Na Benny Mwaipaja, WFM-Dodoma
Serikali
imeeleza kuwa inajitahidi kuboresha miundombinu kama vile teknolojia ya
Mawasiliano, Barabara, Ulinzi, Maji na Umeme katika maeneo ya vijijini
ili kuweka mazingira bora yatakayovutia wawekezaji kutoka sekta binafsi
kuwekeza katika sekta ya fedha ili kupanua huduma hiyo katika maeneo ya
mijini na vijijini.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti
Maalum Mhe. Josephine Chagulla (CCM), aliyetaka kujua mpango wa
Serikali wa kuwapa wanawake elimu kuhusu mikopo pamoja na kufikisha
huduma za kibenki maeneo ya vijijini ili waweze kufikiwa na huduma za
kifedha.
Mhe.
Josephine Chagulla ameeleza kuwa wanawake wengi wa vijijini
hawakopesheki kwa sababu benki haziwafikii, pia hawana mafunzo maalumu
ya kuwasaidia ujuzi wa namna ya kuzifikia huduma hiyo ya kukopeshwa
Akijibu
swali hilo Dkt. Kijaji alisema kuwa, elimu ya fedha inahusisha wadau
mbalimbali ikiwemo Serikali na Taasisi zake, ambapo kwa upande wa
Serikali, Benki Kuu inaratibu uanzishwaji wa taasisi ya kitaifa
itakayokuwa na jukumu la kuratibu, kuwezesha na kusimamia utoaji wa
elimu ya fedha kwa jamii.
“Serikali
kupitia Benki Kuu imetoa mwongozo wa Uwakala wa Huduma za Kibenki ili
kupanua wigo wa huduma za kibenki kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi
na kwa gharama nafuu hasa katika maeneo ya vijijini”. Alisema Dkt.
Kijaji.
Alisema
kuwa baada ya kuunda taasisi ya kitaifa ya Uratibu wa Elimu ya Fedha,
kutakuwepo na mfumo rasmi nchini wa utoaji wa elimu ya masuala ya fedha
kwa wananchi wote wakiwemo akina mama wa vijijini.” Alisema Dkt. Kijaji.
Dkt.
Kijaji alifafanua kuwa, Taasisi za fedha zina utaratibu wa kutoa elimu
ya fedha kwa wateja wao wakiwemo wanawake ili kuhakikisha kwamba wateja wao wanaendesha biashara zao kwa ufanisi.
“Serikali
inatambua umuhimu wa wananchi kupata huduma za kibenki karibu na maeneo
yao, pia inatambua umuhimu wa taasisi hizo katika kuwasaidia wananchi
kujikwamua kiuchumi.” Alieleza Dkt. Kijaji.
Aidha,
Dkt. Kijaji aliongeza kuwa Serikali inatambua benki nyingi zinaendesha
shughuli zake mijini kwa sababu ya urahisi wa upatikanaji wa miundombinu
muhimu kwa ajili ya uendeshaji wa shughuli za kibenki.
Katika
swali la nyongeza Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Josephine Chagulla (CCM),
alitaka kujua mpango Serikali wa kufungua matawi ya benki ya Wanawake
katika mikoa yote ya Tanzania ili kuwasaidia wanawake kupata mikopo kwa
urahisi.
Swali
hilo lilijibiwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe. Ummy Mwalimu, ambaye aliahidi kuwasiliana na Wizara ya
Fedha na Mipango ili itimize ahadi iliyotolewa na Rais wa Awamu ya Nne
Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete ya kuipatia mtaji Benki ya Wanawake Tanzania
ili iweze kufungua matawi nchi nzima na kutoa mikopo yenye masharti
nafuu ikilinganishwa na benki nyingine.
0 comments:
Post a Comment