Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI imesema uamuzi wa kurudia uchaguzi wa urais Zanzibar ni
halali na wa kisheria na kwamba wanaotafuta suluhu nje ya Katiba,
wanakosea. Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa jana na Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais Mazingira, January Makamba alipokuwa akihitimisha
majadiliano ya kuchangia hotuba ya Rais John Magufuli.
Alisema uchaguzi ulifutwa kisheria na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC)
kwa Tangazo la Serikali Namba 6587. Makamba alisema Katiba ya Zanzibar,
imeeleza wazi kuwa hakuna mamlaka ambayo itahoji uamuzi wa tume, hata
kama ni Mahakama. Alisema akidi ilitimia wakati tume inafikia hatua
hiyo.
Waziri huyo alisema wanaotaka kutumia suala hilo kuleta vurugu
Zanzibar, damu za Watanzania zitawalilia. Alisema viongozi wakuu wa
nchi, wamefanya kazi kubwa katika kulitafutia ufumbuzi suala hilo na
hivyo ieleweke kuwa ZEC na NEC ni tume zinazojitegemea.
Alisisitiza NEC haiwezi kuingilia uamuzi wa ZEC, kwani uchaguzi wa
rais uliofanyika kwa siku moja Tanzania Bara na Zanzibar, umekuwa
ukiendeshwa na Tume mbili tofauti. Alisema uchaguzi huo, ulifanywa na
tume tofauti na hata wino uliotumika katika chaguzi hizo ni tofauti .
Alisema wajibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni kuhakikisha kuwa amani
na utulivu, vinalindwa Zanzibar katika marudio ya uchaguzi unaotarajiwa
kufanyika Machi 20 mwaka huu. Oktoba 28 mwaka jana, Mwenyekiti wa ZEC,
Jecha Salim Jecha, alitoa “Taarifa Kwa Umma ya Kufuta Uchaguzi wa
Zanzibar”.
Katika taarifa hiyo, Jecha Salim Jecha alisema “Mimi nikiwa
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, nimeridhika kwamba uchaguzi
huu haukuwa wa haki na kuna ukiukwaji mkubwa wa sheria na taratibu za
uchaguzi. Hivyo, kwa uwezo nilionao natangaza rasmi kwamba uchaguzi huu
na matokeo yake yote yamefutwa na kwamba kuna haja ya kurudia uchaguzi
huu”.
CHANZO ; HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment