Na Mwandishi Wetu
Dodoma
MAAFISA
Habari na Mawasiliano Serikalini wametakiwa kutoa taarifa kwa haraka
zaidi kwa kutumia njia za kisasa za mawasiliano ikiwemo tovuti na
mitandao ya kijamii ili kusaidia kutangaza Mafanikio ya Serikali katika
maeneo yao ya kazi.
Hayo
yamesemwa jana Mkoani Dodoma na Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO)
na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, alipokuwa akizungumza
na maafisa habari na TEHAMA katika mafunzo elekezi ya uwekaji wa taarifa
katika tovuti yanayofadhiliwa na Shirika la Misaada la Marekani (USAID)
na kusimamiwa na Ofisi ya Rais- TAMISEMI na Wakala ya Serikali Mtandao
(EGA).
Dkt.
Abbas alisema kuwa mara baada ya tovuti kuzinduliwa rasmi, Maafisa
Habari wana wajibu wa kuweka taarifa mpya zinazozingatia muda na wakati
kwa kuwa malengo ya tovuti hizo ni kumsaidia mwananchi kuweza kupata
taarifa mbalimbali za Serikali.
“Tukifungua
tovuti hizi tunapaswa kuona taarifa mpya, kwa sasa suala la upashanaji
wa habari na taarifa za miradi ya Serikali isisubiri tena michakato,
isipokuwa kama kutatokea suala kubwa ambalo litahitaji ufafanuzi kutoka
katika ngazi za juu katika maeneo yenu ya kazi” alisema Dkt. Abbasi
Aliongeza
kuwa, taaluma ya habari katika zama za sasa inahitaji ubunifu mkubwa
katika kuisemea Serikali kwa kutafuta njia mbalimbali za kubaharisha
umma badala ya kutumia njia za kawaida na za kila siku.
“Katika
maeneo yetu ya kazi tuna vituo vya redio na televisheni ambazo
zinawahitaji Viongozi wetu kufanya nao mahojiano maalum kuhusu masuala
mbalimbali ya Serikali, ni wajibu wetu kutumia fursa hizo kuhakikisha
tunaisemea Serikali” alisema Dkt. Abbasi.
Kwa
mujibu wa Dkt. Abbasi alisema Serikali itaweka utaratibu maalum wa
kupima utendaji kazi wa kila Afisa Habari katika Wizara, Idara, Taasisi,
Wakala na Mamlaka za Mikoa na Wilaya na Mikoa ili kuona ni namna gani
ameweza kutoa taarifa za Serikali kuhusu masuala mbalimbali ya Serikali.
“Katika
kipindi hiki Serikali ya Awamu ya tano imetekeleza na inatekeleza
miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo miradi ya umeme vijijini (REA), na
ujenzi wa miundombinu mingine kwa kutumia fedha nyingi katika kutekeleza
miradi hiyo, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kueleza wananchi
utekelezaji wa miradi hiyo” alisema Dkt. Abbasi.
Alisema
kuwa ili taarifa hizo za utekelezaji wa mafanikio hayo ya Serikali
ziweze kuwafikia wananchi, ni wajibu wa Maafisa Habari na Mawasiliano
kujenga na kuimarisha mtandao wa mawasiliano baina yao pamoja na
watendaji wengine katika maeneo yao ya kazi.
Aliongeza
kuwa ubunifu ni siri nyingine ya mafanikio katika suala la upashanaji
wa taarifa za Serikali, hivyo ni wajibu wa Maafisa Habari kuwa mbunifu
badala ya kulalamika kutokana na changamoto mbalimbali zinazomkabili
katika maeneo yao ya kazi ikiwemo ufinyu wa bajeti na changamoto ya
ukosefu wa vitendea kazi.
Mafunzo
hayo ya wiki moja yalishirikisha mikoa na Halmashauri za Mikoa ya
Arusha, Manyara, Singida, Dar es salaam, Pwani na Dodoma.
0 comments:
Post a Comment