Na Benny Mwaipaja,WFM
Wadau
wanaofanya tafiti mbalimbali za Maendeleo ya uchumi nchini hasa maeneo
ya vijijini kuhusu Mabadiliko ya Tabia nchi wametakiwa kuwasilisha
matokeo ya tafiti hizo Serikalini na katika Mashirika mengine ya
Maendeleo ili matokeo yake yafanyiwe kazi na kusudio la tafiti hizo
liweze kufikiwa.
Rai
hiyo imetolewa Jijini Dar es salaam na Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi
wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo vijijini - Dodoma, Prof. Razack Lokina
wakati wa Mkutano uliohusu mabadiliko ya tabia nchi na athari zake
kiuchumi uliozihusisha Taasisi za Serikali na Binafsi pamoja na Washirika wa Maendeleo.
Amesema
Chuo cha Mipango kimekuwa kikifanya kazi zake vijijini, zikiwemo za
tafiti mbalimbali na matokeo hayo huwasilishwa katika ngazi husika
ikiwemo Ofisi ya Makamu wa Rais inayoshughulikia mazingira pamoja na
Wizara ya Maliasili na Utalii ili kutumia matokeo hayo kwa manufaa ya
maendeleo ya jamii hasa vijijini.
“Mkutano
wa Mabadiliko ya Tabia nchi ambao umejadili mbinu mbalimbali za
kukabiliana na athari za kiuchumi zinazotokana na Mabadiliko hayo,
umetokana na andiko la Wanafunzi wa Chuo hicho waliokwenda katika
mafunzo kwa vitendo vijijini na kushuhudia namna mabadiliko ya tabia
nchi yalivyoathiri maendeleo ya wananchi”. Alifafanua Prof. Lokina
Tayari Chuo kina mradi ujulikanao kama Chololo Ecovillage unaofadhiliwa
na Umoja wa Ulaya (EU) Mkoani Dodoma, ambao huwafundisha wanakijiji
njia bora za uzalishaji mali, hivyo kuwafanya baadhi ya Wananchi
waliokuwa wanakosa chakula, kutokana na hali ya Ukame wa Mkoa huo kuanza
kupata mazao ya kutosha na kuongeza pato lao.
Naye Mkuu wa Chuo hicho cha Mipango ya Maendeleo vijijini- Dodoma, Dkt. Frank Hawassi, amezitaka
Taasisi na Mashirika ya umma na Binafsi kuunganisha nguvu katika
kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia nchi kwa kuwa kama juhudi
hazitachukuliwa athari zake zitampata kila mmoja.
Aidha,
amesema hakuna nchi inayoweza kufanikiwa kukabiliana na tatizo hilo
bila kushirikiana hata kama nchi hiyo imeendelea kwa kiasi kikubwa. Pia
Jamii inapaswa kujua kuwa hata matatizo ya wafugaji, wakulima na wengine
kuhusu ardhi ni matokeo ya athari za Mabadiliko ya Tabia nchi, hivyo
kila mmoja anatakiwa kuwa chachu ya utunzaji wa mazingira, ili maendeleo yanayopatikana yawe endelevu.
Ameongeza
kuwa Chuo cha Mipango Dodoma kinatoa nafasi kwa wadau kote nchini
kukitumia kikamilifu katika kutatua changamoto za kimazingira kwa kuwa
ipo Idara iliyo na jukumu la kushughulikia suala la Mazingira na
Mabadiliko ya Tabia nchi.
Kwa upande wake aliyekuwa Balozi wa Umoja wa ulaya nchini Tanzania Tim
Clarke, ambaye ameongoza timu ya washirika wa Maendeleo katika Mkutano
huo ameitaka Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini kujitahidi
kuwahamasisha wananchi kutumia Nishati mbadala ikiwemo Gesi ili
kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu kwa kukata miti kwa ajili ya
kupata Mkaa.
Vilevile
ametoa rai kwa Serikali kuwa karibu na jamii na kuwaelimisha kuhusu
kutunza mazingira katika shughuli zao za kila siku za kujipatia kipato
ili kusaidia kulinda mazingira ya asili yatakayochochea kukua kwa uchumi
wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
0 comments:
Post a Comment