Na. Lilian Lundo –
MAELEZO
Mratibu Elimu Kata
(MEK) ni mmoja kati ya kiungo kikubwa kati ya ofisi ya elimu ya wilaya na shule
za serikali katika ngazi ya kata ambaye ndiye mfuatiliaji mkubwa wa maendeleo
ya elimu ndani ya kata.
Shughuli nyingine
zinazofanywa na MEK ni pamoja na kufuatilia maendeleo ya taalamu ya wanafunzi
katika kata yake, kukagua ufundishaji wa walimu, kufuatilia mahudhurio ya
wanafunzi pamoja na kusimamia vikao mbalimbali vya shule zilizoko katika kata
yake.
Asilimia kubwa ya
Waratibu Elimu Kata walikuwa wanashindwa kufikia malengo ya kazi zao kutokana
na changamoto ya usafiri, ambapo wengi wao walikuwa wakitumia usafiri wa
baiskeli ambao ha
ukuwa
usafiri rafiki kutokana na kazi yao ya kukagua shule zote katika kata
wanazozisimamia.
Serikali kwa kuliona
hilo, kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (Education Quality
Improvement Programme -Tanzania) EQUIP-T
ilitoa pikipiki kwa kila MEK katika mikoa ya Dodoma, Kigoma, Lindi, Shinyanga,
Simiyu na Mara ili kurahisha ufuatiliaji wa mendeleo ya shule zao kwa urahisi.
Pikipiki hizo zimeleta
mafanikio makubwa kama vile kupungua kwa
idadi ya wanafunzi watoro, kiwango cha ufaulu kupanda kutokana na ukaguzi wa
mara kwa mara wa walimu pamoja na matatizo kutatuliwa kwa haraka kutokana na
taarifa za shule kufika wilayani kwa wakati.
Sweetbert Malimi ni Mratibu Elimu Kata
wa Sanzawa Wilaya ya Chemba, Mkoani Dodoma anasema kwamba Pikipiki imemuwezesha
kushughulikia kwa wakati matatizo yanayotokea katika shule anazozisimamia
tofauti na kipindi ambacho hakuwa na pikipiki.
Anaendelea kwa kusema kuwa, matatizo
yalipokuwa yakitokea katika shule anazosimamia yalikuwa yakimsubiri MEK hata
kwa mwezi mzima. Lakini sasa hivi imekuwa tofauti kutokana na kutembelea shule
zake hata mara mbili kwa wiki.
Vilevile ameweza kufuatilia kwa wakati
maendeleo ya taaluma ya wanafunzi pamoja na ufundishaji wa walimu ambapo kabla
ya kuwa na pikipiki kuna baadhi ya walimu walijisahau kutokana na kutokaguliwa
mara kwa mara.
Anaendelea kwa kusema kuwa, ufuatiliaji
huo umeletea mafanikio makubwa katika Mkoa wa Dodoma, ambapo ufaulu wa darasa
la saba kwa wilaya ya Chemba peke yake ulipanda kutoka asilimia 30 mwaka 2015
mpaka asilimia 46 mwaka 2016.
Kwa upande wake Mratibu Elimu Kata wa
Songambele iliyoko Wilaya ya Kongwa, Mkoani Dodoma amesema kuwa katika kata
yake ana shule Sita za kuzifuatilia ambapo kabla ya kupata pikipiki alikuwa
anatumia baiskeli kutembelea shule hizo na aliweza kutembelea shule hizo mara
moja kwa wiki.
Baada ya kupata pikipiki anauwezo wa
kutembelea shule hizo mara tatu hadi nne kwa wiki akifuatilia maandalio ya
walimu, maazimio ya kazi, utengenezaji wa zana za kufundishia, mahudhurio ya
wanafunzi pamoja na kuhudhuria vikao vya kamati ya shule.
Aidha amesema kuwa, kutokana na
ufuatiliaji huo wa mara kwa mara katika shule hizo kumepelekea umakini mkubwa
wa ufundishaji wa walimu kwa kufuata taratibu za ufundishaji kama vile kuwa na
maandalio, maazimio ya kazi pamoja na kuwa na zana za ufundishaji.
Pia amesema kwamba kwa kutumia pikipiki
aliyopewa amekuwa akiwatembelea wazazi ambao watoto wao ni watoro, na
kuwashauri juu ya umuhimu wa elimu kwa watoto wao na wazazi wenyewe. Juhudi
hizo zimepelekea wazazi wengi kubadilika na kushirikiana na walimu katika kufuatilia
mahudhurio na maendeleo ya taaluma ya watoto wao.
Nae, Mratibu Elimu Kata wa Kagera wilaya
ya Kigoma Manispaa, Mkoa wa Kigoma Jovitus Augustus anasema kuwa kabla ya kupewa
pikipiki kata yake ilikuwa na changamoto ya utoro kwa wanafunzi pamoja na
ufaulu duni wa wanafunzi wa darasa la saba.
“Pikipiki niliyopewa kupitia mpango w
EQUIP-T umeniwezesha kutengeneza mipango kazi ya wiki na kuisambaza katika
shule zote za kata pamoja na kufuatilia utekelezaji wake,” alifafanua Jovitus.
Aliendelea kwa kusema kuwa pikipiki hiyo
imemuwezesha kukagua utekelezaji na utoaji taaluma kwa kukagua maazimio ya kazi
na maandilio ya somo pamoja na kufanya vikao vya mara mara kwa mara na walimu
ili kupata maelezo ya walimu walioshindwa kutekeleza wajibu wao.
Aidha kupitia juhudi hizo zilizofanyika,
ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba shule za msingi za kagera na Mgumile
ulipanda pmoja na mahudhurio ya walimu
na wanafunzi katika kata hiyo umeongezeka .
Vilevile umeanzishwa utaratibu wa
mitihani ya kata kwa darasa la saba pamoja na kuweka kambi kwa wanafunzi
wanaojiandaa na mitihani wa darasa la Saba.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa Shule ya
Msingi ya Mazoezi Bunda iliko Halmashauri ya Mji Bunda Mkoa wa Mara, Mwalimu Vicent
Ndunguru, aliipongeza Serikali kupitia Mpango wa EQUIP-T kwa kutoa pikipiki kwa
Waratibu Elimu Kata ambao kwa kiasi kikubwa umewarahisishia utendaji kazi wao.
Amesema kuwa, kulikuwa na mambo mengi
ambayo yalikuwa hayaendi inavyotakiwa kutokana na MEK anayosimamia shule yake
kutotembea shule hiyo mara kwa mara kutokana na ukosefu wa usafiri wa uhakika.
Amesema kuwa, baada ya MEK huyo kupatiwa
pikipiki amekuwa akitembelea shuleni hapo mara kwa mara kufuatilia maendeleo ya
shule na kuchukua taarifa za shule na kuziwasilisha wilayani kwa wakati.
Mwalimu Ndunguru ambaye pia ni msaidizi
wa MEK katika kata ya Nyasura amesema kuwa, MEK huyo amekuwa akiitisha vikao
vya mara kwa mara kujadili maendeleo ya shule katika kata yake. Ambapo Shule ya
Msingi Mazoezi Bunda ndio eneo lilochaguliwa kwa ajili ya kufanyia mikutano
hiyo.
Aliendelea kwa kusema kuwa, MEK huyo
amekuwa chachu ya maendeleo ya shule zilizoko katika kata hiyo hasa baada ya
kuwa na uhakika na usafiri ambao kwa asilimia kubwa umemuwezesha kufanya kazi
zake kwa urahisi na hata kufikia malengo aliyowekewa na mwajiri wake na yale
aliyojiwekea yeye mwenyewe katika kuhakikisha ubora wa elimu uaongezeka siku
hadi siku kutoka ngazi ya kata mpaka Taifa.
Aidha Mwalimu Ndunguru, ameiomba
Serikali kuendeleza na utaratibu wa ugawaji wa pikipiki kwa Waratibu Elimu Kata
wa mikoa mingine iliyobaki ili na wao waweze kufanya kazi kwa ufanisi kama
ambavyo wenzao waliopewa pikipiki ambavyo wameweza kufanikiwa na hata
kupandisha kiwango cha ufaulu na kukomesha tatizo la utoro kwa wanafunzi.
Serikali kupitia mpango huo pia umetoa
vishikwambi kwa Waratibu Elimu Kata hao, ambao wamekuwa wakitumia vifaa hivyo
kwa ajili ya kupokea taarifa kutoka kwa walimu wakuu wa shule wanazozisimamia
na wao kuzituma taarifa hizo ofisi za elimu za wilaya.
Mpango wa EQUIP-T umetoa jumla ya pikipiki
1,000 kwa Waratibu Elimu Kata wa mikoa
ya Dodoma, Kigoma, Lindi, Shinyanga,
Simiyu, Shinyanga na Mara. Pikipiki hizo zilitolewa kati ya mwaka 2014 na 2015
ambapo mpango huo unawawezesha waratibu hao kupata fedha ya mafuta na
utengenezaji wa pikipiki hizo kila mwezi.
0 comments:
Post a Comment