Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
VURUGU kubwa jana zimeibuka bungeni baada ya wabunge wa kambi ya
upinzani kuendelea kushikilia msimamo wao wa kutaka kauli ya Waziri wa
Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye kuhusu kutorushwa moja
kwa moja kwa matangazo ya Bunge ijadiliwe.
Mapema jana asubuhi Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge aliahirisha
kikao hicho baada ya kuona wabunge wa upinzani wakianzisha vurugu wakati
wakipinga kauli hiyo ya Serikali.
Vurugu hizo ziliibuka tena wakati Bunge liliporejea saa 10 alasiri
ambapo Mwenyekiti Chenge alikaa kimya kwa takriban dakika 10 hadi Mbunge
wa Singida Mashariki, Tundu Lissu alipoomba mwongozo wa mwenyekiti
kukaa kimya.
Chenge alisimama na kutoa taarifa ya Kamati ya Uongozi, akisema mambo matatu ndiyo yaliyoamuliwa.
“Kamati ya Uongozi imeamua mambo yafuatayo, kwanza Mwenyekiti alikuwa
sahihi kukataa kukatisha mjadala wa hotuba ya rais. Kuhusu kanuni ya
51, hakuna kanuni yoyote iliyovunjwa hasa ile ya Haki, Hadhi na Madaraka
ya Bunge,” alisema Chenge na kuongeza:
“Hoja iliyo mbele yetu yaani hotuba ya rais iendelee na endapo kuna
mbunge yeyote ambaye hataridhika na hatua hiyo, atumie kanuni ya nne
fasiri ya tano kuwasilisha malalamiko yake.”
Baada ya Chenge kutoa maelezo hayo na kumwalika mbunge aliyetakiwa
kuchangia, Lissu aliinuka na kuomba mwongozo akisema haikuwa sahihi kwa
mwenyekiti kupeleka tatizo hilo kwenye Kamati ya Uongozi badala ya
Kamati ya Kanuni.
“Ni sahihi kwa masuala ya kanuni kupelekwa kwenye Kamati ya Uongozi
badala ya Kamati ya Kanuni? Pili, kwanini mwenyekiti unakaimisha mamlaka
ya kiti chako kwenye Kamati ya Uongozi? Naomba mwongozo wako,” alisema
Lissu.
Akijibu mwongozo huo, Chenge alisema ametumia busara ya kawaida kumtaka Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe alete hoja yake.
“‘No any monopoly and I am very open’, someni kanuni,” alisema Chenge.
Baada ya hapo alimkaribisha katibu ili ataje utaratibu, naye akasema
ni kuendelea kwa mjadala. Lakini wabunge wa upinzani waliendelea kuomba
mwongozo.
Mbunge wa Babati Mjini, Paulina Gekul, alisimama na kuomba mwongozo jambo lililomkera Chenge, hata hivyo alimruhusu.
Gekul alitaja kanuni ya 49 akisema kauli za mawaziri hazipaswi kuzua mjadala.
“Kauli ya waziri imezua mjadala kwanini unatukataza kuijadili wakati kanuni zimeruhusu?” alihoji Gekul.
Naye Mbunge wa Tarime, John Heche, aliomba mwongozo na kusema kauli ya Waziri Nape imekwenda kinyume na Katiba ibara ya 18 (d).
“Tuko hapa kujadili mambo muhimu, wananchi wana haki ya kupata taarifa. Tutakuwa watu wa ajabu kuvunja Katiba,” alisema Heche.
Alipomaliza wabunge wote wa upinzani walisimama wakitaka mwongozo.
Chenge alijaribu kuwasihi wabunge hao wakae, lakini waligoma.
Aliwaambia kama hawajaridhika wafuate kanuni.
Wakati huo, baadhi ya wabunge wa CCM walikuwa wakipiga kelele, “toa nje haoooo”.
Chenge aliwaambia wabunge wa upinzani kuwa kama hawataki huo mjadala
watoke nje. Wakati huo pia mmoja wa wasaidizi wa Katibu wa Bunge alimpa
Chenge orodha ya majina aliyosema watoke nje.
Aliwataja wabunge hao kuwa ni Tundu Lissu, Esther Bulaya, Godbless Lema na Paulina Gekul. Lakini waligoma.
Lema aliinuka na kusema “Wataniua hapa siondoki,” huku wabunge wa
upinzani wakishangilia. Ndipo Chenge alipoagiza wabunge wote wa upinzani
watoke nje.
“Naahirisha shughuli za Bunge kwa dakika 10 ili polisi wafanye kazi yao,” alisema Chenge na kutoka nje ya Bunge.
Wakati huo, baadhi ya askari wa Bunge walifika na kuwasihi wabunge wa upinzani watoke nje nao wakagoma.
FFU WAWADHIBITI UKAWA.
Ghafla askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) waliingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kuwazunguka wabunge wa upinzani.
Askari hao walijaribu kila namna, lakini walishindwa kuwatoa.
Ilichukua takriban nusu saa kuwalazimisha wabunge hao kutoka nje. Mwishowe askari hao walianza kumtoa mmoja mmoja kwa nguvu.
Baadhi ya wabunge wakiwemo, Susan Kiwanga wa Kilombero na Halima Mdee wa Kawe waliburutwa kwa nguvu na askari hao.
WAANDISHI WANYANG’ANYWA SIMU, KAMERA
Wakati vurugu hizo zikiendelea, Mkuu wa Idara ya Habari na Uhusiano
bungeni, Owen Mwandumbya, akiwa na maofisa wenzake waliwaondoa waandishi
wa habari kwenye vyumba vyao na kuwapiga marufuku wapigapicha kuchukua
matukio yaliyokuwa yakiendelea bungeni.
Hata waandishi wa habari walipotoka nje, maofisa usalama waliwazuia
kuandika kitu chochote wala kupiga picha nje ya maeneo ya Bunge kabla ya
kuruhusiwa kuingia tena ndani, lakini hawakutakiwa kufanya kazi nje ya
Bunge na wengine wakinyang’anywa simu, kamera na vifaa vingine na
kutakiwa kufuta picha walizozipiga katika tukio hilo.
CHANZO; MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment