Hussein Makame, NEC
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa wito kwa wananchi
walioko kwenye halmashauri mbalimbali nchini, kuitumia vyema fursa ya utoaji wa
elimu ya mpiga kura kupitia redio za kijamii kwenye halmashauri zao ili kuondoa
manung’uniko kwenye chaguzi.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume
hiyo Bw. Kailima Ramadhani wakati akizungumzia mpango wa kutoa elimu ya mpiga
kura nchi nzima ulioanza kutekelezwa Mei 8 mwaka huu hii katika mikoa kumi nchini.
Alisema kupitia mpango huo wananchi wanaosikiliza redio za
kijamii kwenye halmashauri nchini, watapata fursa ya kujifunza elimu ya mpiga
kura na kuelewa masuala yote muhimu yanayohusu mfumo mzima wa kupiga kura.
“Tumepanga mpango, Tume itasambaa nchi nzima kuzungumzia
elimu ya mpiga kura kwenye redio za kijamii zilizoko kwenye halmashauri zote za
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.” alisema Bw. Kailima.
Alisisitiza kwa kutoa wito kwa wananchi walioko maeneo ambayo
Tume itakwenda kutoa elimu ya mpiga kura, wasikilize na kuuliza maswali ili
waweze kuelewa.
“Hii ni fursa kwa
wananchi ambayo muda mrefu hawajawahi kuipata, hivyo nawaomba wafuatilie ili
waweze kuelimika zaidi ili yale manung’uniko ya kura yatakuwa yamekwisha na
tutakuwa na uchaguzi mzuri zaidi ya ile ambayo tumeifanya.” Alifafanua Bw.
Kailima.
Utekelezaji wa mpango huo umegawanyika katika makundi
matatu ambapo kundi la kwanza limeanza kutoa elimu hiyo elimu hiyo kwenye mikoa
ya Kagera,Mwanza, Kilimanjaro, Morogoro, Mbeya na Dodoma.
Mikoa mingine itakayojumuishwa kwenye kundi hilo ni
Ruvuma, Mara, Pwani na Mtwara ambapo elimu hiyo itatolewa kuanzia tarehe 8 Mei
hadi tarehe 20 Mei mwaka 2017.
Kundi la pili linatarajiwa kutoa elimu hiyo kuanzia tarehe
24 Mei hadi tarehe 7 Juni mwaka huu katika mikoa ya Geita, Tanga, Singida, Shinyanga,
Lindi, Arusha, Tabora, Kigoma, Iringa, Manyara, Rukwa, Katavi, Songwe, Njombe
na Simiyu.
Bw. Kailima alisema kuwa utoaji wa elimu hiyo utajikita
kwenye mada kuu ya Elimu ya Mpiga Kura iliyogawanywa kwenye vipindi vitano,
itakaytoolewa kwenye redio hizo kulingana mada husika na wananchi kuuliza
maswali na kujibiwa na wawasilishaji wa mada hizo kutoka Tume.
“Ni mada ambayo imejumuisha masuala yote muhumu yatakayofanya
mpiga kura yeyote au mdau yeyote wa uchaguzi kuisoma au kuisikiliza na akaelewa
mfumo mzima wa masuala ya kupiga kura” alisema.
Mbali na kutoa elimu ya mpiga kura kupitia vituo vya
redio za kijamii katika halmashauri nchi nzima, Tume pia inatoa elimu hiyo kwa
njia ya magazeti na vyombo vingine vya habari
na mitandao ya kijamii, kushiriki kwenye mikutano na maonesho mbalimbali
nchini.
Mwisho
0 comments:
Post a Comment