Na Eleuteri Mangi
Maafisa
Mawasiliano Serikalini wametakiwa kuendelea kuitendea haki taaluma yao
kwa kuhabarisha na kuisemea Serikali juu ya utoaji huduma za jamii na
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Hayo
yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Prof. Elisante Ole Gabriel kwa niaba ya Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
Mhandisi John Kijazi wakati wa kufunga Kikao Kazi cha mwaka cha Maafisa
Mawasiliano Serikalini mjini Dodoma.
“Mtaheshimika
kwa kuiambia jamii na kuwapa taarifa kwa wakati. Nguvu ya habari ni
kubwa, muitumie vizuri kwa kuongeza thamani ya kazi zenu na wafikisheni
viongozi wenu kwenye mafanikio ya malengo yaliyowekwa ambapo uwepo wenu
utasaidia kwa mchango wako wa kuwa mbunifu katika kutekeleza majukumu
yako” alisema Prof. Ole Gabriel.
Prof.
Ole Gabriel aliwahimiza Maafisa hao kushirikiana na vyombo vya habari
katika kutoa habari kwa manufaa ya Watanzania kwa kuzingatia Sheria za
nchi ikiwemo Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 na kanuni zake.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) ambaye pia ni
Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa ili Vitengo vya
Mawasiliano Serikalini viweze kuuhabarisha Umma kwa wakati ni lazima
kuwe na mawasiliano ya kimkakati ambayo yatasaidia kuisemea Serikali kwa
wananchi wake katika mambo mbalimbali yanayotekelezwa na Serikali yao.
Dkt.
Abbasi aliongeza kuwa ili kufikisha taarifa kwa umma kwa wakati zipo
njia kuu ambazo zinaweza kusaidia kufikia malengo ya mawasiliano ya
kimkakati katika kuhabarisha umma ikiwemo kuweka malengo makubwa.
“Rais
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alipoweka
lengo la ununuzi wa Ndege ilionekana inawezekana vipi? Matokeo yake
ndege mpya aina ya Bombardier zipo na zinafanya kazi nchini,haya ni
matokeo ya malengo makubwa aliyojiwekea, nasi tufanye hivyo katika
tasnia ya habari” alisema Dkt. Abbasi.
Awali
akimkaribisha Mgeni Rasmi kufunga kikao kazi hicho, Mwenyekiti wa
Mkutano huo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Nuru Millao aliwataka Maafisa Mawasiliano kuandika
habari na makala za miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na
Serikali pamoja na kufuatilia na kujibu ya hoja na kero za wananchi kwa
wakati kwa kushirikiana na Idara ya Habari (MAELEZO) ambayo ndiyo
kiunganishi cha Vitengo vya Mawasiliano Serikalini nchini.
Naye
Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano ya Serikalini (TAGCO)
Paschal Shelutete amemuahidi Mgeni Rasmi kwa niaba ya Washiriki wa
Mkutano huo kuwa watayafanyia kazi maagizo yaliyotolewa pamoja na
maazimio yaliyofikiwa katika mkutano huo na kufanya kazi kwa weledi na kwa wakati ili kuhakikisha kazi za Serikali zinafahamika kwa Umma wa Watanzania.
Mkutano
huo ulihudhuriwa na jumla ya washiriki wapatao 231 kutoka Wizara
mbalimbali, Idara za Serikali, Taasisi, Wakala, Miji, Majiji, Mikoa na
Halmashauri mbalimbali nchini.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment