WIZARA ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto itahamia Dodoma ndani ya siku 14 zijazo.
Waziri Ummy Mwalimu amesema tayari wizara yake imejiandaa kuhamia
Dodoma, kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la serikali kuhamia
Dodoma kabla ya 2020.
“Tutahamia Dodoma ndani ya muda wa wiki mbili,” alisema Ummy wakati
akifungua semina ya kitaifa ya afya mjini hapa juzi. Aliwatangazia wadau
wa afya nchini kwamba atatangaza kabla ya kuhamia Dodoma ni huduma gani
zitaendelea kutolewa Dar es Salaam na zile zitakazohamishiwa Dodoma.
Alithibitisha kwamba ofisi yake kama waziri, ya naibu waziri, na
Katibu Mkuu wake wa wizara, hazitabaki Dar es Salaam, bali zitakuwa
Dodoma.
Kuhamia kwa wizara hiyo Dodoma, itakuwa ni wizara ya tano, uhamisho
huyo ulitanguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyehamia Septemba
mwaka jana na baadaye akafuata Waziri wa Nchi katika ofisi yake, Jenista
Mhagama anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu.
Mawaziri wengine waliohamia Dodoma ni wa Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene na msaidizi wake,
Selemani Jafo pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Harrison
Mwakyembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa
Umma na Utawala Bora, Angellah Kairuki.
Kutokana na ratiba iliyotangazwa na Waziri Mkuu mwaka jana, waziri
mkuu na mawaziri wote pamoja na makatibu wakuu wa wizara, wanatakiwa
kuwa tayari wamehamia Dodoma kufikia Februari 28, mwaka huu.
Ratiba hiyo inaonesha kati ya Machi na Agosti mwaka huu, watendaji wa
wizara wanatakiwa kupanga na kutenga bajeti kwa maofisa wao kuhamia
makao makuu ya nchi.
Chanzo Gazeti la Habari leo
0 comments:
Post a Comment