*Bashe, Zitto wajiuzulu, wabunge wengine 22 wapanguliwa
NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai, amefanya mabadiliko ya baadhi ya wajumbe
wa Kamati za Kudumu za Bunge, huku akiwaondoa wenyeviti na makamu
wenyeviti watano katika kamati walizokuwa wakiziongoza.
Katika mabadiliko hayo yaliyowagusa jumla ya wabunge 27, Spika
Ndugai, ametoa maelekezo ya kujazwa kwa nafasi zilizoachwa wazi za
wenyeviti na makamu wenyeviti walioguswa na panga pangua hiyo na
kusititiza utekelezaji wa maagizo yake kuanza mara moja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Ofisi
ya Bunge, Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano ya Umma, uamuzi wa
Spika umezingatia mahitaji mapya na changamoto zilizojitokeza baada ya
kuundwa kwa Kamati za Bunge hapo Januari mwaka huu.
Taarifa hiyo ilieleza kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Spika ya kuteua
wabunge na kuunda kamati za Bunge, alizingatia kanuni ya 116 (3) ya
kanuni za Bunge kuwaondoa viongozi watano wa kamati na kwamba kamati
ambazo zitaathirika na uamuzi wake zitapaswa kufanya uchaguzi wa
viongozi walioondolewa kwa mujibu wa kanuni ya 116 (10).
Wenyeviti walioguswa la rungu la mabadiliko yaliyofanywa na Spika
Ndugai ni Mbunge wa Viti Maalumu, Martha Mlata (CCM) ambaye alikuwa
Mwenyekiti wa Kamati ya Nishati na Madini aliyehamishiwa Kamati ya
Viwanda, Biashara na Mazingira, Mbunge wa Sumve, Richard Ndassa (CCM),
ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uwekezaji na Mitaji (PIC),
aliyehamishiwa kamati ya Katiba na Sheria.
Mwingine ni Mbunge wa Viti Maalumu, Dk. Mary Mwanjelwa (CCM), ambaye
alikuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ambapo
amejikuta akihamishiwa Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira.
Makamu wenyeviti walioondolewa kwenye kamati zao ni Mbunge wa Busega,
Dk. Raphael Chegeni (CCM), ambaye alikuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati
ya Huduma na Maendeleo ya Jamii pamoja na Mbunge wa Mwibara, Kangi
Lugola (CCM), ambaye aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za
Serikali za Mitaa (LAAC).
Sambamba na hao, wabunge wengine 22 nao wamehamishwa kutoka kamati
walizokuwa kwenda kamati nyingine na taarifa za Bunge ambazo gazeti
hili limezipata zimeeleza kuwa mabadiliko hayo yamelenga kuwaondoa
waliokuwa wakilalamikiwa kuhusu mienendo yao ya kikazi kwenye kamati
walizokuwa huku wengine wakihamishwa kwa ajili ya kwenda kujenga taswira
mpya ya kamati zinazonyooshewa vidole.
Panga pangua hiyo ya Kamati za Bunge iliyofanywa na Spika Ndugai,
imekuja siku mbili baada ya gazeti hili kuwa la kwanza kuripoti kuhusu
tuhuma za ufisadi dhidi ya baadhi wabunge wakiwemo viongozi wa kamati
pamoja na uwezekano wa kuwepo kwa mabadiliko ya wajumbe na viongozi wa
kamati hizo yaliyofanyika jana.
Gazeti hili liliripoti kuwa ripoti ya uchunguzi wa mwenendo wa
wabunge iliyofikishwa mezani kwa Spika, iliwatuhumu viongozi wa kamati
ambao ni Mlata, Ndassa, Dk. Mwanjelwa, Dk. Chegeni na Lugola pamoja na
baadhi ya wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Kutokana na hali hiyo Spika Ndugai, alilazimika kufanya kikao na
wabunge hao ambapo pamoja na mambo mengine aliwaeleza jinsi majina yao
yanavyohusishwa na tuhuma hizo na kuwataka kuwafikishia ujumbe kwa
wajumbe wa kamati zao kwa kuwataka kujisahihisha kutokana na baadhi ya
wajumbe wa kamati hizo kudaiwa kutumia jina la Bunge vibaya.
Aidha, gazeti la MTANZANIA lilikariri taarifa za kibunge zilizoeleza
kuwa taasisi zilizofikiwa na wabunge wanaotuhumiwa kuombwa rushwa kuwa
ni Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco), Shirika la Nyumba la
Taifa (NHC), Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Hata hivyo, walipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizo, Mlata, Dk.
Mwanjelwa na Lugola walikanusha kuhusika nazo huku wakieleza kuwa
alichofanya Spika baada ya kuwaita ofisini kwake ni kuwapa maelekezo ya
kikazi na kuwatuma kufikisha ujumbe wa kujisahihisha kwa wajumbe wa
kamati zao.
Kwa upande wake Dk. Chegeni alisema hafahamu jambo lolote kuhusu
kashfa hiyo na kutilia shaka uwezekano wa kuwepo mkakati wa kuichafua
kamati yake.
Bashe, Zitto wajiuzulu
Muda mfupi baada ya Ofisi ya Bunge kutoa tangazo la kupanguliwa kwa
Kamati za Bunge, wabunge wawili ambao ni wajumbe wa Kamati ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM) na Zitto
Kabwe wa Kigoma Mjini (ACT – Wazalendo), walimwandikia barua Spika ya
kuomba kuachia ngazi kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa
kwenye kamati yao.
Katika barua yake ya Machi 22, mwaka huu Bashe alimwandikia Spika
akieleza kuwa kuna tuhuma nzito zilizochapishwa katika vyombo vya habari
zikieleza kuwepo kwa ufisadi katika kamati za Bunge jambo ambalo
linaweza kuharibu sifa ya kamati za Bunge, Bunge na wabunge binafsi
hivyo uchunguzi wa kina ufanyike na hatua kali zichukuliwe dhidi ya
watakaobanika kuhusika.
“Ninajiuzulu ujumbe wa kamati ninayohudumia sasa ili kupisha
uchunguzi. Bunge litaje wahusika hata nikiwa mimi ili kutunza heshima ya
kamati na taasisi. Ni vigumu kuhudumia wakati umma unaitizama kamati
kama corrupt, ili niweze kutimiza wajibu wangu ni vizuri kujiridhisha,
uhusika wa kamati na namna tulivyohusika,” ilisomeka sehemu ya barua
hiyo ya kujiuzulu ya Bashe.
Wakati Bashe akiandika hayo, Zitto katika barua yake ya Machi 22,
mwaka huu aliyoipa kichwa cha maneno ‘tuhuma za ufisadi dhidi ya Kamati
ya Huduma na Maendeleo ya Jamii,’ aliandika kuwa ameamua kujiuzulu
ujumbe wa kamati anayohudumia ili kupisha uchunguzi dhidi ya vitendo vya
ufisadi vya baadhi ya wabunge vilivyoripotiwa na gazeti la MTANZANIA.
“Tuhuma hizi ni nzito sana na zinaweza kuharibu kabisa sifa ya Bunge
na kamati zake, kwa vyovyote vile tuhuma hizi zimeharibu sifa ya wabunge
binafsi. Kwa barua hii naomba Bunge liagize uchunguzi wa kina na
kuchukua hatua kali dhidi ya yeyote atakayekutwa kahusika.
“Kumekuwa na tuhuma za mara kwa mara dhidi ya wabunge nyakati
tofauti. Kufanyika uchunguzi na kuchukua hatua ni chanzo cha mwendelezo
wa tuhuma za namna hii. Nashauri kuwa safari hii jambo hili lichukuliwe
kwa uzito unaostahili,” alisema Zitto katika barua yake kwenda kwa
Spika.
Kamati yagomea kazi
Katika mwendelezo huo wa kuachia ngazi, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti
wa Kamati ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Dk. Chegeni naye jana
aliwasilisha dokezo la kamati yake ofisini kwa Spika lililoeleza kuwa
kamati yake iliyokutana jana katika ukumbi wa Saadan uliopo Jengo la
LAPF, Kijitonyama baada ya kumaliza majukumu yake ya kibunge ilijadili
tuhuma za rushwa ilizoelekezewa.
Dokeza hilo lilieleza kusikitishwa na tuhuma hizo na kwamba wajumbe
waliazimia kulitaka Bunge kufanya uchunguzi wa tuhuma hizo na kwamba
kuanzia leo, wanasitisha kufanya kazi yoyote ya kamati hadi uchunguzi
utakapokamilika.
Kwa upande mwingine katika mitandao mbalimbali ya kijamii, mijadala
mikali kuhusu mienendo isiyoridhisha ya baadhi ya wabunge ilitawala.
Mjadala mzito
Mmoja wa wachangiaji katika mitandao hiyo aliandika kuwa taarifa za
baadhi ya wabunge kujihusisha na vitendo vya rushwa ni za muda mrefu na
kukumbushia kashfa ya aina hiyo iliyoibuliwa bungeni Juni 13, 2012
ikiwahusisha baadhi ya wabunge wa Bunge la 10 kushiriki vitendo hivyo
wakiwa katika shughuli za kamati huko Handeni mkoani Tanga.
Katika andishi lake hilo alieleza mwendelezo wa kashfa za rushwa
dhidi ya wabunge, wapo waliopata kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na kufikishwa mahakamini lakini hadi sasa
bado ni wabunge.
Mchangiaji huyo anaandika kushangaa jinsi Bunge linavyoshindwa
kufuata mila, desturi na utamaduni wa mabunge ya Jumuiya ya Madola
ambayo wabunge wake waliopata kukumbwa na kashfa za rushwa walivuliwa
nyadhfa zao na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.
“Kuna haja ya tatizo hili kulibeba serious kwa sababu kwa mujibu wa
kanuni za Bunge, Spika anafanya maamuzi kwa mujibu wa katiba, sheria,
kanuni, maamuzi ya maspika waliopita na uzoefu wa mabunge ya Jumuiya ya
Madola.
“Kwa uzoefu huo, mwaka 2005 India ilifukuza wabunge 11 kwa tuhuma za
rushwa na kuacha mahakama iendelee nao na kuanzia mwaka 1624 hadi sasa
Uingereza imekwishafukuza wabunge wengi sana,” aliandika mchangiaji
huyo.
Taarifa za TAKUKURU
Hata hivyo jana Taasisi za Kuzuia na Kupamba na Rushwa nchini
(Takukuru), ilimuhoji mmoja wa wenyeviti wa kamati kutokana na
kuhusishwa na tuhuma za rushwa.
Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilipomuuliza Mkurugenzi wa TAKUKURU,
Kamishna Valentino Mlowola, kuhusu taarifa hizo, alisema kwamba hawezi
kuzungumzia suala hilo na kutaka atumiwe maswali ambayo angeyajibu kwa
ufasaha.
“Swali hilo ninaomba niandikie maswali nitayajibu kwa ufasaha na kwa wakati,” alisema Kamishna Mlowola.
Chanzo Gazeti la Mtanzania
0 comments:
Post a Comment