida ya Benki Kuu. Alitaja nyingine
kuwa ni utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, ushiriki wa
Zanzibar katika taasisi za nje, ajira za Zanzibar katika taasisi za
Muungano, usajili wa vyombo vya moto na Tume ya Pamoja ya Fedha. Alisema
ni dhamira ya serikali mbili hizo kuzipatia ufumbuzi hoja hizo haraka
inavyowezekana.
UJENZI BANDARI MPYA Alisema ujenzi wa bandari kubwa kuliko zote
ukanda wa Afrika Mashariki na kati unatarajiwa kuanza 2015/16, eneo la
Mbegani, wilayani Bagamoyo.
NISHATI Waziri Mkuu Pinda alisema, serikali imekamilisha kwa
asilimia 84 utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi wa kufua umeme wa
Kinyerezi utakaozalisha megawati 150 kwa kutumia gesi asilia. Alisema
utekelezaji wa awamu ya tatu ya mradi huo utakaozalisha megawati 300
unaendelea.
GESI ASILIA
Alisema ugunduzi wa kiasi kikubwa cha gesi asilia nchini umeiweka
Tanzania katika orodha ya nchi zinazozalisha gesi asilia nyingi duniani
na kutoa matumaini makubwa ya kukuza uchumi. Alisema hadi kufika
Desemba, mwaka jana, gesi asilia yenye futi za ujazo trilioni 53.28
ilikuwa imegunduliwa na kazi ya utafutaji inaendelea.
Imeandikwa na Jacqueline Massano, Gaudencia Mngumi na John Ngunge, Dodoma
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment