NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia
Wambura, ameagiza Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) kuhakikisha
nyumba zilizotelekezwa na shirika hilo kwa zaidi ya miaka 20
zinakarabatiwa haraka iwezekanavyo.
Akizungumza wakati wa kupata mrejesho wa maagizo aliyoyatoa kwenye
ziara yake ya kwanza ya kukagua mali za TBC, Aprili 9 mwaka huu, Wambura
alisema ni vyema kumalizia ujenzi wa nyumba hizo ambazo awali zilikuwa
ndani ya pori.
Katika ziara yake ya kwanza, Wambura aliitaka TBC kuhakikisha
inafanyia usafi eneo hilo ambalo lilikuwa pori na kushirikiana na
Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kuhakikisha wanapata hati ya kiwanja
hicho.
“Mimi sitakubali kuona rasilimali kama hii inapotea na kuharibika
bure wakati ni kodi za wananchi, sasa muamue kama mnataka kuendeleza
eneo hilo basi muliweke kwenye mpango wa kulitekeleza haraka sana,”
alisema.
Alisema andapo TBC itaona hawawezi kuliendeleza eneo hilo basi
walipeleke Halmashauri ili wananchi walitumie kama mabweni ya wanafunzi
kama ambavyo diwani wa kata ya Kisarawe alivyoomba.
“Ukiangalia ni majengo imara na uwekezaji wake unaonekana ulitumia
fedha nyingi, kwani kutokana na kuwa magofu kwa zaidi ya miaka 20,
lakini nyumba hizi (ziko hatua ya linta) hazina nyufa ingawa kuna nondo
zimeibiwa,” alisema.
Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa TBC, Joselin Lugola alisema uamuzi
wa kuendeleza eneo hilo au la litajadiliwa kwenye menejimenti.
“Tutalijadili kwenye manejimenti. Tunachofanya sasa ni kuwaomba
Wakala wa Majengo (TBA) kutufanyia tathimini ya gharama baada ya hapo
tutajua nini cha kufanya ili tuingize kwenye bajeti ya mwaka 2017/18,”
alisema.
Alisema TBC imekuwa ikiweka mipango ya kukarabati katika majengo
katika maeneo mengi, lakini inakwama kutokana na ufinyu wa bajeti huku
akisisitiza kuwa bajeti ijayo wamepanga kukarabati majengo ya Mwanza,
Arusha na Dodoma.
Kuhusu hati ya kiwanja chenye meta za mraba 9,567 kilipimwa na
kusajiliwa kwa namba 68,480 mwaka 2012, Wambura alipongeza hatua
iliyofikia ya kupelekwa maombi ya hati kwa Kamshina ya ardha kanda ya
Mashariki iliyopo Morogoro.
Awali, Ofisa Ardhi, Cheyo Nkelege alikiri ofisi yake kukosea kutoa
fomu iliyokuwa ina sehemu ya kusaini mtu mmoja badala ya watu wawili
kama inavyotakiwa kwenye fomu za taasisi au kampuni.
Fomu za awali zilikuwa na eneo moja la kusaini na zilisainiwa na
Meneja Rasilimali Watu, Neema Mrindoko ikiwa ni kinyume na taratibu za
fomu za umiliki wa ardhi wa taasisi au kampuni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kisarawe, Mwanamvua Mrindoko alisema
kwa kushirikiana na TBC wamerekebisha makosa ya awali na kuwa fomu hizo
zimeshapelekwa kwa kamishna wa ardhi. Alisema muda wowote shirika
litakabidhiwa hati ya umiliki wa kiwanja hicho.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment