Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399
Serikali imetoa mapendekezo ya mwelekeo wa mpango wa pili wa miaka mitano wa maendeleo wa Taifa unaolenga zaidi kuinua sekta ya viwanda, kueleza vipaumbele 20, kikiwamo cha kununua ndege mbili za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Imesema fedha za kutekeleza mpango huo zitatokana na vyanzo vya mapato vya ndani na nje, ubia kati ya sekta ya umma na binafsi, uwekezaji wa sekta binafsi na mikopo nafuu kutoka taasisi za benki nchini.
Kabla ya kuwasilishwa kwa mapendekezo hayo, Serikali ilieleza changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya mpango uliopita na kusababisha utekelezaji ufanikiwe kwa asilimia 60.
Akiwasilisha mapendekezo hayo, Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi, Dk Ashatu Kijaji alitaja aina za viwanda vitakavyoanzishwa na Serikali, huku akisisitiza kuwa lengo ni kutimiza ahadi yake ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda.
“Tutakuwa na viwanda vya aina zote; vinavyotumia malighafi za ndani ya nchi vitakavyozalisha bidhaa zitakazotumiwa na watu wote, vinavyotumia teknolojia ya kati na viwanda vya Tehama,” alisema na kuongeza:
“Lengo ni kuimarisha usafiri na usafirishaji wa abiria na mizigo. Kwanza ni ununuzi wa meli za abiria na mizigo katika Ziwa Victoria (meli moja), Ziwa Tanganyika (meli moja) na Ziwa Nyasa (meli moja) na kukarabati meli zilizosimama.
“Ununuzi wa vivuko vipya vinne vya Kigongo (Busisi –Mwanza), Rugezi (Kisorya – Mwanza), Pangani (Bweni – Tanga) na Magogoni (Kigamboni – Dar es Salaam) na ukarabati wa vivuko vilivyosimama.”
Alisema Serikali imeazimia kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga ili kuongeza ufanisi wa viwanja vya ndege na upembuzi yakinifu na usanifu wa kina katika viwanja vipya vya ndege.
Alisema katika kutekeleza mpango huo wa miaka mitano, Serikali itaimarisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa, utawala bora, sekta ya madini, hali ya hewa, elimu na afya, kazi na ajira.
Hoja za wabunge
Mbunge wa Hai(Chadema), Freeman Mbowe aliibua suala la mkwamo wa kisiasa visiwani Zanzibar akisema nchi haiwezi kuwa na uchumi mzuri na kuendesha mipango yake ya maendeleo kama haina utawala bora.
“Yanayofanyika Zanzibar leo ya kutumia nguvu katika kujenga mustakabali wa nchi yetu, huku tunapanga mipango endelevu wa maendeleo tunajidanganya na kujichanganya,” alisema Mbowe.
Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda alisema mapendekezo hayo hayajaeleza lini Serikali itaanzisha viwanda na vitakuwa vya aina gani na kuhoji kama vitaanzishwa na sekta binafsi au Serikali yenyewe.
Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Kyerwa (CCM), Innocent Bilakatwe ambaye pia alihoji takwimu zilizotumiwa na Serikali katika kulinganisha mafanikio iliyoyapata katika mpango wa maendeleo uliopita.
“Ukitizama takwimu zilizotumika ni za mwaka 2012 hadi 2013 wakati leo ni mwaka 2016. Mlitumia vigezo gani kusema wananchi wanaopata maji ni asilimia 60 nchi nzima wakati jimboni kwangu Kyerwa na hata huko Dar es Salaam maji hakuna,” alisema.
Akijibu hoja za wabunge hao, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alisema Serikali itayafanyia kazi maoni yote ya wabunge hasa kuhusu takwimu, huku suala la Zanzibar akishauri liachwe litatuliwe na Wazanzibari wenyewe.
CHANZO ; MWANANCHI.
0 comments:
Post a Comment