Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako,
amefuta mfumo wa uwekaji matokeo wa ‘Grade Point Average (GPA)
ulioanza kutumiwa na Baraza la Taifa la Mitihani (NECTA) mwaka 2014.
Mfumo huo uliofuta mfumo uliokuwapo wa Divisheni, ulianza kutumika kwa kidato cha nne na sita na vyuo vya ualimu.
Inaelezwa kuwa mfumo huo ulianzishwa kujaribu kupandisha ufaulu
baada ya kuonekana wanafunzi wengi walishindwa mitihani ya kidato cha
nne, hasa mwaka 2013.
Mfumo huo ulilalamikiwa na wadau wa elimu waliodai kuwa ulikuwa unashusha kiwango cha elimu na kuwachanganya wanafunzi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dodoma jana, Profesa Ndalichako,
ambaye aliwahi kuwa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa
(NECTA), alisema baraza hilo limeshindwa kueleza sababu za kutumia mfumo
huo badala yake limeishia kutoa utaratibu uliotumika tu.
“Kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 20 cha Sheria ya Baraza
la Mitihani Tanzania, sura ya 107, naliagiza Baraza kufanya mapitio ya
mfumo unaotumika sasa wa wastani wa alama (GPA) kwa lengo la kurudi
kwenye mfumo wa awali wa Divisheni.
“Viwango vya ufaulu vizingatie azma ya nchi kuelekea kwenye uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda,” alisema Profesa Ndalichako.
Kuhusu mtihani wa pili (Paper two), aliitaka NECTA kuufuta kwa watahiniwa wa kujitegemea.
Mtihani huo ulianzishwa kama alama ya maendeleo wakati ni mtihani wa mwisho.
“Wizara haiwezi kufikia azma ya kusimamia ubora wa elimu katika ngazi
zote bila kuhakikisha viwango vya ufaulu vinawezesha kutoa wataalamu
wenye stadi na maarifa badala ya kuwa na wahitimu wengi wenye vyeti
lakini hawakidhi mahitaji ya soko la ajira,” alisema Profesa Ndalichako.
Januari 7 mwaka huu, Waziri Ndalichako alitembelea Necta na kuitaka
itoe ufafanuzi wa kuacha kutumia mfumo wa divisheni na kutumia GPA.
Pia aliitaka itoe maelezo ya kuanzishwa kwa mtihani wa pili kwa watahiniwa wa kujitegemea.
Hata hivyo alisema jana kuwa maelezo yaliyotolewa yalikuwa
yamejikita katika kueleza utaratibu badala ya sababu za kuutumia mfumo
huo.
“Taarifa imebainisha kuwa uanzishwaji wa mfumo wa GPA ulitokana na
maoni ya wadau bila kuwataja wadau husika na kueleza sababu walizotoa.
“Taarifa ya utafiti uliofanywea na Wizara ya Elimu haijataja idadi ya
wadau waliojaza madodoso na wala haionyeshi mikutano ya kupata maoni ya
wadau ilihusisha watu gani, ilifanyika wapi na lini,” alisema Profesa
Ndalichako.
Kuhusu sababu kuwa NECTA ilipata maelekezo kutoka wa Wizara ya Elimu
mwaka 2014, Profesa Ndalichako, alisema uchambuzi unaonyesha kuwa wizara
ilikuwa imeelekeza baraza la mitihani liandae mfumo huo na
kuuwasilisha kwa Kamishna wa Elimu upate kibali cha Serikali kabla ya
kuanza kutumika.
“Hata hivyo, jambo hilo halikufanyika na badala yake Baraza hilo
likaanza kutumia mfumo huo mwaka 2014. Nyaraka zilizowasilishwa
hazionyeshi kama mapendekezo ya mfumo huo yaliwasilishwa kwa Kamishna wa
Elimu,” alisema.
Alisema Baraza lilieleza faida ya kutumia GPA kuwa ni kueleweka kwake
kwa urahisi na wadau jambo ambalo linapingana na maoni ya wadau
yanayojitokeza kwenye vyombo vya habari, huku likishindwa kueleza
udhaifu wa mfumo wa Divisheni.
“NECTA wameeleza kuwa mfumo wa GPA umerahisisha udahili wa wanafunzi
wa vyuo vya elimu ya juu (Collective Admission System- CAS) jambo ambalo
si sahihi.
“Mfumo wa CAS ulianza kutumika Aprili 2010 wakati mfumo wa GPA
ulianza kutumika mwaka 2014. Isitoshe huzingatia masomo mawili ya fani
anayotarajia kusoma mwanafunzi siyo ufaulu wa jumla,” alisema.
Waziri alisema mfumo wa GPA ulikuwa bado kwenye majaribio hivyo haukupaswa kutumika kufanyia majaribio kwenye maisha ya watu.
Kuhusu sababu ya kuongeza mtihani wa pili kwa watahiniwa wa
kujitegemea kama mbadala wa upimaji endelevu, alisema maelezo ya NECTA
kuwa mtihani huo ni mbadala wa upimaji endelevu hayatekelezeki.
“Kitaalamu ‘paper two’ haiwezi kuwa alama ya maendeleo ya kila siku
kwa kuwa inafanyika sambamba na mitihani mingine ya mwisho,” alisema
Profesa Ndalichako.
Kwa sababu hiyo, Profesa Ndalichako, alisema kitendo cha baraza hilo
kuingiza mfumo huo wa GPA katika marekebisho ya kanuni zake
yaliyosainiwa na Waziri Oktoba 28 mwaka jana na kuchapishwa Novemba 6
mwaka jana kwenye gazeti la Serikali, ni kuonyesha kuwa mfumo huo
ulianza kutumika bila kukamilika matakwa ya sheria.
“Mfumo wa GPA ulianza kutumika mwaka mmoja kabla haujaingizwa kwenye kanuni za mitihani,” alisema.
Akizungumzia hasara ya mfumo huo, Waziri Ndalichako alisema baadhi ya
watahiniwa waliofaulu mitihani wanaonyesha kiwango kidogo cha maarifa
kuliko kiwango cha ufaulu.
Alisema kuwapo daraja E kwenye alama za ufaulu wakati haihesabiki
katika upangaji wa GPA kunawafanya watahiniwa waliopata E zote kwenye
mitihani kujiona wako bora kuliko wenye D mbili na F zote, ambaye
anahesabika kuwa amefaulu mtihani.
“Uwepo wa pointi za mfiko kwenye madaraja ya ufaulu kwa ngazi
mbalimbali za elimu kunaleta mkanganyiko kwani inakuwa vigumu kueleza
tafsiri ya madaraja hayo. Kwa mfano ‘Distinction’ ya kidato cha nne
inaanza pointi 3.6 wakati ya ualimu inaanzia pointi 4.4,” alisema Waziri
Ndalichako.
Pamoja na hatua hiyo aliyochukua, Profesa Ndalichako alisema bado Serikali haijaamua kuwachukualia hatua viongozi wa NECTA.
TAMONGSCO WAPONGEZA
Wakati huohuo, Chama cha Wamiliki wa Vyuo na Shule binafsi Tanzania
(TAMONGSCO) kimepongeza hatua ya Profesa Ndalichako kufuta mfumo huo na
kurejesha ule wa zamani wa Divisheni.
Katibu Mkuu wa Shrikisho hilo, Benjamin Nkonya aliliambia MTANZANIA
jana kwamba mfumo wa GPA ulishusha madaraja ya ufaulu na kusaidia
kusindikiza wanafunzi wengi zaidi kushindwa mitihani.
“Mfumo wa GPA ulikuwa mpango wa siasa, serikali iliona haijawekeza
katika shule zake kwa kuweka maabara bora, kulipa vizuri walimu, kuweka
mazingira mazuri hivyo kuchangia wanafunzi kufeli.
“Hivyo waliona wawadanganye wazazi kwa kuwaletea mfumo wasioujua huku wakitukwepa kutushirikisha wadau tukiwamo sisi.
“TAMONGSCO tunampongeza sana Waziri, Ndalichako na tunamshauri aweke
mifumo endelevu ya kuzuia udhaifu wa aina hiyo kuingizwa katika sekta ya
elimu katika siku za baadaye,” alisema Nkonya.
CHANZO: MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment