Na.Aron Msigwa - MAELEZO, DODOMA
Serikali
imetangaza rasmi kuanza kwa kampeni ya kuwashughulikia na kuwaondoa
katika utumishi wa umma watumishi wote walioajiriwa katika sekta hiyo wakitumia vyeti bandia.
Aidha,
imewataka watumishi hao kuanza kujiondoa wenyewe kabla ya kufikiwa na
mabadiliko makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na utumishi wa umma
yanayokuja na kusisitiza kuwa wale wote waliotumia njia za udanganyifu kujinufaisha kwa maslahi yao binafsi kupitia sekta ya elimu mwisho wao umefika.
Kauli
hiyo imetolewa Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Elimu, Sayansi na
Mafunzo ya Ufundi Prof.Joyce Ndalichako wakati wa majumuisho ya
Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha
2016/2017.
Amesema
Serikali ya awamu ya tano imejipanga kufanya mabadiliko makubwa katika
Sekta ya Elimu nchini ili kuhakikisha kuwa Elimu inayotolewa katika
shule, vyuo na taasisi mbalimbali inazalisha wahitimu wenye sifa na
ubora kwa maslahi ya Taifa .
Amesema
katika kulitimiza hilo Serikali itawachukulia hatua kali za kinidhamu
na kisheria watendaji wote walioshiriki na wale wanaoendelea kushiriki
kwa namna moja au nyingine kukwamisha maendeleo ya elimu nchini ikiwa ni
pamoja na wale waliohusika katika udahili wa wanafunzi wasio na sifa
katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph Songea.
"Serikali
ya awamu ya tano imedhamilia kwa dhati kabisa kuboresha kiwango cha
elimu yetu kwa kufanya mabadiliko makubwa katika mfumo wa elimu, naomba
niwahakikishie kwamba pale panapohitajika kufanyika mabadiliko
tutayafanya bila woga" Amesisitiza.
Amesema
katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto mbalimbali za elimu hapa nchini,
serikali imejipanga kubadilisha mfumo wa elimu ambao umekuwa
ukilalamikiwa kwa muda mrefu na kwamba mabadiliko hayo yatafanyika kwa
kuwashirikisha wadau wote wa sekta hiyo.
" Tunapotaka kufanya mabadiliko kwenye mfumo wetu wa elimu tumekubali tumekubali kwamba tuna changamoto, katika
changamoto hizi lazima tuwe na mahali pa kuanzia hivyo tunapochukua
hatua tunaomba Watanzania mtuunge mkono" Amesisitiza Prof.Ndalichako.
Prof.Ndalichako
Amesema lengo la Serikali kupitia Wizara yake ni kuhakikisha sekta ya
elimu inaboreshwa hapa nchini kwa kuendelea kutoa wahitimu bora
wanaokidhi vigezo na viwango katika soko la ajira.
Amesisitiza
kuwa mkakati wa Serikali ni kuanza kuwafuatilia wahitimu wote wasio na
viwango ambao wako katika maeneo mbalimbali ya ajira huku akisisitiza
kwamba elimu ya Tanzania ni sawa na kiwanda kinahitaji malighafi nzuri
ili kitoe bidhaa bora.
Ameeleza
kuwa Serikali imejipanga kikamilifu kuvikagua vyuo vyote vinavyotoa
elimu ya juu kuona kama vinakidhi sifa na vigezo vya kiutendaji ili
hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa wale wote wanaowadanganya wananchi na kuwapotezea muda vijana wanaowadahili bila kuzingatia sifa.
"Wizara
yangu tunaendelea kufanya mawasiliano na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali ili tuchukue hatua kwa wote walioichezea sekta hii muhimu,
tulichofanya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph kinaendelea kwa vyuo
vingine"
Akizungumzia
suala la Ada elekezi amefafanua kuwa suala hilo linaendelea kutazamwa
kwa umakini mkubwa kwa kuwashirikisha wadau husika wa sekta hiyo kwa
kulifanyia utafiti kwa kuzingatia changamoto zinazojitokeza.
Ili
kukidhi matarajio ya wananchi kuhusu suala la ada elekezi amesema
serikali inaendelea kuchukua hatua kwa kulifanyia utafiti kuliangalia na
madaraja ya shule binafsi na kuongeza kuwa serikali itaendelea kutumia
taratibu zilizowekwa na Ofisi ya Kamishna wa Elimu nchini.
Amesema
Serikali kupitia Ofisi ya Kamishna wa Elimu inaendelea kulifuatilia kwa
karibu suala la ada na michango mingine kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa
mara ili kuona kama michango na ada zinazotozwa zinazingatia maslahi ya
Taifa.
Prof.
Ndalichako amebainisha kuwa ukaguzi utakaofanywa katika shule hizo
utajielekeza katika kuangalia uhalali wa michango inayotozwa kwa
wanafunzi ikiwemo michango ya kila muhula ya majengo, ulinzi na
mingineyo ambayo imekuwa kero kwa wananchi.
"
Kama Serikali hatuwezi kukubali wananchi kuendelea kutozwa michango ya
majengo wakati kigezo kimojawapo cha mtu kuruhusiwa kutoa elimu ni kuwa
na majengo, hili halikubaliki na hatutalifumbia macho" Amesisitiza Prof.Ndalichako.
Amewataka
wananchi kuelewa kwamba serikali kutotoa ada elekezi haina maana kwamba
imejitoa kabisa katika kufuatilia masuala ya elimu hapa nchini bali
itaendelea kujenga mazingira mazuri ya kuwawezesha watanzania kupata
elimu bora kwa gharama nafuu.
Kuhusu
ujenzi wa maabara amesema kuwa Serikali imetenga kiasi cha shilingi
Bilioni 12 kwa ajili ya kununulia vifaa vya maabara kwa shule zote 1536
ambazo zimekamilisha ujenzi wa majengo ya maabara kote nchini.
Katika
hatua nyingine amesema kuwa Serikali katika mwaka wa fedha wa 2016/2017
itafanya ukaguzi wa vyuo vyote vya Maendeleo ya Jamii kote nchini ili
majengo ya vyuo hivyo yaweze kutumika kuanzishia
vyuo vya Ufundi Stadi VETA katika wilaya na mikoa ili kuwapatia stadi za
kazi vijana waweze kujitegemea kwa kujiajiri wenyewe.
Kwa
upande wao baadhi ya Wabunge waliopata nafasi ya kuchangia wakati wa
Kupitisha Bajeti ya wizara hiyo wameiomba Serikali kuweka mkazo katika
usimamizi wa Sekta ya Elimu nchini ili shule, Taasisi na vyuo vya
Tanzania vitoe wahitimu wenye ubora kwa maslahi ya Taifa.
Aidha,
wameiomba Serikali kupitia Bajeti hiyo itenge fedha za kutosha kwa
ajili ya kuimarisha shughuli za ukaguzi wa shule, kuboresha maslahi na
kulipa madai ya walimu pamoja na kuziimarisha Mamlaka za Udhibiti wa
Elimu ili ziweze kutimiza majukumu yao ipasavyo.
0 comments:
Post a Comment