Home » » UANDIKISHAJI WAPIGAKURA KUANZA LEO MBEYA, DODOMA KESHO.

UANDIKISHAJI WAPIGAKURA KUANZA LEO MBEYA, DODOMA KESHO.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Mstaafu Damiani Lubuva.

Wakati uandikishaji wapigakura katika daftari la kudumu la wapigakura kwa kutumia mfumo mpya ya Biometric Voters Registration (BVR) ukianza leo jijini Mbeya, mchakato huo utaanza mkoani Dodoma kesho.
 
Awali, mchakato huo ulipangwa kuanza leo mkoani humo, lakini ulishindikana kutokana na waandikishaji wa ngazi mbalimbali kuchelewa kupata mafunzo.
 
Mratibu wa Uandikishaji mkoani humo, Paulo Ngusa, alisema utoaji mafunzo ya uandikishaji kwa ngazi ya maafisa waandikishaji wasaidizi na maafisa uchaguzi wa halmashauri kwa mkoa wa Dodoma yalifanyika Jumatatu na Jumanne, wiki iliyopita na kwamba, ndicho kilikuwa kitu cha kwanza.
 
Alisema baada ya kupata mafunzo, maafisa hao walienda katika wilaya zao na kuanza kutoa mafunzo kwa ngazi ya maafisa waandikishaji wasaidizi katika ngazi ya kata, ambayo yalifanyika Alhamisi na Ijumaa wiki iliyopita.
 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa, Isdory Mwalongo, alisema mchakato huo kwa wilaya yake utaanza Mei 21, mwaka huu, kutokana na kuchelewa kupata mafunzo.
 
MBEYA
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Mussa Zungiza, alisema maandalizi ya uandikishaji wapigakura yamekamilika na kwa hiyo mchakato huo utaanza leo.
 
Alisema waandikishaji 430 tayari wamepewa mafunzo ya namna ya kuandikisha wapigakura kwa mfumo huo na kwamba, ofisi yake imejipanga kuhakikisha mchakato unakamilika bila matatizo.
 
“Tumekuwa tukitoa mafunzo kwa waandikishaji wapigakura wapatao 430 na hivi leo (jana) tunafunga mafunzo tukiwa tumejiridhisha kuwa wataifanya kazi hii kwa ufanisi mkubwa,” alisema Zungiza.
 
Alisema mchakato huo katika halmashauri hiyo utafanyika kwa awamu tatu; ya kwanza ambayo inaanza leo itakuwa kwenye kata 10 zenye vituo 65 vya kuandikishia wapigakura.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa