Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma
Serikali
inatarajia kupiga marufuku utengenezaji na uingizaji wa pombe za bei
rahisi maarufu kama “Viroba” Nchini, ndani ya miezi mitatu ijayo.
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Hamisi
Kigwangalla ameyasema hayo leo Bungeni, Mjini Dodoma alipokuwa akijibu
hoja za wabunge waliokuwa wakilalamikia kilevi hicho
kinavyopunguza nguvu kazi ya Taifa, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa
za kamati ya kudumu ya Bunge ya masuala ya Ukimwi pamoja na Huduma na
Maendeleo ya Jamii kwa mwaka 2016/17.
Dkt.
Kigwangalla amesema kuwa baada ya miezi mitatu kilevi hicho kitapigwa
marufuku kutengenezwa au kuingizwa nchini pamoja na kuziba mianya yote
ya uingizaji wa kilevi hicho ambacho kimekuwa kikitumiwa na vijana
wengi, hivyo kuharibu nguvu kazi ya Taifa.
Kwa
upande wake Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Esther Matiko amesema
kwamba pombe hiyo inasababisha vifo vya vijana wengi nchini ambao ndio
tegemeo kubwa na nguvu kazi ya Taifa.
“Katika
kipindi hiki kifupi cha likizo yangu, nilikuwa jimboni kwangu na
tumezika vijana wanne ambao wamefariki kutokana na matumizi ya viroba.
Hivyo wananchi wa jimbo langu wameniagiza kuja kulieleza Bunge athari za
pombe hiyo ili tuweze kujadili na kuona namna gani ya kuliokoa Taifa hasa vijana kutoka katika janga hilo,” alifafanua Matiko.
Akiwasilisha
taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Dkt. Faustine
Ndugulile amesema kuwa Kamati imebaini uwepo wa uhusiano mkubwa kati ya
matumizi ya pombe hizo na kuongezeka kwa tabia hatarishi zinazochangia
ongezeko la vijana katika matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha
amesema kuwa hali hiyo inaathiri ufanisi wa nguvu kazi ya Taifa
kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya. Hivyo Kamati
imeishauri Serikali kufungia kabisa uzalishaji na uuzwaji wa pombe hizo
za viroba ili kulinusuru Taifa.
Mwisho…
0 comments:
Post a Comment