SERIKALI imewaomba wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Taasisi ya
Sekta Binafsi (TPSF), wakawekeze katika kuujenga mji huo ili uendane na
hadhi ya makao makuu ya nchi.
Jana, Waziri wa Nchi Ofisi ya WAziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana
na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu Dodoma (CDA), Paskasi Muragili
walikutana na wafanyabiashara hao, ambako waliwaorodheshea fursa
mbalimbali, zinazopatikana Dodoma katika kipindi hiki, ambacho Serikali
imetangaza kuhamia huko.
Huduma ya maji
Katika mkutano huo, wafanyabiashara hao walielezwa kuwa Dodoma hakuna
shida ya maji, kwani kwa sasa zinazalishwa mita za ujazo milioni 65
kila siku na zinatozumika ni mita za ujazo milioni 40 tu; na hivyo
kuwepo na ziada ya mita za ujazo milioni 20.
Sekta ya umeme Kwa upande wa umeme, Muragili kuwa kituo cha Tanesco
cha Zuzu kinazalisha megawati 48 kwa siku na zinazotumika ni megawati 25
tu, hivyo kuwepo na ziada ya umeme ya megawati 23, “hivyo hofu ya
tatizo la maji na umeme halipo, njooni mjenge viwanda.”
Katika mkutano huo, Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF) iliazimia
kwamba inaunga mkono azimio la Rais John Magufuli la kuhamia Dodoma, na
wameahidi kuchangamkia fursa zilizoko katika mkoa huo. Lakini, pia
wameiomba Serikali kuweka vivutio mbalimbali kwa wale wote ambao
watakuwa tayari kuwekeza mkoani humo.
Mhagama katika maelezo yake kwa wafanyabiashara hao, alisema mchakato
wa kutunga sheria za kufanya Dodoma uwe makao makuu ya Serikali, uko
kwenye hatua za mwisho na lengo hasa ni kutaka kila jambo litakalofanywa
katika mji huo kusimamiwa na sheria moja.
Alisema sheria hiyo itaeleza vivutio vitakavyowekwa kwa wawekezaji,
watakaoenda kuwekeza katika mji huo. Pia alisema sheria hiyo itaweka
mfumo ambao sekta binafsi, itashirikiana na Serikali katika kuijenga
Dodoma.
“Nawaomba mchangamkie fursa hii katika kupanua wigo wa biashara yenu,
mimi niko tayari kushirikiana na nyinyi usiku na mchana; semeni
mmepanga nini, mnataka nini, sisi tupo tayari ili mradi msibaki nyuma
katika kuijenga Dodoma,” alisema Mhagama.
Alisema Watanzania wanatakiwa kumuunga mkono Rais Magufuli kuhamia
Dodoma kwa vitendo, na akaeleza kuwa ndani ya Serikali wanaendelea na
taratibu za kuhama, hivyo wafanyabiashara wanaweza kwenda sasa hivi kwa
ajili ya kuweka miunbombinu mbalimbali.
Waziri huyo alisema Serikali inapoenda kuhamia Dodoma kujenga makao
makuu ya nchi, inawahitaji sekta binafsi kwani serikali peke yake
haiwezi kujenga mji huo peke yake.
Alisema tayari ameiagiza CDA kuacha urasimu kwa wawekezaji, ambao wataonesha nia ya kuwekeza mkoani humo.
“Nimeagiza kama mfanyabiashara anahitaji kiwanja apewe ndani ya wiki
moja, kama unataka kujenga hoteli njoo upate kiwanja, lakini ukiendeleze
sio kikae miaka 20 bila kuendelezwa,” alisema na kusisitiza kuwa
Serikali inataka kuwepo na spidi kali inayoongozwa na uzale ndo katika
kuwekeza Dodoma.
Fursa zilizopo Dodoma
Awali, Muragili alitaja fursa mbalimbali zilizoko katika mji wa
Dodoma kuwa ni ujenzi wa nyumba za kupangisha kwa kuwa kutakuwa na idadi
kubwa ya watu ambao watahamia makao makuu ya nchi.
Alisema ujenzi wa majengo makubwa kwa ajili ya upatikanaji wa ofisi
nao unahitajika haraka kwa kuwa kwa sasa hakuna majengo hayo katika mji
huo.
“Hakuna majengo mengi ya ofisi yenye hadhi ambayo yanaendana na makao
makuu ya nchi, serikali haiwezi kujenga ni jukumu lenu nyinyi sekta
binafsi,” alisema.
Mkurugenzi huyo alitaja fursa nyingine kuwa ni ujenzi wa hoteli,
kwani kwa sasa Dodoma kuna hoteli nne tu ambazo zina hadhi ya nyota
tatu.
Alisema hakuna hoteli hata moja yenye hadhi ya hoteli tano ; na hivyo
akasema ni fursa kwa wafanyabiashara kwenda kujenga hoteli hizo zenye
hadhi, ziendanane na makao makuu ya nchi. Alisema mkoa pia hauna maghala
ya kuhifadhi vyakula, ambavyo vitaagizwa na wafanyabiashara kutoka nje
ya mkoa ili kutosheleza kuwalisha watu ambao wataongezeka katika mji
huo.
Alisema ujenzi wa maghala, unahitajika kwa pia. Kwenye kilimo, pia
alisema kunahitajika kilimo cha matunda kwa wingi kutokana na mkoa huo
kuwa na maji mengi. Alisema ujenzi wa viwanda pia ni fursa kubwa na
akatoa mfano ujenzi wa Kiwanda cha Bia ni wa muhimu mkoani humo kutokana
na mkoa huo kuwa maarufu kwa kilimo cha nafaka mbalimbali.
Ujenzi wa maeneo ya burudani yenye hadhi, pia yanahitajika pamoja na
viwanja vya michezo mbalimbali ili watu wakimaliza kufanya kazi wawe na
sehemu za kupumzika. Alisema kwa kuwa wenyeji wa Dodoma ni wafugaji,
kuna haja ya kujenga machinjio ya kisasa ambayo yatasaidia hata nchi
kusafirisha nyama nje ya nchi.
Akiongezea kutaja fursa hizo, Waziri Mhagama alisema kunahitajika
ujenzi wa shule za msingi na sekondari, ambazo alisema haziwezi kujengwa
na Serikali peke yake. “Njooni mjenge shule, ni fursa kubwa,”
alihimiza.
Pia alisema ujenzi wa majengo mbalimbali utakuwa mkubwa; hivyo
akawataka wafanyabiashara kufanya tathmini kama hapa nchini kuna nondo
ambazo zinatosheleza kuhimili ujenzi, unaoenda kufanyika katika mji huo.
Hiyo nayo ni fursa kubwa.
Alisema kwa kuwa idadi ya watu itaongezeka hadi kufikia watu milioni
moja, ni wazi kuwa kutakuwa na mahitaji makubwa ya mafuta, hivyo akataka
wafanyabiashara wajipange kuwekeza katika sekta ya mafuta.
TPSF wamsifu Dk Magufuli
Mwenyekiti wa TPSF, Dk Reginald Mengi alisema Rais Magufuli anatakiwa
kuungwa mkono kwa uamuzi mgumu alioufanya wa kuhamia Dodoma baada ya
miaka 40 tangu kuasisiwa kwa mpango huo na Serikali.
“Huyu ni Rais ambaye anatembea kwenye maneno yake, anafanya yale
anayoyasema, kutekeleza mpango huu ni jambo la ujasiri na amefanya
maamuzi magumu, sio jambo rahisi kutekeleza jambo ambalo limeshindikana
kwa miaka 40,” alisema.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara ni jukumu lao kuwa na macho yanayoona
fursa katika mkoa huo na wasisubiri kuhamasishwa na Serikali. Alisema
hiyo ni fursa ya kupanua biashara yao na wengine ni fursa ya kuanzisha
biashara mpya.
Katika maazimio yao, TPSF ilikubali kwenda kuwekeza mkoani humo, ila
wakataka kuwepo na kamati itakayoundwa kati ya Serikali na sekta binafsi
ili kuzungumza maeneo ya uwekezaji, ambayo yatafnaywa na sekta binafsi
na yale ambayo yatafanywa na serikali yenyewe.
Shule za Al Muntazir kutua Dodoma
Katika hatua nyingine, uongozi wa Shule za Al Muntazir za jijini Dar
es Salaam umesema utajenga shule zake mjini Dodoma katika kile
walichokiita kuunga mkono uamuzi huo wa Dk Magufuli.
Shule za Al Muntazir zinamilikiwa na Taasisi ya Kiislamu ya Khoja
Shia Ithnasheri Jamaat (KSIJ) na zinatoa elimu kwa watoto kuanzia umri
wa miaka mitatu hadi 18 kwa kutoa elimu katika ngazi za elimu ya awali,
elimu ya msingi, sekondari na sekondari ya juu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Khoja Shia Ithnasheri Jamaat, Azim Dewji,
wameitikia mwito wa Rais Magufuli wa serikali yake kuhamia Dodoma na
wao kama taasisi inayojihusisha na masuala ya kijamii ikiwamo elimu,
wameona ni vyema wakaanzisha shule mkoani Dodoma ili kusaidia jamii ya
huko.
“Tumeamua kuunga mkono uamuzi wa Rais John Magufuli wa kuhamishia
serikali mkoani Dodoma. Kama unavyojua taasisi yetu inamiliki shule za
Al Muntazir kwa hiyo, katika elimu tumekuwa na mchango mkubwa katika
maendeleo ya jamii nchini. Kwa msingi huo tumeona tunayo fursa ya
kusaidia kuwezesha Dodoma kuwa makao makuu ya nchi,” alisema Azim Dewji.
Alieleza kuwa katika kutekeleza azma hiyo, wiki hii uongozi wa Khoja
Shia Ithnaasheri Jamaat utakwenda mkoani Dodoma kuonana na Mkuu wa Mkoa
huo, Jordan Rugimbana kwa ajili ya kujadiliana naye kuhusu kupewa eneo
kwa ajili ya ujenzi wa shule hizo.
Aliongeza kuwa wanaamini katika muda mfupi watakamilisha ujenzi wa
shule hizo ili kutoa fursa kwa wakazi wa Dodoma na watumishi wa umma
ambao watakuwa wamehamia katika makao makuu ya nchi, kupeleka watoto wao
kupata elimu.
Shule hizo za Al Muntazir, zinafundisha kwa kufuata mitaala ya
kitaifa na ya kimataifa kupitia Cambridge International Schools na ni
shule pekee yenye cheti cha Taasisi ya Kimataifa ya Viwango (ISO) katika
ukanda huu.
Shule hizo zina wanafunzi zaidi ya 4,500 kila moja ikiwa na wanafunzi
zaidi ya 1,000. Pia shule hizo zimeajiri zaidi ya wafanyakazi 500
katika nafasi mbalimbali, ikiifanya Al Muntazir kuwa moja ya shule kubwa
katika ukanda huo.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment