Na. Eliphace Marwa
MAELEZO
29.5.2017
SERIKALI imesema
kuwa Tanzania bado haijafikiwa na ugonjwa hatari wa Ebola na kuwatoa
hofu wananchi baada ya mlipuko wa ugonjwa huo kuikumba nchi jirani ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amewataka
wananchi kutokuwa na hofu bali wachukue tahadhari za kujikinga na
ugonjwa huo, kwani hadi sasa hakuna mtu aliyethibitishwa kuugua ugonjwa
huo hapa nchini.
Waziri
Ummy amewataka wananchi hususani wanaoishi mikoa ya karibu na nchi ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ikiwemo mikoa ya Mwanza, Kagera,
Kigoma, Rukwa, Katavi na Songwe wanapaswa kuwa makini kwani tayari
mlipuko wa ugonjwa wa Ebola umethibitishwa DRC.
“Mpaka sasa Jamhuri
ya Kidemokrasia ya Congo imethibitika kuwa na wagonjwa 43 na wagonjwa
wanne wamekwisha poteza maisha hadi sasa,” alisema Waziri Ummy.
Mbali
na hayo Waziri Ummy amesema kuwa Wizara itahakikisha inashirikiana na
wadau mbalimbali wa afya ili kupata mbinu za kudhibiti ugonjwa huo
usiingie nchini.
“Kupitia
wataalam wa afya waliopo katika mipaka ya nchi serikali itakuwa ikitoa
taarifa za mara kwa mara ya namna uzuiaji wa ugonjwa huo kwa wananchi na
wanapata elimu ya kutosha ya kujikinga na virusi vya Ebola”, alisema
Waziri Ummy.
Waziri
Ummy aliongeza kuwa wananchi wanashauriwa kutoa taarifa pamoja na
kupata elimu kuhusu ugonjwa wa Ebola kwa kupiga simu namba 117 na kupata
huduma bila ya malipo kwa mitandao yote.
Aliongeza
kuwa Serikali imeendelea kutoa mafunzo kwa wataalamu wake walioko
mipakani ikiwa ni pamoja na utoaji wa vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo
pamoja na vidonge kwa wataalamu hao walioko mipakani.
“Serikali
tayari imeagiza mashine nne kwa ajili ya kufanya vipimo katika mipaka
yetu pamoja na viwanja vya ndege na bandari zetu na tutahakikisha kila
mgeni anayewasili nchini kutokea Congo anasajiliwa,” alisema Waziri
Ummy.
Ugonjwa
wa Ebola unasababishwa na kugusa majimaji yanayotoka kwa mgonjwa mwenye
virusi vya Ebola na mizoga na dalili za ugonjwa huu zinatokea baada ya
siku mbili pindi mgonjwa anapopata maambukizi ya ugonjwa huo zikiwemo
kutokwa na damu sehemu za puani, masikioni na homa kali.
0 comments:
Post a Comment