Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Maafisa
Mawasiliano Serikalini wametakiwa kutumia tovuti za ofisi na tovuti kuu
ya Serikali kwa kuweka taarifa mbalimbali zinazohusu huduma na bidhaa
zinazotolewa na taasisi hizo ili kuwawezesha wananchi kuzifahamu huduma
hizo kirahisi.
Rai
hiyo imetolewa leo Mkoani Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Serikali
Mtandao (EGA), Dkt. Jabir Bakari alipokuwa akitoa semina juu ya
matumizi na umuhimu wa tovuti za Serikali katika kikao kazi cha Maafisa
Mawasiliano Serikalini kinachoendelea Mkoani humo.
Dkt. Bakari amesema dhana ya Serikali Mtandao ni kuhuisha
matumizi ya TEHAMA kwenye utoaji wa taarifa mbalimbali za Serikali kwa
wananchi hivyo ni muhimu kwa kila taasisi kuwa na tovuti zenye taarifa
za uhakika na zinazoendana na wakati ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo.
“Wakala
kwa kushirikiana na TAMISEMI pamoja na Wizara ya Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo tumetengeneza mfumo unaotumia muda mfupi kwa taasisi za
Serikali kutengeneza tovuti zao ili ifikapo Juni mwaka huu taasisi zote
ziwe na tovuti zao zitakazowarahisisha wananchi kufahamu huduma
kirahisi,”alisema Dkt.Bakari.
Mtendaji
Mkuu huyo ameongeza kuwa tovuti za taasisi zisitumike tu katika kutoa
taarifa za huduma na bidhaa zao bali zitumike kuelezea mambo mengine
muhimu yanayofanywa na taasisi hizo.
Akielezea
kuhusu tovuti kuu ya Serikali, Dkt. Bakari amesema ni muhimu
kuhakikisha taarifa muhimu na za kudumu za taasisi husika zinawekwa ili
kusaidia wananchi kufahamu kiundani kazi wanazozifanya.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Maafisa Mawasiliano (TAGCO),
Bw.Innocent Mungy amesema mbali na kuweka taarifa katika tovuti za
Serikali, ni wajibu wa Maafisa Mawasiliano Serikalini kutumia mitandao
ya kijamii kufikisha taarifa muhimu kwa wananchi .
“Kutokana
na maendeleo ya teknolojia duniani hasa katika upande wa mawasiliano,
matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa yakileta tija kwa taasisi za
Umma kwani yanasaidia Serikali kujibu haraka hoja zinazowasumbua
wananchi”alisema Mungy.
Pia
aliwataka Maafisa Mawasiliano kuwa wabunifu katika kutumia mitandao ya
kijamii kwani mitandao hiyo inatoa fursa ya kushirikiana, kutangaza
huduma na bidhaa za taasisi, kufahamu matatizo ya wananchi.
0 comments:
Post a Comment