Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na Mwandishi,Dodoma.
Mkoa wa Dodoma unakusudia kuandaa
kongamano la kuzitangaza fursa zilizopo katika mkoa huu baadae mwakani ili
kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza na kukuza uchimi na kuongeza
kipato cha wananchi wake.
Hayo yalielezwa jana hapa mjini
Dodoma na mchumi wa kamati ya maendeleo ya mkoa, Bwana Paulo Ngussa alipokuwa
akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake. Alisema, mkoa wetu wa Dodoma
inazo fursa nyingi ambazo bado hazijapata wawekezaji hivyo kamati ya maendeleo
ya mkoa huu kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa imekusudia kuandaa kongamano hilo
litakalofanyika mwanzoni mwa mwezi wa nane.
Alizita baadhi ya fursa hizo kuwa
ni uwekezaji katika sekta ya kilimo na mifugo ambapo alitaja ukulima wa zabibu
na ngozi toka machinjio ya Dodoma yanayozalisha ngozi za kutosha kibiashara.
Alisema kwa sasa zabibu zinalimwa hapa Dodoma lakini hakuna soko la uhakika
hivyo wangependa apatikane mwekezaji wa kujenga kiwanda cha kutengeneza juisi
au wani. Alienda mbali kidogo katika sekta ya kilimo kwa kubainisha kuwa, mkoa
huu wa Dodoma mvua zake ni chache sana na karibuni kipindi cha miezi tisa ni
ukame na watu wake hukaa bila shughuli za kufanya. Mkoa unakusudia wapatikane
wawekezaji katika mpango wa umwagiliaji ili wananchi wake waweze kujishughulisha
na kilimo cha umwagiliaji mfano mbogamboga nk.
Alitaja eneo jingi kuwa ni sekta
ya elimu ambapo mkoa wa Dodoma unao vyuo vingi vya elimu ya juu lakini lipo
tatizo kubwa la hosteli za wanafunzi na nyumba za watumishi. Kwa sasa nyumba
zilizopo Dodoma ni zile za asili ambazo haziwezi kukidhi haja ya jamii ya sasa,
alieleza mchumi huyo.
Pia eneo jingine ni la sekta ya
utalii ambapo hadi sasa Dodoma haina kumbi kubwa za kutosha za mikutano ya kitaifa na kimataifa. Pia mkoa
hauna hoteli kubwa za kiwango cha nyota tano. Alieleza kuwa pamoja na mkoa kuwa
ni makao makuu tarajiwa ya nchi, na pia kufanyika kwa vikao vya bunge lakini
lipo tatizo kuwa la kumbi za mikutano kwa viongozi na watendaji wa serikali. “Wageni
wanaotaka kuja kuwaona viongozo Dodoma lazima wavizie wakati wa shughuli za
bunge na kurejea Dar es Salaam”, alifafanua hivyo.
Alimalizia kwa kutaja pia sekta
ya madini ambayo inakuwa kwa kasi hapa nchini. Maeneo ya milima ya Mpwawa
yamegundulika kuwa na aina mbalimbali za madini lakini bado fursa hiyo haija
tangazwa vya kutosha.
Kulingana na takwimu za mwaka
2013 za kipato cha mtu mmoja mmoja kwa mkoa wa Dodoma ni shilingi 757,696.00 kwa
mwaka, ambapo mikoa mingine mfano Dar es Salaam ni zaidi ya milioni moja.
Imeelezwa pia kuwa maadalizi hayo yanatarajiwa kugharamiwa na wadau wote wa
maendeleo hapa mkoani na inakadiriwa kiasi cha shilingi milioni mia nane
kufanikisha kongamano hilo.
0 comments:
Post a Comment