Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
RAIS John Magufuli ameridhia kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Songwe na
kuanzishwa kwa wilaya za Kibiti, Ubungo, Kigamboni, Malinyi na
Tanganyika. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), George
Simbachawene alitoa taarifa hiyo jana mjini hapa, kwenye mkutano na
waandishi wa habari.
Mkoa wa Songwe unaundwa na wilaya za Mbozi, Momba na Ileje. Kwa
upande wilaya mpya zilizoanzishwa mikoa yake kwenye mabano ni Kibiti
(Pwani), Ubungo na Kigamboni (Dar es Salaam), Malinyi (Morogoro) na
Tanganyika (Katavi).
Mchakato wa kuanzishwa kwa maeneo mapya ya utawala ulihitimishwa kwa
Tangazo la Serikali la Januari 29, mwaka huu. Waziri alisema Mkoa wa
Songwe uliomegwa kutoka Mbeya pamoja na wilaya hizo, zimeanzishwa kwa
mujibu wa sheria.
Aliagiza wakuu wa mikoa ambao katika mikoa yao imeanzishwa mkoa
pamoja na wilaya mpya, wafanye maandalizi muhimu kuwezesha kuanza rasmi.
Miongoni mwa mambo ambayo waziri amesisitiza yatiliwe mkazo ni
upatikanaji wa majengo ya ofisi na huduma muhimu kuweka mazingira ya
shughuli za kiutawala, kuanza kufanyika katika maeneo hayo ya kiutawala.
Waziri alifafanua Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka
1977, inampa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uwezo wa
kugawa nchi kwa kadri ambavyo ataona inafaa.
Alisema kwa kutumia madaraka hayo kikatiba, Rais wa Awamu ya Nne,
Jakaya Kikwete, Oktoba 18, mwaka jana alitangaza nia ya kugawa Mkoa wa
Mbeya na kuanzisha Songwe kwa Tangazo la Serikali Namba GN 461.
Alisema tarehe hiyo, rais alitoa tangazo namba GN 462 iliyokusudia
kuanzisha wilaya hizo. Tangazo hilo liliweka muda wa wananchi kutoa
maoni yao, ushauri na hata pingamizi. Alisema siku 30 zilizowekwa,
hakukuwa na pingamizi zozote.
Kuongezwa kwa Mkoa wa Songwe kunafanya idadi ya mikoa ya Tanzania
Bara kufikia 26. Mikoa mingine iliyoongezwa katika Serikali ya Awamu ya
Nne ni Geita, Katavi, Njombe na Simiyu. Awali, mikoa ya Tanzania Bara
ilikuwa 21 ambayo ni Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Kagera,
Kigoma, Kilimanjaro, Lindi, Manyara, Mara, Mbeya, Morogoro, Mtwara,
Mwanza, Pwani, Rukwa, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Tabora na Tanga.
Zanzibar ipo mikoa mitano ambayo ni Kaskazini Pemba, Kusini Pemba,
Mkoa wa Mjini, Mkoa wa Kusini Unguja na Mkoa wa Kaskazini Unguja. Wakati
huo huo, Waziri Simbachawene amesema wizara yake imeshatoa maelekezo
kuwa uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ufanyike Februari 8,
mwaka huu.
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment